Mabadiliko ya mitaala yanavyochangia mabadiliko katika uandishi na ufundishaji wa Kiswahili

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, April 18   2017 at  14:21

Kwa Mukhtasari

DHANA mtaala imeelezwa kwa namna mbalimbali na wataalamu tofauti wa elimu. Bobbit (1968 katika Okech & Asiachi 1992) kwa mfano amedai kuwa mtaala ni ule mfululizo wa vitu ambavyo watoto na vijana ni lazima wavifanye na wavipitie maishani mwao kama njia mojawapo ya kukuza uwezo wao wa kufanya kimwafaka mambo ambayo ni ya kiutu-uzima. 

 

Naye Beauchamp (1968 katika Okech & Asiachi 1992) ameeleza kuwa mtaala ni masomo na yaliyomo katika kozi fulani. Hususan amedai kuwa mtaala ni hati iliyoandikwa ambayo inajumuisha viambato, lakini hasa mpango wa elimu ya watoto wanapokuwa wamesajiliwa katika shule fulani. 

Kufuatia madai ya wataalamu hawa, Okech & Asiachi (1992:4) wameeleza mtaala kuwa:
“...mpangilio wa matendo yaliyonuiwa kumfanya mwanafunzi atimize kadiri inavyowezekana malengo fulani ya kielimu.” 

Katika hali finyu, mtaala ni masomo yanayofundishwa, au kiupana mtaala ni matukio anayoyapitia mwanafunzi nje na ndani ya skuli.

Mabadiliko ya kimitaala yanayohusiana na uandishi na uchapishaji wa Kiswahili yanahusiana na mabadiliko ya mifumo ya elimu nchini Kenya.

Mfumo wa elimu unapobadilika unaathiri masomo mengi. Hata hivyo, katika makala hii tutalenga mabadiliko yaliyohusiana na Kiswahili pekee. 

Mnamo 1964, serikali iliteua Tume ya Elimu ya Kenya iliyoongozwa na Profesa Ominde.

Tume hiyo ilipendekeza mfumo wa elimu wa 7-4-2-3. Pia ikapendekeza matumizi ya Kiingereza katika kufundishia tangu shule za msingi. Kutekelezwa kwa pendekezo hilo kulichcohea kuanzishwa kwa Mwelekeo Mpya wa Msingi. Hata hivyo, tume ikatahadharisha kwamba lugha za kikabila zisipuuzwe. 
    

       
Kipindi kimoja
Kwanza, ikapendekeza pawepo na angalau kipindi kimoja cha fasihi simulizi (kutoa hadithi) kila siku katika ratiba ya shule kati ya madarasa ya 1 na 3.

Pia Kiswahili kilitambuliwa kama lugha ya taifa na utaifa wa Afrika. Kwa sababu hiyo, tume ikapendekeza mpango maalum wa kuwaandaa walimu wa Kiswahili na Kiarabu nyakati za likizo.

Hata kama Kiswahili kilitambuliwa, ufundishaji wake katika skuli za msingi haukutiliwa maanani. Kilitengewa vipindi vichache sana na hakikutahiniwa katika mtihani wa mwisho wa Darasa la Saba – Certificate of Primary Education (CPE).

Kwa hivyo, shule nyingi hazikukifundisha kamwe na vipindi vyake vikatumiwa kwa ajili ya masomo 'muhimu’ kama vile Hisabati na Kiingereza (Ogechi 2002b).

Kufikia mwaka wa 1967, shule nyingi hasa za mashambani zilikumbwa na matatio kufuata MwelekeoMpya wa Msingi na zikaanza kufundisha kwa lugha za kikabila.

Mwelekeo Mpya wa Msingi ukapuuzwa na kukaanza kufundishwa lugha za kikabila kwa miaka ya kwanza mitatu ya shule za msingi.

Mtaala huu uliathiri ufundishaji wa lugha za kikabila na hivyo kitengo cha Mbinu za Kijumla katika Taasisi ya Elimu ya Kenya (KIE) kilianzisha uchapishaji wa mfululizo wa vitabu katika lugha za kienyeji ulioitwa Tujifunze Kusoma Kikwetu. Kwa sasa KIE yaitwa Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala (KICD). 


Mtazamo ulilegezwa
Kufikia mwaka wa 1970, mtazamo uliotiliwa mkazo na Mwelekeo Mpya wa Msingi ulilegezwa kwa sababu ya ukosefu wa usare katika ufundishaji, marejeleo na ukaguzi mbaya wa ufundishaji shuleni.

7-4-2-3 ina maana: miaka saba ya masomo ya shule ya msingi, minne katika shule ya upili, miwili katika kiwango cha juu cha shule ya upili na angalau mitatu katika chuo kikuu.

Athari kubwa ya mabadiliko ya mitaala kufuatia Tume ya Ominde (1964) mintarafu ya uandishi na uchapishaji imeelezwa na Chakava (1992a: 121):

“…ingawa vitabu ni nguzo muhimu katika ufanisi wa mfumo wowote wa elimu, ripoti ya tume haikusema lolote kuvihusu na jinsi ambavyo vingetungwa, vikazalishwa na kusambazwa ili kuutumikia mfumo wa elimu uliopendekezwa.” 

Na kwa kuwa ripoti hii muhimu haikusema lolote, nafasi muhimu ya kupendekeza sera ya taifa kuhusu uchapishaji wa vitabu na usambazaji wao ilipotezwa.

Mtaala tena ukabadilika mnamo 1976 kupitia kwa tume ya serikali iliyoongozwa na Gachathi (Jamhuri ya Kenya 1976). 

Tume hiyo ikapendekeza ufundishaji kwa lugha za kikabila hadi Darasa la Tatu. Pia ikapendekeza ufundishaji na utahini wa Kiswahili katika mtihani wa CPE.

Hata hivyo, mintarafu ya Okech & Asiachi (1992:135) “bado tutaendelea kukitumia Kiingereza kama lugha ya taifa na lugha ambayo kwayo vifaa vyote vya kufundishia vitatungwa.”

Labda kwa sababu hii na nyinginezo za kisiasa, Kiswahili hakikutahiniwa katika mtihani wa CPE. Vipindi vyake bado vikaendelea kutumiwa kufundishia masomo muhimu.

Katika shule za upili, Kiswahili kilikuwa somo la hiari na skuli nyingi hazikukifundisha.

Mnamo 1981, aliyekuwa rais wa Kenya, Daniel arap Moi, aliunda tume iliyoongozwa na Mackay.

Tume hii ilipendekeza mtaala ambao unabobea mwelekeo wa kiufundi badala ya ule wa awali uliokuwa wa kinadharia. 

Mfumo wa awali ulimtayarisha mwanafunzi kuishinda mitihani tu na kutafuta kazi za ofisini. Ikapendekezwa kuwa mfumo wa elimu ubadilike kutoka 7-4-2-3 hadi 8-4-4. 

Somo la lazima
Isitoshe, ili kuhakikisha kuwa ufundi umeufikia umma, ikatakiwa lugha ya Kiswahili isisitizwe.

Hii hasa ilitokana na ugunduzi kuwa wengi wa wanafunzi waliofuzu kutoka vyuo vikuu hawangeweza kujieleza kwa Kiswahili (Jamhuri ya Kenya 1981: 40).

Basi ikawa Kiswahili ni somo la lazima la kufundishwa na kutahiniwa katika mitihani ya shule za msingi na sekondari.

Alivyodai Mukuria (1995) Kenya ilijikuta haina vifaa (vitabu na walimu wa Kiswahili) vya kutekeleza pendekezo hili. Mitaala ya awali ilifanya wachapishaji kutopendelea kupokea miswada ya Kiswahili kwa kuwa soko la lugha hii lilikuwa finyu. 

Mitaala ilihimiza uandishi na uchapishaji kwa Kiingereza. Wanasiasa waliokuwa na ushawishi mkubwa wakati huo kama vile Mkuu wa Sheria, Charles Njonjo, walikuwa wanakipiga vita Kiswahili na kudai kuwa hakikuwa lugha ya Kiafrika na kwamba hakingeweza kutumika katika taaluma.