http://www.swahilihub.com/image/view/-/4392590/medRes/1938400/-/j5oqu7z/-/maina.jpg

 

Kitovu cha Kiswahili (Swahili Hub)

Stephen Maina

Bw Stephen Maina. Picha/MAKTABA 

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Monday, September 17  2018 at  15:53

Kwa Muhtasari

Tovuti ya www.swahilihub.com ilianzishwa ili kukidhi haja ya mawawasiliano ya kidijitali kwa watumiaji wa Kiswahili duniani kote.

 

1.0  Utangulizi

KAMPUNI ya Nation Media Group (NMG) imekuwa mstari wa mbele kwa muda mrefu katika kukikuza, kukiendeleza na kukisambaza Kiswahili tangu ilipoanzishwa mwaka 1959. Magazeti ya Kiswahili kama Taifa Leo linalochapishwa nchini Kenya, Mwananchi na Mwanaspoti yanayochapishwa Tanzania pamoja na runinga kama NTV na stesheni za redio huendesha vipindi vya Kiswahili.

Tovuti ya www.swahilihub.com ilianzishwa ili kukidhi haja ya mawawasiliano ya kidijitali kwa watumiaji wa Kiswahili duniani kote.

2.0 Historia ya Kiswahili

Lugha ya Kiswahili ni lugha ya Kibantu na chimbuko lake ni upwa wa Afrika Mashariki kuanzia kusini mwa Somalia hadi kaskazini mwa Msumbuji zikiwamo lahaja  takriban 15 kama Kiunguja, Kipemba, Kihadimu, Kimtang’ata, Kingare, Kijomvu, Kipate, Kiamu, Kimvita, nk. Lahaja ya Kiunguja ilichaguliwa enzi wa ukoloni ili isanifiwe  kutokana na ueneaji wake bara kwa njia isiyo rasmi na iliyo rasmi kwa mujibu wa Whiteley (1988). Njia za uenezaji wa Kiswahili ni pamoja na biashara, tawala mbalimbali wa Kiarabu,  Kijerumani na Kiingereza, harakati za ukombozi, elimu na dini.

Lugha ya Kiswahili imetumika kama ni mojawapo ya mbinu za kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa makabilla mbalimali. Ni ishara ya utambulisho wa ukombozi wa nchi za Afrika Mashariki kutokana na athari za wageni kama Wazungu na Waarabu  kama alivyobainisha Ngugi wa Thiong'o (1993).

Ili kufanikisha azma hiyo, shughuli zote za ukuzaji na usanifishaji wa lahaja ya Kiunguja, iliundwa Kamati ya lugha (Kiswahili) ya Afrika Mashariki na katibu wake wa kwanza akiwa hayati Frederich Johnson.

Vilevile Shirika la Uchapishaji vitabu la Afrika Mashariki (EALB). liliundwa ili kuwahamasisha waandishi chipukizi na pia kutoa muhuri wa ithibati kwa vitabu vya ziada na kiada.

3.0 Usanifishaji

Usanifishaji wa Kiswahili ulianzishwa enzi za ukoloni mwaka 1930 na kutekelezwa na Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki ambayo ilifikia hatima yake mwaka 1964 ilipoundwa Taasisi ya Ukuzaji wa Kiswahili (TUKI) chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hatua hii ilichukuliwa baada ya kila nchi katika Afrika Mashariki kupata uhuru na hivyo kuwa na sera tofauti.  

Kwa mujibu wa Jarida la Pan African Studies Vol 2 la March 2009, maeneo mbalimbali yaliainishwa kusaidia kuimarisha Kiswahili kama vile biashara za mpakani, muziki wa taarab, wa  kisasa na wa Injili. Pia kulikuwa na uandishi wa tenzi, hadithi, mashairi na semi ambapo waandishi nguli kama Shaaban Robert, Mathias Mnyampala, Akilimali Snowhite, Shafii A. Shafii, Mwenda Mbatiah, Kyallo Wamitila, Chiraghbin (1977), Muyaka bin Haji, nk. walivuma.

Kazi za tafsiri nazo zilifanyika kama maandishi ya vitabu  kama Wimbo wa Lowino (Okot P’ Bit P’Poitek) Usaliti (Betrayal) na F. Imbuga, Mabeberu wa Venice, Julius Kaisari na J.K. Nyerere, na kadhalika.

4.0 Mchango wake katika maendeleo

Kabla ya uhuru, Kiswahili kilitumika kama chombo cha  kuwaunganisha Waafrika wakati wa ukoloni kutokana na kutumika kwake kwenye Umoja wa Waafrika uliojulikana kama PAFMECA na kusaidia wakati wa harakati za kupigania uhuru.

Dini za Ukristo na Uislamu zilitumika kukieneza Kiswahili kwenye hotuba/mihadhara, uandishi na  ellmu.

Biashara ya mpakani ilifanyika kwa kutumia Kiswahili na ilipunguza mikwaruzano ya kikabila na kuimarisha umoja na utangamano.

5.0 Ukuzaji wa Kiswahili

Kiswahili ni lugha yenye historia ndefu ya uandishi hasa mashairi na tenzi. Mabingwa wabobezi wa Kiswahili walianza kujitokeza. Utunzi wa tenzi na mashairi katika pwani ya Kenya kama Lamu, Pate na Mombasa wakiwamo kina Fumo Liyongo (karne ya 14), Muyaka bin Haji (karne ya 17) na baadaye Alamin Mazrui na Abdulatif Abdallah waliinukia.   

Hatua za makusudi zilianzishwa kukiimarisha Kiswahili kwa kuongeza msamiati na istilahi za taaluma mbalimbali.

Kwa kutumia vyombo vya habari kama redio, magazeti na runinga mada mbalimbali zilibuniwa na kuenezwa ili kukikuza na kukiimarisha.

Kimataifa:

Inafahamika kuwa wazungumzaji wa Kiswahili wanazidi kuongezeka na lugha ya Kiswahili inazungumzwa katika maeneo ya Afrika Mashariki na Kati, Visiwa vya Comoro, Kaskazini ya Msumbiji na kusini mwa Somalia.

Nje ya Afrika  Mashariki, Kiswahili kinatumika kwa kusomeshwa na kutangazwa sehemu mbalimbali za Afrika na nje ya bara hili. Ziko redio, runinga, mitandao ya kijamii na tovuti ambazo zinatumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano. Baadhi ya nchi hizi ni Uingereza, Ufaransa,  Marekani, India, Korea Kusini, Sweden, Finland, Norway, Ujerumani na Japan.

Swahili Hub (Kitovu cha Kiswahili)

Ili kushadidia juhudi zilizopo za ukuzaji wa Kiswahili, Kampuni ya Nation Media Group (MNG) ilibuni mradi wa Swahili hub kwa lengo la kukiendeleza Kiswahili ili kiweze kuimarika katika matumizi yake ya fasihi na isimu kwenye elimu, siasa, uchumi, utamaduni na teknolojia.

Mradi huu ulioanzishwa nchini Kenya mwaka 2012, chini ya usimamizi wa NMG na mwaka 2016 makao makuu yake yalihamishiwa katika Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Sababu za kuhama

Kiswahili ni lugha yaTaifa na pia ni lugha rasmi nchini Tanzania. Ni lugha rasmi ya mawasiliano katika shughuli za kiserikali na pia mhimili muhimu kama Bunge na Baraza la Wawakilishi.  Ziko taasisi na asasi nyingi za kitaifa na binafsi zinazojishughulisha na Kiswahili kama Taasisi za Taaluma ya Kiswahili (Tataki), Baraza la Kiswahili Bara (Bakita) na Visiwani kuna Baraza la Kiswahili (Bakiza), Chama cha Usanifu na Ushairi Tanzania (Ukuta), Chama cha Waandishi wa Vitabu vya Kiswahili (Uwavita), Chama cha waandishi na watangazaji wa Kiswahili katika Jumuiya ya AFrika Mashariki, Chama cha Walimu na Wahadhiri wa Kiswahili (CHAKAMA), Chama cha wanachuo wa Kiswahili wa vyuo vikuu (CHAWAKAMA), Skuli ya Kiswahili Zanzibar (SUZA) na  makao makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kiswahili ni lugha ya kufundishia katika shule za msingi vyuo vya ualimu Daraja la A, na ni somo la lazima kwa shule za sekondari hadi kidato cha nne. Iko pia Taasisi ya Ukuzaji wa Mitalaa ambapo vitabu, silabasi za somo la Kiswahili huratibiwa. Mwishowe yako magazeti ya Kiswahili takriban kumi na wataalamu wasomi wengi wa Kiswahili ambao wanaweza kuchangia katika taaluma ya Kiswahili.

Kwa hiyo ni rahisi kukusanya taarifa, kufanya utafiti, kupata mawaidha kuhusu Kiswahili na kusambaza maudhui ya Kiswahili kwa urahisi.

Matumizi ya Kiswahili kidijitali

Kwa kutambua umuhimu wa Kiswahili hasa katika kuimarisha uelewano na ushirikiano katika jamii ya Afrika Mashariki na Kati, Kampuni ya NMG mbali na kutumia redio, runinga na magazeti, imebuni njia nyingine mpya ya mawasiliano kwa digitali. Hii ina maana kwamba taarifa mbalimbali za kiuchumi, siasa, elimu, utamaduni, nk. zinaweza kuifikia jamii na wadau wengi wa maendeleo kwa wepesi kwa kutumia tovuti  ya ‘Swahili Hub,’ na mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter na Intagram. Kompyuta au simu za kiganjani zenye Intaneti nazo zinaweza kukupatia  huduma kwa kutumia ya tovuti ya www.swahilihub.com

Mchango wake katika maendeleo

Katika makala yaliyoandikwa na Dkt John Habwe wa Chuo Kikuu cha Nairobi kuhusu nafasi ya Kiswahili katika utangamano wa wananchi wa nchi za Afrika Mashariki, yametajwa mambo yafuatayo ambayo ni muhimu kuzingatiwa. Kwanza ni kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa makundi mbalimbali ya kikabila. Istilahi kutoka lugha za makabilia zinaweza kuingizwa katika Kiswahili ili kukiimarisha. Yako maneno ya kikabila yaliyoingizwa katika lugha ya Kswahili kama Ikulu, Bunge, kung’atuka, kitivo, hala-Kigogo (peneplain), itale-Kisukuma- (granite),Kilala-Kihaya, Kinyamwezi- (fallow), nk. Istilahi hizi zinatumika katika taaluma mbalimbali kama Jiografia, jiolojia, siasa na utawala, nk. Pili, ni kuimarisha ubadilishanaji wa bidhaa za biashara mpakani. Tatu, ni uendelezaji wa lugha kwa kutumia tenzi, mashairi, tungo mbalimbali kama hadithi na insha kama walivyofanya kina Said A. Mohamed, Shafii A. Shafii, E. Kezilahabi, nk. (Tanzania), Mwenda Mbattiah, Kyallo Wamitila,  Aliamin Mazrui, nk. (Kenya), na wengine wengi.

Nne, wakati wa shughuli za kazi Kiswahili kinatumika mashambani, viwandani, biashara za aina mbalimbali za mipakani, pia usafiirishaj wa vitu na abiria. Tano, kwenye mawasiliano wa habari kwa kutumia vitabu, magazeti, redio, runinga na tovuti Kiswahili kinatumika na hii inatokana na utandawazi.

Kuhuishwa kwa Tovuti

Tangu kuanzishwa kwake, Tovuti ya Swahili Hub ina vipengele vitano kama Habari Mseto, Tahariri, Michezo, Habari za Kitaifa na pia za Kimataifa. Vilevile viko vipengele vinavyohusu makala za elimu, siasa, uchumi, biashara, utamaduni na michezo.

Katika kuiimarisha tovuti hii, imependekezwa viainishwe vipengele vingine na kuongezwa kama  fasihi (mashairi, tenzi, semi, hadithi, methali, tungo, uandishi na uhakiki wa vitabu na makala, nk.) Kwa upande wa isimu kuwe na masuala ya isimu kama sarufi maumbo, miundo ya sentensi, fonetiki, maana za maneno na kadhalika.

Vilevile kuwe na nafasi ya kuongeza uchambuzi wa vitabu, utafiti wa fasihi na isimu  pamoja na ikisiri zinazoandikwa na wataalamu mbalimbali ili kuwavutia wasomi wa Kiswahili

Vipengele hivi kwenye tovuti au mitandao ya kijamii vitasaidia kuielimisha jamii pamoja na wageni wanataka kujifunza na kijiendeleza katika lugha ya Kiswahili.

Mafunzo

Katika ulimwengi huu wa utandawazi, mafunzo ya Kiswahili yanatumia mifumo ya aina mbili ya Kiswahili. Mfumo mmojawapo  ni kwa mwanafunzi kushiriki moja kwa moja akiwa darasani na mwalimu. Pili, ni kwa njia ya kieletroniki kama digitali inayofahamika kama ‘E-Learning’.

Wenyeji na  wageni wanaweza kujifunza Kiswahili kwa mifumo hii miwili  yaani kwa njia ya tovuti na mitandao badala ya kuingia darasani. Njia hii inatumia tovuti ya www.swahilihub.com au kwa mitandao ya kijamii inayotumia mfumo wa YouTube.

Mfumo unaotumika kufundisha Kiswahili kwa wageni  kama ilivyo kwa Skuli ya Kiswahili, SUZA Zanzibar au Kituo cha Kiswahili cha Usa River, Arusha imeezoeleka  zaidi ni ya ana kwa ana. Mfumo wa kieletroniki ni mgeni hasa kwa wenyeji. Uko mpango unaoandaliwa na Kitengo cha Swahili hub wa kuanzisha mfumo wa ufundishaji wa Kiswahili kwa njia ya kidigitali ukianzia na hatua ya awali; ya kati ya cheti na diploma; na hatimaye hatua ya juu kwa kupata shahada ya chuo kikuu. Mipango iko mbioni kuuandaa mfumo huu.

Kazi za Swahili hub

Kazi kubwa ya Kitovu cha Kiswahili (Swahili Hub) ni kukusanya na kusambaza kwa kupakia f kwenye tovuti na mitandao ya kijamii fani mbalimbali za Kiswahili. Fani hizi ni mashairi, tenzi, hadithi, tamthiliya, sarufi miundo, sarufi maumbo, mapitio ya vitabu, tafiti za kitaaluma zilizofanywa na wataalamu wa Kiswahili.

Lengo ni kuielimisha jamii juu ya masuala ya uchumi, siasa, elimu, sayansi na utamaduni yanayotokea duniani kote.

Shabaha

i) Kutayarisha, kuendeleza na kuisimamia  tovuti ya Swahili Hub.

ii) Kukusanya mada za Kiswahili na kuzisambaza kwa watumiaji.