Kiswahili sanifu na lahaja ya Kipemba

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, April 18  2017 at  12:06

Kwa Mukhtasari

KWA muda mrefu, dhana ya Kiswahili Sanifu imejadiliwa sana na katika kazi mbalimbali za Fasihi ya Kiswahili – fikra ya kwamba fasihi inayostahiki kusomwa miongoni mwa watu wetu wa Afrika Mashariki nzima ni ile inayoandikwa kwa Kiswahili Sanifu.

 

Jambo hili linasisitizwa mno hata baadhi yetu huwa tunashindwa kuelezea kwa ufasaha Kiswahili Sanifu ni kipi. Je, ni Kiswahili chenye msingi wa lahaja ya Kiunguja? Au ni Kiswahili cha lahaja ya Mrima, Tanzania Bara?

Au ni lugha dhahania iliyotengenezwa makusudi na wakoloni kwa madhumuni ya kufanikisha sajili ya elimu, hasa kimaandishi?

Kama kweli msingi wa Kiswahili Sanifu mmojawapo miongoni mwa yote hii ulikuwepo tokea mwanzo, je, bado msingi huo unafuatwa mpaka leo kama kigezo cha Kiswahili kinachotumiwa katika shughuli rasmi na kueleweka na watu wote?

Tukipeleleza sana, na tukiacha siasa ya nchi kwa nchi au eneo kwa eneo, tunataona kwamba hakuna Kiswahili Sanifu kinachotawala janibu zote za Afrika ya Mashariki namna hiyo.

Kile kilichopo ni misingi fulani tu ya Kiswahili Sanifu inayoishia pahala fulani, na mbele ya hapo, kuna kuingiza maneno na hata sarufi ya viswahili vya maeneo mbalimbali, na wakati mwingine, hata misamiati na sarufi za lugha nyingine za Kibantu.

Mimi binafsi silalamiki hata kidogo kuwepo mchango wa lahaja mbalimbali za Kiswahili au hata wa lugha za Kibantu za Afrika ya Mashariki.

Siwezi kulalamika kwa jambo hilo, kwa sababu Kiswahili Sanifu kama kilivyo hakina upana wa kumpa mwandishi, hasa wa fasihi, kuweza kujifaragua apendavyo kwa mapana na marefu.

Kwa hivyo kuingiza maneno, misemo, na mipangilio ya kisintaksia katika misingi ya Kiswahili sanifu kutokana na lahaja zake au hata kutokana na lugha za Kibantu, kutakipanua na kukikuza Kiswahili Sanifu.

Kwa hivyo, Kiswahili Sanifu lazima kikubali kubwia utajiri wa msamiati na ukunjufu wa kisarufi unaotokana na majilio mengine.

Watu wanaoshughulika na elimu na mitaala ya masomo ya Kiswahili, pamoja na watoa vitabu wetu wa Afrika ya Mashariki, lazima wasaidie jambo hili, badala ya kudai mihuri rasmi ya kuingizwa vitabu shuleni.

Hapa, sharti ifahamike vizuri, hatusisitizi kuwepo uovyo na vurugu katika Kiswahili Sanifu, bali lazima kuwepo taratibu na mifumo maalumu ya ukubalifu wa uingizaji maneno na mipangilio yake na viwango mbalimbali vya matumizi ya baadhi ya maneno yanayotokana na Kimrima, Kiamu, Kimvita, Kimtang’ata, Kipemba. Kipate na hata Kikikuyu, Kihaya, Kikamba, Kikerewe na kadhalika.

Ni wazi kwamba upanuzi wa Kiswahili sanifu umefikia upeo mkubwa sana katika kiwango cha istilahi za fani na sayansi maalumu, hasa katika uwanja wa magazeti, sayansi jamii, sheria, sayansi ya taalaki za ubinadamu, isimu, lugha, fasihi, falasafa ya lugha na uandishi wa habari, bado lakini upanuzi wa Kiswahili bado unazorota katika matumizi ya maneno ya maisha ya kawaida.

Kwa maneno mengine, makamusi yetu tuliyonayo yanaacha maneno ya msingi kutoka Viswahili mbalimbali, maneno na mipangilio ambayo inatumiwa katika janibu nyingi za Kenya, Tanzania na Uganda, licha Rwanda, Burundi na Congo.