Washairi Tanzania

Na Nyembo Atwai Nyembo

Imepakiwa - Monday, March 4  2019 at  15:22

 

Hadi hodi gazetini, kwenu naja kurasani,

Niweke japo pembeni, nisomeke hadharani.

Niyatowe ya moyoni, kwa washairi nchini,

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Ni ukweli usopingika, kutengeneza kikundi,

Washairi kuunganika na kutoweka kilindi,
Mwisho tutanufaika, kwa kupitia  kikundi,

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Mbetumbetu tuwe moja, shime na tubebe dhima,

Nguvu yetu kuwa moja, tujenge yaliyo mema,

Kikundi ni nguvu moja, kwa kauli ya Karima,

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Wa bara na visiwani, wote tuwe kundi moja,

Tukitoka hadharani, na tulonge lugha moja,

Jahazi litoke chini, kwa nguvu jasho kuvuja,

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Watunzi wale watangu, na hawa wa zama hizi,

Katu tusiwe  mafungu, kama jani na mizizi,

Tushiriki ndugu zangu, kwa ukweli na uwazi,

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Vyama vimekuwa vingi, wakati dhana ni moja,

Vingine siyo msingi, ushairi vinatija,

Twajiwekea vigingi, kutokuivuka moja,

Washairi Tanzania, tengenezeni  umoja.

Umoja ni nguvu sana, waliyasema wahenga,

Watu ni kushikamana, kwa malengo ya kujenga,

Kwa nini tunatengana, kama wachezao vanga

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Kalamu naweka chini, naikunja karatasi,

Niiweke bahashani, shairi langu jepesi,

Nitume gazetini nikawatowe ugwasi, 

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

 

 

ZAMA ZA HAPA KAZI

Na Shaaban Maulidi maulidishaaban54@gmail.com

Imepakiwa - Monday, March 4  2019 at  15:15

 

Ni zama za Magufuli, John Pombe wa Josefu, 
Kuongoza serikali, ya taifa takatifu, 
Niwa chuma mhimili, kiboko ya wakosefu, 
Ni zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Ni rais wa wanyonge, mkombozi Tanzania, 
Msururu tuupange, medai kwenda kuvaa, 
Tukalimiliki tonge, John Pombe ni Shujaa, 
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Zama za kujenga nchi, kuondoa mafisadi, 
Zama zetu wananchi, nchi yetu kufaidi, 
Zama siyo za wadachi, kujidai yatubidi, 
Ni zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Tanzania ya viwanda, ndiyo sasa inajengwa, 
Uchumi nao wapanda, hilo si la kupingwa, 
Rasilimali kulinda, nchi isiwe jangwa, 
Ni zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando

Za kujenga barabara, mijini na vijijini, 
Kuijenga reli bora, ya kwenda mikoani, 
Na daraja la Tazara, magari pita hewani, 
Ni zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Ndege tatu kwa mpigo, usarifi wa angani, 
Bandari kutega tego, kuwakamata wahuni, 
Na viongozi mizigo, wamekimbia gizani, 
Ni zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Zama za kutema rushwa, siyo zama za kuila, 
Uvivu unakomeshwa, kufanya kazi ni kula, 
Ajira za kurithishwa, hivi sasa zimelala, 
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Siyo zama za Ulaya, ni zama za majimboni, 
Zile posho posho mbaya, kupeana vikaoni, 
Zama za kuchuja chuya, mchele ubaki ungoni, 
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Siyo zama za kupinga, elimu sasa ni bure, 
Zama mkono kuunga, sote tuwe saresare, 
Kwa pamoja tunapanga, kuyarudi ya nyerere, 
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Twende mbele rudi nyuma, huo ndiyo mwendo bora, 
Kama baba wa huruma, tena aliye busara, 
Fumbua macho tazama, kisha uchore dira, 
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Tazama sisi wanao, tuliotumwa kusoma, 
Sikia chetu kilio, tungali bado twahema, 
Hlaafu tega sikio, irudi yetu heshima,
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Wape vijana ajira, walomaliza kusoma,
Sanaa sio hasara, sisi ni walimu wema,
Tukipata mishahara, kwetu sisi ni salama,
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Zama za hapa kazi, twaomba mtupe kazi,
Tazama haya machozi, ya BAED yetu kozi,
Sisi ni wachapakazi, tupeni tupige kazi,
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

 

 

 

TANZANIA YA FURAHA

Na  Shaaban Maulidi 0718526159/ 0763902318

Imepakiwa - Monday, March 4  2019 at  15:27

 

Nabakia Tanzania, siondoki Tanzania,
Nitaishi Tanzania, na kukua Tanzania,
Nitajenga Tanzania, na kuoa Tanzania,
Tanzania nchi bora, busitani ya furaha.

Kuna nini Tanzania, hadi nikuchukie, 
Ulaya kufikiria, Marekani kimbilie,
Kutaka kwenda India, nini nikakigundue?
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha amani.

Tulivu hali ya hewa, miti ya kila aina,
kuna mito na maziwa, samaki kila aina,
Bahari tumeletewa, ile ya Indiana,
Tanzania nchi bora, busitani ya furaha.

Tanzania ya neema, tunacho chakula tele,
Unga dona na mtama, mahindi hata uwele,
Tunda tamu la kuchuma, alizeti na mchele,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha amani.

Tumepewa wengi kuku, wa mayai na wa nyama,
Mbuzi ng'ombe wapo huku, kula nyama za kuchoma,
Kwa maziwa si kapuku, kwa hakika ninasema,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha furaha.

Watu wake watu wema, wapole na wakarimu,
Walojawa na huruma, roho za kibinadamu,
Tena wanayo heshima, ya kauli na salamu,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha amani.

Mlima wa Kilimanjaro, ni ishara ya upendo,
Hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti ni uhondo,
Aridhi ya Morogoro, na mbozi kuna kimondo,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha furaha.

Ziwa refu Tanganyika, ziwa kubwa lipo Mwanza,
Fukwe zilizopangika, bahari hindi ya kwanza,
Migodi iliyotajirika, ya Mwadui na Uvinza,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha amani.

Tembo na pundamilia, simba, twiga na viboko,
Mito ya kuogelea, gesi na maporomoko,
Ndege wa kila jamia, huruka huku na huko,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha furaha.

Karibuni Tanzania, busitani ya Edeni,
Mbuga zake tembelea, maajabu tazameni,
Tabora Mbeya Songea, Zanzibar kisiwani,
Tanzania nchi bora, busitani ya amani.

 

 

 

 

MAMA AFRIKA

Na Richard Boniface Kumyola

Imepakiwa - Monday, May 14  2018 at  14:44

Kwa Muhtasari

Mama wa kiafrika, nguzo  yetu kiukwasi,

Juhudi akajitwika, mengine ya ukakasi,

 

Mama wa kiafrika, nguzo yetu kiukwasi, Juhudi akajitwika, mengine ya ukakasi,

Mama wa kiafrika, nguzo  yetu kiukwasi,

Juhudi akajitwika, mengine ya ukakasi,

Licholima akipika, moyo  hauna kisasi,

Mwanamke kakamavu, asiwepo wa mfano.

 

Nimejipanga zaidi, kumpa yake kongole,

Hunifanya nifaidi, nisikiapo kengele,

Kama ua uwaridi, kanifaa kwa milele,

Mwanamke  kakamavu, asiwepo  wa mfano.


Katunza jamii yake, yeye machoni angavu,

Katazama na upweke, siwe kama wapumbavu,

Siteme watoto wake, alishe wasiwe mbavu,

Kama ukipigwa teke, akufuta chozi  shavu,

Mwanamke  kakamavu, asiwepo wa  mfano.


Mama wa utamaduni, kisima cha chemchem,

Angeishi uzunguni, yu talanta kemkem,

Chachandu ya mafigani, mlo  ulio  adhim,

Mwanamke  kakamavu,asiwepo wa mfano.


Bingwa  kutoa  malezi, adimu  kwa  wahadhini,

Nikiwapo  matembezi, dira kaa akilini,

Megewa haipendezi, chota yote kiganjani,

Mwanamke  kakamavu, asiwepo wa mfano.


Wake kuku vifaranga, ni moto otea  mbali,

Ndiye mama kajipanga, sikose  yetu makali,

Mwendo  hajatupa  nanga, simama hana kibali,

Baba akitangatanga, mezani tenga futali,

Mwanamke kakamavu, asiwepo wa mfano.


Kimwili pamoja roho, thamaniye  aijua,

Mwana amvisha joho, shahada akichukua,

Changanyia pishi hoho, haidhuru akijua,

Mwanamke  kakamavu, asiwepo wa mfano.


Ala zisizo mkito, hulifuta  lake vumbi,

Kasimama na mapito, wakati wa kumbikumbi,

Moyoni furikwa wito, kalivuka kila wimbi,

Tumwache lalie mito, hukuwa hadhiye vumbi,

Mwanamke kakamavu, asiwepo  wa mfano.


Topasi asikomee, nguvu ipo  tushangaza,

Mfumo dume kakome, akapate  kuangaza,

Wazo sumu tuzomee, ushindi kuutangaza,

Mwanamke kakamavu, asiwepo  wa mfano.


Karakana yangu sasa, naifunga kwa ubao,

Hata akibaki tasa, bado  akawa  ni zao,

 

 

MAMA AFRIKA

Na Richard Boniface Kumyola

Imepakiwa - Monday, May 14  2018 at  14:44

Kwa Muhtasari

Mama wa kiafrika, nguzo  yetu kiukwasi,

Juhudi akajitwika, mengine ya ukakasi,

 

Mama wa kiafrika, nguzo yetu kiukwasi, Juhudi akajitwika, mengine ya ukakasi,

Mama wa kiafrika, nguzo  yetu kiukwasi,

Juhudi akajitwika, mengine ya ukakasi,

Licholima akipika, moyo  hauna kisasi,

Mwanamke kakamavu, asiwepo wa mfano.

 

Nimejipanga zaidi, kumpa yake kongole,

Hunifanya nifaidi, nisikiapo kengele,

Kama ua uwaridi, kanifaa kwa milele,

Mwanamke  kakamavu, asiwepo  wa mfano.


Katunza jamii yake, yeye machoni angavu,

Katazama na upweke, siwe kama wapumbavu,

Siteme watoto wake, alishe wasiwe mbavu,

Kama ukipigwa teke, akufuta chozi  shavu,

Mwanamke  kakamavu, asiwepo wa  mfano.


Mama wa utamaduni, kisima cha chemchem,

Angeishi uzunguni, yu talanta kemkem,

Chachandu ya mafigani, mlo  ulio  adhim,

Mwanamke  kakamavu,asiwepo wa mfano.


Bingwa  kutoa  malezi, adimu  kwa  wahadhini,

Nikiwapo  matembezi, dira kaa akilini,

Megewa haipendezi, chota yote kiganjani,

Mwanamke  kakamavu, asiwepo wa mfano.


Wake kuku vifaranga, ni moto otea  mbali,

Ndiye mama kajipanga, sikose  yetu makali,

Mwendo  hajatupa  nanga, simama hana kibali,

Baba akitangatanga, mezani tenga futali,

Mwanamke kakamavu, asiwepo wa mfano.


Kimwili pamoja roho, thamaniye  aijua,

Mwana amvisha joho, shahada akichukua,

Changanyia pishi hoho, haidhuru akijua,

Mwanamke  kakamavu, asiwepo wa mfano.


Ala zisizo mkito, hulifuta  lake vumbi,

Kasimama na mapito, wakati wa kumbikumbi,

Moyoni furikwa wito, kalivuka kila wimbi,

Tumwache lalie mito, hukuwa hadhiye vumbi,

Mwanamke kakamavu, asiwepo  wa mfano.


Topasi asikomee, nguvu ipo  tushangaza,

Mfumo dume kakome, akapate  kuangaza,

Wazo sumu tuzomee, ushindi kuutangaza,

Mwanamke kakamavu, asiwepo  wa mfano.


Karakana yangu sasa, naifunga kwa ubao,

Hata akibaki tasa, bado  akawa  ni zao,

 

 

Tusidunishe Kiswahili

Mary Nanjala Kilob

Mary Nanjala Kilobi - mwandishi na mwanahabari ambaye upekee wa sauti yake kila anaporipoti na kutangaza habari katika runinga ya KTN unazidi kumzolea umaarufu miongoni mwa wapenzi na watetezi wa Kiswahili. PICHA/ CHRIS ADUNGO 

Na JOSEPH MOCHECHE, AYIEKO JAKOYO

Imepakiwa - Monday, October 2  2017 at  11:08

Kwa Muhtasari

KISWAHILI lugha yetu, mbona tunakidunisha,
Twakikabili ja chatu, maisha kinahatarisha?
Wanakitumia watu, wasokuwa na maisha!

 

Kina mengi mashairi, kama lugha nyinginezo,
Hata hakina dosari, mbona kwetu masazo?
Kuboronga kwa athari, za lugha za mwanzo!

Kinacho pia fasihi, riwaya tamthilia,
Usisahau tarihi, mbona twakiachilia?
Sasa chakosa wajihi, babu walokipatia!

Oneni yake fasihi, nzuri ya kujifunzeni!
Kinatumia herufi, kama lugha za kigeni!
Tumefanya kiwe fifi, jama twakiulizani?
JOSEPH MOCHECHE

Kiswahili kitukuzwe

Kiswahili kwetu mali, lugha imeshanawiri,
Ndiyo lugha ya asili, kutujuza yalojiri,
Misemo na tamathali, Kiswahili chashamiri,
Tutukuze Kiswahili, kizazi hata kizazi.

Lugha tamu ka asali, kitamuka kijasiri,
Ila haina ukali, yaleta yetu fasiri,
Kiswahili kwetu mali, masikini na tajiri,
Tutukuze Kiswahili, kizazi hata kizazi.

Kiswahili mashuleni, masomo kinafundisha,
Kiswahili kanisani, injili chatushibisha,
Kiswahili ofisini, pia kinaburudisha,
Tutukuze Kiswahili, kizazi hata kizazi.

Ngano na chemsha bongo, pia zatupa nasaha,
Zatuliza zetu bongo, kututolea karaha,
Ni kweli sio urongo, lugha inaleta raha,
Tutukuze Kiswahili, kizazi hata kizazi.


AYIEKO JAKOYO
‘Malenga wa Bara’
Mumias

 

 

MWENYEKITI  MAGUFULI

John Magufuli

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli. Picha/MAKTABA 

Na Abdallah Bin Eifan

Imepakiwa - Thursday, July 28  2016 at  15:00

Kwa Muhtasari

Ninatunga kumi beti, shairi kwa Kiswahili,

Nawasalimu umati, kawajalia Jalali,

 

Ninatunga kumibeti, shairi kwa Kiswahili,

Nawasalimu umati, kawajalia Jalali,

Kumpata ni bahati, mtu kama Magufuli,

Shika kiti Magufuli, umekuwa Mwenyekiti.

 

Umekuwa Mwenyekiti, sasa endesha shughuli,

Chama kiwe madhubuti, ndugu ongeza ukali,

Usikwame katikati, wewe nahodha wa meli,

Shika kiti Magufuli, umekuwa Mwenyekiti.

 

Sote tumevaa suti, furaha kila mahali,

Twakupigia saluti, kwa furaha hatulali,

Na chama ukidhibiti, kisafishe usijali,

Shika kiti Magufuli, umekuwa Mwenyekiti.

 

Kiti hicho kiti nyeti, kihifadhi tafadhali,

Badilisha na kamati, nyuso mpya afadhali,

Wafuatane na wakati, na mengi kuyabadili,

Shika kiti Magufuli, umekuwa Mwenyekiti.

 

Kilikuwa mahututi, Chama kingekufa kweli,

Mambo sasa ni tafauti, yanahitaji akili,

Yalo ndani ya kabati, yatowe uyakabili,

Shika kiti Magufuli, umekuwa Mwenyekiti.

 

Ona KANU ni maiti, chama cha Kenya awali,

Zimekwisha harakati, kuifufua muhali,

Yote tamaa ya viti, na chama kutoijali,

Shika kiti Magufuli, umekuwa Mwenyekiti.

 

Utupe yako ripoti, ya chama na serikali,

Fanya yako utafiti, ilikuwa mbaya hali,

Tangaza kwenye gazeti, wasome kila pahali,

Shika kiti Magufuli, umekuwa Mwenyekiti.

 

Hata wapige magoti, huruma ondoa mbali,

Wamevuka vizingiti, walikuwa hawajali,

Kama wapo wasaliti, hao watie kufuli,

Shika kiti Magufuli, umekuwa Mwenyekiti.

 

Tumia yako tiketi, watu wamekukubali,

Chunguza sana bajeti, iendeshwe kihalali,

Kila kitu kwa risiti, walete pia dalili,

Shika kiti Magufuli, umekuwa Mwenyekiti.

 

Shairi hapa tamati, mwisho nimeshawasili,

Nawaombea kwa dhati, atawalinda Jalali,

Itikieni sauti, akiita Magufuli,

Shika kiti Magufuli, umekuwa Mwenyekiti.

  

 

 

 Furaha ya Ndoa Watoto

Na Yahya O Barshid (YOB)

Imepakiwa - Thursday, July 28  2016 at  15:54

Kwa Muhtasari

YOB nasema, ya ndoa huwa watoto,

Oa mke hata kama, kwa mapenzi motomoto,

 

YOB nasema, ya ndoa huwa watoto,

Oa mke hata kama, kwa mapenzi motomoto,

Bila watoto huruma, nyumba hukosa uzito,

Furaha ya Ndoa Watoto.

 

YOB hilo nimepima, kisha nimelichungua,

Ona mwenyewe tazama, kizazi  kikizingua,

Bure hata ukichuma, tegemeo hupungua,

YOB Ninasisitiza.

 

YOB katika kurasa, nawaombea Mwenyezi

Oa kuoa si kosa, awajalie kizazi

Baa hil la utasa, liwaondoke wazazi,

Furaha ya Ndoa watoto.

 

YOB hapa nasimama, nimefikia mwishoni,

Ongezeko la heshima, kwanza kuanzia ndani,

Baba watoto na mama, ndiyo kamati makini,

YOB Nasisitiiza.

Na Yahya O Barshid (YOB)

              

 

 

VIWANDA: Nguvukazi ya vijana

Na Khamisi Mari (Better King)

Imepakiwa - Thursday, July 28  2016 at  15:05

Kwa Muhtasari

Twakumbusha viwanda, vimekosa muamala,

Wamevurundavurunda, mliyowapa dhamana,

 

Twakumbusha viwanda, vimekosa muamala,

Wamevurundavurunda, mliyowapa dhamana,

Vingi wameshaviponda, walengwa kazi hawana,

Nguvukazi ya vijana,  kurudishiwa viwanda.

 

Nguvukazi itapanda, wajibu kukosoana,

Awe mnene konda, tuache kuogopana,

Kukosa funga mkanda, vizuri kuelezana,

Nguvukazi ya vijana, kurudiishiwa viwanda.

 

Raia hawajapenda, wajibu kukosoana,

Hawapaoni pa kwenda, wamebaki kubishana,

Humpati aloshinda, kisa kutoelewana,

Nguvukazi ya vijana, kurudishiwa viwanda.

 

Tamati hapa Kihonda, mafundi kukosekana,

Waharibifu manunda, mabingwa  wa kilindana,

Mashine wakizibonda, lawama  kutupiana,

Nguvukazi ya vjana, kurudishiwa viwanda.

Na Khamisi Mari (Better King)

 

 

Mke mzuri tabia

Na  Kimani Eric Kamau

Imepakiwa - Thursday, July 28  2016 at  15:09

Kwa Muhtasari

Mabibi ni mama zetu, si vyema kuwaingilia,

Wengine ni dada zetu, hatarini wajitia,

 

Mabibi ni mama zetu, si vyema kuwaingilia,

Wengine ni dada zetu, hatarini wajitia,

Wajifanya mtukutu, utajikuta pabaya,

Mke mzuri tabia, sura haina maana,

 

Kila mtu mwenye bongo, na akili sawasawa,

Punguza vyako vishingo, na akili kukutuwa,

Usijifanye uchongo, huoni lililo sawa,

Mke mzuri tabia, sura haina maana.

 

Wake waliosifika, ni tabia nawaambia,

Sio sura na kucheka, wasokuwa na tabia, 

Uzuri wa kupendeka, ni nzuri njema tabia,

Mke mzuri tabia, sura haina maana.

 

Warembo wazuri sana, unapowaangalia,

Lakini hawana mana, bwana wamewakimbia,

Mke mzuri tabia, sura haina maana.

 

Miji wamejazana, sura nzuri nakwambia,

Bali waume hawana, kwa tabia za udhia,

Wengi wao ni vijana, wazuri wakusifia,

Mke mzuri tabia, sura haina maana.

 

Chunguza utawaona, na sura nzuri nakwambia,

Wote hawana mabwana, nyumba wamezikimbia,

Na wazee kina mama, sasa wanajijutia,

Mke mzuri tabia, sura haina maana.

Na Kimani Eric Kamau

 

                         

 

 

 

Kitanda kinacholia

Na J.S. Mhoni (Nguvu za Mwanza)

Imepakiwa - Monday, July 25  2016 at  16:58

Kwa Muhtasari

Edita naja kiwandani, nifae tungo pa safu,

Nimeipata ajenda, kwa Siwema maarufu,

 

Edita naja kiwandani, nifae tungo pa safu,

Nimeipata ajenda, kwa Siwema maarufu,

La kitanda kwa kibada, ninayo mengi marefu,

Vipi waweka turufu kilotulia kitanda.

 

(Jibu)

Na Magdalena Maregesi

Mhariri mhisani, naomba kwako nafasi,

Jibu nimpe Mhoni, tulie yake nafsi,

Maana hajabaini, kitanda fumbo kiasi,

Kunesa yake tabia, kuhema na kugumia.

 

Siwema sitokipenda, kitanda kinacholia,

Abadani sitopanda, kitanda chenye ghasia,

Moyoni kitanitenda, na huzuni kunitia,

Kunesa yake tabia, kuhena na kugumia.

 

Funga pembeni kitanda, katikati chaumia,

Kibanzi na kibaranda, kulia cha kuibia,

Hushukapo na kupanda, fundi utamsikia,

Kunesa yake tabia, kuhema na kuguma.

 

 

 

UJANA

Na SHAABAN ROBERT

Imepakiwa - Monday, July 25  2016 at  17:21

Kwa Muhtasari

Ujana kitu kitamu, tena ni azizi sana,

Maungoni mwangu humu, nilikuwa nao jana,

 

UJANA

Ujana kitu kitamu, tena ni azizi sana,

Maungoni mwangu humu, nilikuwa nao jana,

Kwa wingi katika damu, tahamaki leo sina,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kichwa kimejaa mvi, kinywani meno hamna,

Nikienda kama mlevi, miguu nguvu hamna,

Kama zilizofikichwa, zikang’olewa mashina,

Kumbe ujana ni hivi, rafiki yangu ujana.

Jina langu limekuchwa, na nyota zilizoona,

Ukinitazama kichwa, nywele nyeusi hakina,

Kama zilizofikichwa, ziking’olewa mashina,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Natatizika kauli, midomoni najitafuna,

Nimekusanya adili, walakini hali sina,

Dunia kitu batili, hiki una kile huna,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Nilikuwa ni waridi, furaha, furaha ya wasichana,

Neno hawakunirudi, wakati wa kukutana,

Sasa nanuka baridi, wanionapo waguna,

Nasikitika hadumu, rafiki wengi sana.

Walio wakinihusu, walikuwa wengi sana,

Wanawake wenye busu, uzuri na usichana,

Leo sina hata nusu, ya wanitajao jina,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Wazuri wenye uturi, na mikono yenye ina,

Kila mtu mashuhuri, alipenda kuniona,

Nilifaa kwa shauri, na sasa kauli sina,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Dunia bibi harusi, kwa watu kila namna,

Inapendeza nafsi, wa kati wa kuniona,

Na leo sina nafasi, kwa uzee kunibana,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kilichokuwa gizani, niliwaza kukiona,

Nikakijua thamani, sura yake hata jina,

Leo natazama hasara, hata ikiwa mchana,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kilichotaka fikra, niliweza kukinena,

Kwa mfano na kwa sura, mpaka kikafana,

Leo tazama hasara, nguvu hiyo sina tena,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Hauna dawa uzee, mabega yamepetana,

Anionaye ni wee, ondoka hapa laana,

Wanasema na miye, niliyekuwa na jina,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kaditama nafikiri, uchungu wanitafuna,

Walakini nafikiri, twafuata Subhana,

Katika ile amri, ya kuwa na kutengana,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

 

 

Wachawi saidieni

Na MAKILLA

Imepakiwa - Monday, July 25  2016 at  16:54

Kwa Muhtasari

Sifa zenu naamini, zimeenea mjini,

Kadhalika vijijini, pia kote duniani,

 

SIFA zenu naamini, zimeenea mjini,

Kadhalika vijijini, pia kote duniani,

Kwa kweli twawaamini, ila bado kuwathamini,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Mtunzi nimebaini, mna mengi kwa yakini,

Mwaweza fanya nchini, uchumi usiwe duni,

mkaongeza thamani, dunia kututhamini,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Tunataka televisheni, zenye bei afueni,

Mwazitengeza nyumbani, hamuuzi madukani,

Tunachotaka maishani, hizo ziwe mitaani,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Mwazungumza hewani, ila simu hatuoni,

Nalo hili twaamni, ni biashara auni,

Zije simu za mkononi, tuwe nasi washindani,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Finland na Marekani, kwa Nokia ni makini,

Matorola nayo ndani, ya kwetu iwe akilini,

Tuuite jina gani, pengine la majinuni,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Mashine kazi undeni, tupeleke viwandani,

Msukule watumieni, hata nishati wabuni,

 Ili mradi mwakani, nchi iwe namba wani,

Wachawi  saidieni, tupate maendeleo.

 

Na nungo kageuzeni, tupate ndege angani,

Eitisii iufufueni, iende hadi Japan,

Na mizigo tubebeni, tuiuze kwa jirani,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Elimu yetu ya ndani, mwaisaka ugenini,

Kadhalika mashambani, pamwe yako nyikani,

Vilevile vichakani, yote mnayathamini,

Wachawi tusaidieni, tupate maendeleo.

 

Majongoo geuzeni, wawe wa sasa treni,

Dizeli iacheni umeme tutumieni,

Uchina shirikianeni, mwokoe zetu laini,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

 

Maji huko maziwani, uchawi mtumieni,

Yapande hadi nyikani, tunawesha mashambani,

Tutumie na mijini maana hayaonekani,

Wachawi tusaidieni, tupate maendeleo.

 

 

Salamu kutoka Nakuru

Na  BRYAN ROP KIMUTAI, Nakuru

Imepakiwa - Thursday, July 14  2016 at  20:58

Kwa Muhtasari

Nawasalimu darasa, kitumai mu buheri,

Kipindi cha hivi sasa, aina za mashairi,

 

Nawasalimu darasa, kitumai mu buheri,

Kipindi cha hivi sasa, aina za mashairi,

Tuepuke ukurasa, nyingine kwa usanjari,

Istilahi ndio hasa, tusi kukariri.

 

Kodoa bila kupesa, jalali apate kheri,

Atuepushe mikasa, tukapata tabasuri,

Twaandama kadi, tama kiindi kitatufaa,

Tukianza kimistari, mwanzo mtoto na mleo.

 

 

Mshororo wa shairi, kisha tupate kituo,

Kibwagizo kukariri, ni ule urudiao,

Sitozima kibatari, pasi kutunza mgao,

Ni zinduna na ambari, kwa ukwapi na utao.

 

Tatu mwandamo hatari, utingo ndo ufungao,

Twandamana kadi, tama kipindi kitatufaa,

Ingawa nalipa bili, sikudai weye  kuja,                   

Tathmini ndilo hili, mshororo ni mmoja.

Tathnia ni ya pili, thathlitha na ikaja,

Tarbia ina usuli ya, unne kwa pamoja,

Takhimisa kisasili, utano kwa ukamili,

Tadsisa siwe swali, ndiyo sita mojamoja.

 

Twandamana kadi tama, kipindi kitatufaa,

Si kwa ada ya pesa, nakufundisha bahari,

Sakarani  nakuasa, bbahari kadha habari,

Msuko sitoikosa, ufupisha ni desturi.

 

Tumbuizo kwa usasa, migaomitatu  nari,

Malumbano yakuasa ,uwajibu  washairi,

Sijebaki na hamasa, heri hii nusu shari,

Andamana kadi tama, kipindi kitatufaa.

 

Malenga katika fani, amepatiwa idhini,

Aandikapo diwani, atumie kwa maini

Kwa urari wa mizani, azida kurefusheni,

Inkisari nasemeni, kufupishwa kwa uneni.

 

Tabudila nayo gani? Usanifu haribuni,

Kuboronga eleweni, muafaka changanyeni,

Kaditama ninatua, kongole kunisikia.

 

 

Mke wa mtu ni sumu

Na GEORGE KYOMUSHULA

Imepakiwa - Thursday, July 14  2016 at  20:21

Kwa Muhtasari

Wake mke kamuoa, yanini kumchokoa,

Mahariye katoa, acha kujishongondoa,

 

Wake mke kamuoa, yanini kumchokoa,

Mahariye katoa, acha kujishongondoa,

Mzima kamuopoa, vipi anza mnyofoa,

Mke wa mtu ni sumu, omba sikutwe hukumu.

 

Kwani mkewe mtamu, kipi kuwa chakaramu,

Kumpa yako kalamu, ya mumewe hana hamu,

Nyama mbichi kujihamu, kuiba kwa zamuzamu,

Mke wa mtu ni sumu, omba sikutwe hukumu.

 

 

Sifa zao julikana, heshima hata mchana,

Aweza kuwa kijana, jinamalo akanana,

Chunga mnapokutana, mumewe sije vaana,

Mke wa mtu ni  sumu, omba sikutwe hukmu.

 

Mjini kuwa  mtindo, ndoa vunjika kishindo,

Mume kazi yupo lindo, mke kwenda pigwa tindo,

Miuno kama Mngindo, mwizi kesha piga tindo,

Mke wa mtu ni sumu, omba sikutwe hukumu.

 

Kasheshe unapodakwa, zamu yakowe pakatwa,

Mafuta na akapakwa, vipi goma kupakatwa,

Akaja alipotakwa, giza jua likipatwa,

Mke wa mtu ni sumu, omba sikutwe humu,

 

Onyo jamani nawapa, mke wa mtu ni sumu,

Sione zali mepata, ogopa yake hukumu,

Mke wa mtu ni sumu, omba sikutwe hukumu.

Mwisho.

 

 

 

Wa Shinyanga nambieni

Na MAGDALENA MAREGESI

Imepakiwa - Thursday, July 14  2016 at  20:18

Kwa Muhtasari

Mi Shinyanga sijafika, yalikuwa maongezi,

Aliyenena Mayunga, kwenye zake simulizi,

 

Mi Shinyanga sijafika, yalikuwa maongezi,

Aliyenena Mayunga, kwenye zake simulizi,

Kasema wanarumanga, ugali bila mchuzi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

 

Aliniambia Mayunga, kwao ni Maswa Mwanuzi,

Kuwa mwalima mpunga, kutafuta wanunuzi,

Kula nyie mwajivunga, mapishi hamyawezi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

 

Kanisifia ujinga, kurudi kwao hawezi,

Matajiri wa kufuga, ng’ombe tele kwenye zizi,

Lakini nyumba kujenga, ni tembe boma la zizi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

 

Kasema mkishachunga, katu hamna ajizi,

Mbina ya Mwanagandila,  jadi yenu kuienzi,

Ndiko kwenye chakulaga na kutafuta wapenzi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

 

Kasifu mukijigamba, matajiri mwabarizi,

Kuwa ng’ombe wenu chapa, chini ng’ana matanuzi,

 Juu alama ya pamba viatu vya makubazi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

 

Msimu unapofunga, pamba mwapata mavazi,

Vilabu mnavifunga, kwenye walwa manaizi,

Wanywaji mnawapanga, pombe nyie wanunuzi,

Wa Shinyanga nawambieni, kauli yake  Mayunga.

 

Beti  saba nazifunga, Wasukuma sema wazi,

Mayunga ndiye nyakanga, mkazi na mtambuzi,

Nena nicheke ujinga, nawasifu Wanyamwezi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

Mwisho

 

 

 

 

 

 

 

Shati limenitenda

Na MAGDALENA MAREGESI

Imepakiwa - Thursday, July 14  2016 at  20:00

Kwa Muhtasari

Shati langu nilipenda, nilipata kwa amana,

Nalivaa kwa kupenda, kwa marefu na mapana,

 

Shati langu nilipenda, nilipata kwa amana,

Nalivaa kwa kupenda, kwa marefu na mapana,

Moyoni shati napendawa ungwana nimenena

Ghafla limetoweka, Amani moyoni sina.

 

Hadhi ya shati kupanda, kulipa yangu hazina,

Upendo nikaupanda, mwilini kushikamana,

Thamaniye sijaponda nivaapo naiona,

Ghafla limetoweka, Amani moyoni sina.

 

Rangiye niliipenda, yavutia na vimwana,

Kosa kumbe nilitenda, kulipa yangu dhamana,

Laazimwa na kiranda, Ilala hadi Banana.

Ghafla limetoweka, moyoni Amani sina.

 

Kwa nini limenitenda mwilini sijalikana,

Umeniweka kidonda, naumia sana  sana,

Hasira zimenipanda, kutoweka yangu dhana,

Ghafla limetoweka, moyoni Amani sina.

 

Hakika sijampenda, mtu alonipokonya,

Dukani nipokwenda, mimi pekee bila wana,

Nikanunua kwa tenda, mkataba wa bayana,

Ghafla limetoweka, moyoni Amani sina.

 

Leo niko njiapanda, nyumbani shati hakuna,

Darini nimeshapanda, abadani sijaliona,

Limenicheza kandakanda, wahisani raha sina,

Ghafla limetoweka, moyoni Amani sina.

 

 

 

 

 

 

 

Heko Kikwete, wewe kielelezo

Na Abu Bakari Athumani

Imepakiwa - Thursday, July 14  2016 at  19:57

Kwa Muhtasari

Hivi karibuni yamefanyika mabadiliko ya uongozi katika Serikali ya Tanzania. Mabadiliko haya yanatokana na uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Octoba, 2015 wa kumchagua Rais, Makamu wa Rais, wabunge na madiwani.

 

Hata hivyo wakati wa utawala wake Rais aliyetoka madarakani Jakaya Mrisho Kikwete alifanya mambo mengi mazuri ambayo yatakumbukwa daima. Katika shairi lililoandikwa na Abu Bakari Athumani wa Kaloleni Nairobi, Kenya, ameeleza  umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi zetu mbili. Ameandika:

 

Heko Kikwete, wewe kielelezo:

Na Abu Bakari Athumani

 

Mtu akisema neno, ambalo ni la maana,

Lenye kujaza unono, mazuri kuandamana,

Ni kwetu kwa mfano, tulifurahia sana,

Hongera Bwana Kikwete, Rais wa Tanzania.

 

Kuzungumza maneno, undugu wetu hakika

Si undugu wa mfano, ni undugu wa hakika

Undugu wetu mnono, si undugu wa dhihaka,

Hongera Bwana Kikwete, Rais wa Tanzania.

 

Tena akasema mno, kichokoza  utacheka,

Akatoa na mifano, sisi hatuma mipaka,

Hilo ni letu agano, tokea miaka na miaka,

Hongera Bwana Kikwete, Rais wa Tanzania.

 

Kasema kwa magano, sisi hatuna mipaka,

Kama utaiba pano, Kenya sababu mipaka,

Ujifiche kwa mibano, ukija tutakushika,

Hongera Bwana Kikwete, Rais wa Tanzania.

 

Sasa yao majivuno, mijizi ya kusifika

Wale waloiba pano, Tanzania wakifika,

Wetu ushirikiano, watarudishwa haraka,

Hongera Bwana Kikwete, Rais wa Tanzania.

 

Sasa yao majivuno, mijizi ya kusifika,

Wale walioiba pano, Tanzania wakifika,

Wetu ushirikiano, watarudishwa haraka,

Hongera Bwana Kikwete, Rais wa Tanzania.

 

Na wake wenye midomo, ya kuleta farakano,

Pia wao wamo humo, ndiyo yetu maagano,

Wafunge yao midomo, wasipatwe na sonono,

Hongera Bwana Kikwete, Rais wa Tanzania.   

Mwisho.       

 

 

 

 

 

 

Bangi na Sanaa

Na Idd Ninga wa Tengeru

Imepakiwa - Thursday, July 14  2016 at  19:57

Kwa Muhtasari

Bangi balaa kuvuta, sifa inaharibia,

Inabomoa ukuta mandadi wa sanaa,

Ipo siku ni kujuta, na polisi kuingia,

Bangi na sanaa noma, kama mkijivutia.

 

Wajisifu wakivuta, bangi yawasisimua,

Mwisho siku kujutia, vichwa ikiwasumbua,

Washindwa kufurukuta, wengine kujinunia,

Bangi na sanaa noma, kama mkijivutia.

 

Bangi balaa kuvuta, sifa inaharibia,

Inabomoa ukuta mandadi wa sanaa,

Ipo siku ni kujuta, na polisi kuingia,

Bangi na sanaa noma, kama mkijivutia.

 

Utaona sitasita,kichwani ikikolea,

Hauwezi kufurukuta, hakika nakuambia,

Mgambo wa kutafuta, virungu waje kutia,

Bangi na sanaa noma, kama mkijivutia.

 

Kidogo unapovuta, damu unaishtua,

Na mishipa iso sita, kichwani moshi ingia,

Ukijua umepata, kumbe imekupatia,

Bangi na Sanaa noma, kama  mkijivutia.

 

Maana kioo wajita,  kubwa watuharibia,

Naona wakunja ndita, punde ninamalizia,

Kama uliwahi vuta, najua utachukia,

Bangi na Sanaa noma kamamkijivutia.

Mwisho

 

 

 

 

 

 

Atakaye kusifiwa

Na Makilla.blogspot.com

Imepakiwa - Thursday, July 14  2016 at  19:57

Kwa Muhtasari

Saa hazijafikia, siku ya kuandikiwa,

Shinikizo unatia, ovataimu kupewa,

Mfanyakazi kupewa weye wanakuumbua?

Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia.

 

Kazi umejifanyia na ujura unapewa,

Wajibu uliokuwa, wala haujatimia,

Ufanisi umevia, na ufanifu nafaa,

Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia.

 

Ziada hatujajua, kawaida inakuwa,

Kiasi inapungua, kwa waliotangulia,

Ila wakiri raia, mapambo mwawazidia,

Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia.

 

Wastani wafatia ajabu hajaiba,

Wachache waliopewa, na wengi hawajapewa,

Mizani ukitumia, pande gani yazidia?

Atakaye kusifiwa, wasiwsi anitia.

 

 

Saa hazijafikia, siku ya kuandikiwa,

Shinikizo unatia, ovataimu kupewa,

Mfanyakazi shangaa, weye wanakuumbua?

Atakaye kusifiwa wasiwasi anitia.

 

Kama nguo ingekuwa, wengine wakazivaa,

Sura tu huondoa, zilezile zinakuwa,

Lakuajabikia waliahi sijalijua,

Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia.

 

Saa hazijafikia, siku ya kuandikiwa,

Shinikizo unatia, ovataimu kupewa,

Mfanyakazi kupewa weye wanakuumbua?

Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia.

 

Mbio ingalikuwa, na wale mloanzia,

Wa mwisho mngalikuwa, zawadi mnalilia,

Majaji watazubaa washindwe kukuelewa,

 Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia.

 

Riadha tunafulia, kumbe hivi inakuwa

Tunataka zawadiwa, kwa jasho kulitoa,

Rahisi ilivyokuwa kila mtu anuia,

Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia

 

Rahisi ilivyokuwa, kutwaabila kutoa,

Wengi wanakimbilia, nani atawasumbua,

Kazi tu.singechachua  wengi  wangelikimbia,

Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia.

 

Kandanda twaondolewa, kisa hiki kimekuwa,

Hatujipangi muruwa, na ratiba twakataa,

Uwekezaji wavia, na motisha zafifia,

Atakaye kusifiwa, wasiwasi anitia.

 

 

Afrika ya Leo

Na Idd Ninga wa Tengeru, Arusha

Imepakiwa - Thursday, July 14  2016 at  19:57

Kwa Muhtasari

Siyo, kama ya jana, wakoloni wa mabwana,

Kimya kimya watukana bara halina maana,

Afrika yetu ya kesho, haitokuwa ya leo,

 Afrika yetu ya leo, siyo kama ya jana.

 

Afrika yetu ya leo, siyo kama ya jana,

Binadamu wanauana, kikatili wachinjana,

Hakuna hurumiana, wote wanalaumiana,

Afrika yetu ya kesho, haitokuwa ya leo.

 

Afrika yetu ya leo, siyo kama ya jana,

Ukatili kila kona, waasi wamejazana,

Magaidi wanatuna, pakujificha hakuna,

Afrika yetu ya kesho, haitokuwa ya leo.

 

Afrika yetu ya leo, siyo kama ya jana,

Demokrasia laana yafanya twaumizana,

Madaraka twapigana, na ngozi tunachunana,

Afrika yetu ya  kesho, haitokuwa ya leo.

 

Siyo, kama ya jana, wakoloni wa mabwana,

Kimya kimya watukana bara halina maana,

Afrika yetu ya kesho, haitokuwa ya leo,

 Afrika yetu ya leo, siyo kama ya jana.

 

 

Idd iwe na Amani

Na YAHYA O. BARSHID

Imepakiwa - Thursday, July 14  2016 at  20:26

Kwa Muhtasari

Naanza Bismillah, kwa nguvu zake Wadodi,

Ni sikukuu Wallahi, inayokuja na Idd,

 

Naanza Bismillah, kwa nguvu zake Wadodi,

Ni sikukuu Wallahi, inayokuja na Idd,

Kwa Amani tufurahi, Amani iwe juhudi,

Idd iwe na Amani.

 

Mwezi huu mtukufu, waramadhani swaumu,

Mwezi hu maarufu, una wake umuhimu,

Hivyo tuwe wakunjufu, Kumshukuru Kkaumu,

Idd iwe na Amani.

 

Idd iwe na Amani, ninaomba utulivu,

Tufate ya Qurani, ni kitabu chenye nguvu,

Tusalihusende motoni, tusigeuke majivu,

Idd iwe na Amani.

Siku hizi thelathini, zakaribia kuisha,

Twendeni msikitini, mafupi yetu maisha,

Idd iwe na Amani.

 

 

 

KWAHERI OMAR BABU

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na MWALIMU STEPHEN DIK

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  19:04

Kwa Muhtasari

Kwanza ni mwanzaji, mwisho ni kwa muishaji,

Kwaheri Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

KWANZA ni mwanzaji, mwisho ni kwa muishaji,

Kifo chako ewe gwiji, kwa kweli sikutaraji,

Kilio kwa mtungaji, wa mijini na vijiji,

Kwaheri Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

La sivyo tunakumbuka, wosia ulotuacha,

Lidunde libingirike, jikombora limechacha,

Litupwe na lisiwake, likeshe usiku kucha,

Lala pema Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

Mlo hai sisahau, umoja wetu ndo' nguvu,

Mtu awe akijua, maisha ni kama povu,

Miaka nayo ni ua, mwili wetu ni majivu,

Milele Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

Naandika ukurasa, napiga nduru kichizi,

Naenda nikipapasa, maneno sizungumzi,

Ni Marjan kwa sasa, amaliza matembezi,

Nenda hima Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

Om shanti wa shanti, kaditama wa tamati,

Ole wako we mauti, ningakuvua makoti,

Ondoka kwetu mauti, sura mbaya we mauti,

Ohh nalia Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

MWALIMU STEPHEN DIK,

'Mpenda Ushairi',

Siaya.

 

 

KIFO SOTOA FIDIA!

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na PHIBBIAN MUTHAMA

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  18:46

Kwa Muhtasari

Ni hisia sauti, yake Abu Marijani,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

 

ACHUKUWA kilazima, yeyote amemnyamaa,

Mchangamfu azima, na mwili kumlemaa,

Kwa jeuri na dhuluma, ukatili mekujaa,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

 

Miajali zafanyika, timizie zako mbovu,

Mindwele kali yashika, wasafi waso ovu,

Wako umedhihirika, unapokonya kwa nguvu,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

 

Kwetu watupa daraja, ukisifiye mauti,

Hasa kunapo faraja, wenda chini kwa magoti,

Wona bahati ya luja, tunapochimba mafuti,

Ole wako wachukuwa paso naya kaisari.

 

Kifo huoni huruma! Kichukuwa na wakongwe,

Nyoyoni unatuvama, sowacha dogo vilembwe,

Waja mbele, pia nyuma, haidhuru ndo mizengwe,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

Laiti ungalijuwa, usingalifanya jauri,

Lakini  kesho tajuwa, ya Mola tekwa dhahiri,

Kwako njiya wapitiwa, nasi tungo la shairi,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

 

Kifo nakueleza, kwa wangu utungoni,

Mwawazi takugeuza, tuweke sini maishani,

Asilani wone kiza, tukiwa paradisoni,

Ole wako wachukuwa, pasi naya kaisari.

 

Ni hisia sauti, yake Abu Marijani,

Yalotupata mauti, Jumanne ishirini,

Mgumu hunu wakati, tuwepushiye Manani,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

PHIBBIAN MUTHAMA

'Malenga Mlezi'

 

 

HAKI HAIPO

Dhuluma shule ya Langata

Wanafunzi wa shule ya msingi ya Langata Road Primary wakibebwa kuondolewa kwenye hatari Januari 19, 2015 baada ya polisi kutumia vitoa machozi kutawanya wanafunzi na wanaharakati waliokuwa wakiandamana kupinga kunyakuliwa kwa ardhi ya shule hiyo. Picha/EVANS HABIL 

Na PHILEMON KONGA

Imepakiwa - Saturday, January 24  2015 at  14:55

Kwa Muhtasari

Napangusa machozi, liyotukia Lang’ata,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

 

NAPANGUSA machozi, liyotukia Lang’ata,

Unyanyaso siku hizi, mizizini imekita,

Nasema mi' sinyamazi, ardhi meleta sakata,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

 

Mtoto kupiga kelele, akidai zake haki,

Askari mwaenda mbele, kukinga asishtaki,

Akili zenu mna ndwele, hamfuati itifaki,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

 

Kikosini cha askari, pamejaa sana doa,

Kila wakati tu amri, isiyoweza okoa,

Mliotenda si nadhari, heshimenu mebomoa,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

 

‘Fisa wapigwe kalamu, 'metuaribia sifa,

Nchi iliyotimamu, miongoni mataifa,

Sasa watuuhujumu, tokana hiyo kashfa,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

 

Swala hili la ardhi, kukija ni mahudhui,

Imekuwa  ni hadithi, imezua uadui,

Walaghai wanaridhi, tukiona asubuhi,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

 

Mbona vitoa machozi, watoto wakereketwa,

Chunguza hicho kikosi, kuanzia yule mkubwa,

Huo ni gani uzazi, usiokuwa na utwa,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

 

Hebu nyinyi katubuni, mbele zake Rabuuka,

Apate kuwasamehni, maovu 'liyotendeka,

Maana huo ni 'huni, kweli liyolaanika,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

 

Hapa mimi ninagura, 'mekosa matumaini,

Napunguzami hasira, Mola uwasameheni,

Naomba utupe sura, tustahilisi machoni,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

 

PHILEMON KONGA

"Ustadh Malenga"      

Chuo Kikuu cha Masinde Muliro.                                             

 

 

RAMBIRAMBI BABU

Kariakor, Nairobi

Marafiki na ndugu zake mwandishi Omar Babu wakiwa wamebeba maiti yake kuelekea makaburi ya Kariakor, Nairobi Januari 21 2015. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na LUDOVICK MBOGHOLI

Imepakiwa - Thursday, January 22  2015 at  13:17

Kwa Muhtasari

Swahiba Babu Omari , alikuwa ni mahiri

Mtunzi wa mashairi , mwandishi na mhariri

 

IILIKUWA Januari, asubuhi Jumatano

Nlipopata habari, Babu kafika kikomo

Ametuacha Omari, ulimwenguni hayumo

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

 

Hakika nlishtuka, kupata habari hiyo

Ya Omari kututoka, akatwachia kilio

Hivi nnavyotamka, moyo wanienda mbiyo

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

 

Swahiba Babu Omari, alikuwa ni mahiri

Mtunzi wa mashairi, mwandishi na mhariri

Wa makala na habari, na riwaya kufasiri

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

 

Alikuwa mhadhiri, Omari Babu Chuoni

Vilivyo alishamiri, kazini Ujerumani

Hivi yatubana shari, hayu nasi duniani

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

 

Walakhi Omari Babu, katika historia

Ni mwandishi wa vitabu, kisha m’bunifu pia

Hakubuni kujaribu, ni m’bunifu kwa nia

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

 

Mie moyo waniuma, wanipandisha kiwewe

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe

Na sote nchi nzima, tuombe nyoyo zipowe

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

 

Ingawaje linachoma, tukio la mtu kufa

Ndio ada ya Karima, kinachozaliwa hufa

Kikiishi kitazima, japo kife kwa kifafa

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

 

Leo yeye ameenda, katangulia kuzimu

Tunalia twajipinda, zimetutoka fahamu

Tukumbuke nasi twenda, tutakuwa marehemu

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

 

Jambo la mwisho kunena, sisi sote wafiliwa

Si vyema tulie sana, tumkufuru Moliwa

Ndiyo ada ya Rabbana, ya kufa na kufukiwa

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

 

Naomba naomba sana, tupunguzeni makiwa

Tujaribu kukazana, huzuni kuiondowa

Maana ni dhambi tena, mungu tunamkosowa

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

 

 

 

BURIANI ABU

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na ISMAIL BAKARI

Imepakiwa - Thursday, January 22  2015 at  13:08

Kwa Muhtasari

Alikuwa maridhia, si mtu mwenye kuringa,

Na asingeshabikia, lugha ukiiboronga

 

KILIO tunacholia, kimetanda kwenye anga,

Wengi mmeshasikia, kilotufika kisanga,

Abu ametukimbia, sasa tunalegalega,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Si rahisi kwitikia, kukubali hili janga,

Hasa ukizingatia, juzi tukiwa twalonga,

Kwenda kumsalimia, Omar kumwengaenga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Hayo yameshatukia, hakuna wakuyapinga,

Na kazi yake jalia, si ya mavangamavanga,

Msizue yakuzua, maneno kuungaunga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Mwalimu mulimjua, ni bingwa wa umalenga,

Vipindi alichangia, kwa radio na runinga,

Wengi vikawaingia, kuwatoa ushambenga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Vitabu katwandikia, vyenye tungo zenye kunga,

Na vya Kiswahili pia, riwaya zenye muanga,

Vyote vimesaidia, kuongoza vijulanga,
Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Alikuwa maridhia, si mtu mwenye kuringa,
Hakupenda kupapia, mambo yasiyomlenga,

Na asingeshabikia, lugha ukiiboronga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Nataka kuwahusia, kina manju na malenga,

Japo ameshakimbia, hatupo naye mkunga,

Fuateni zake njia, na ninyi muwe wahenga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Maswahiba na insia, jamaa na wamachinga,

Mwaombwa kuvumilia, wala sio kujitenga,

Poleni twawatumia, tena bila kujivunga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Maneno yaniishia, sina tena la kubonga,

Kilobaki kumwombea, ndugu yetu na malenga,

Mola kutakabalia, dua zetu kutopinga,
Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

ISMAIL BAKARI

(Swila Mchiriza Sumu)

NAIROBI.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

 

 

MLAZE PEMA BABU

Kariakor, Nairobi

Marafiki na ndugu zake mwandishi Omar Babu wakiwa wamebeba maiti yake kuelekea makaburi ya Kariakor, Nairobi Januari 21 2015. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na FOCUS KAWA MWANDEMBO

Imepakiwa - Thursday, January 22  2015 at  12:00

Kwa Muhtasari

Shaha akatutokeko, dunina kaiagako,

Roho yake Marjani, Ilazwe pema peponi.

 

LIMEFIKA tamauko, pamoja nalo  payuko,

Hanasi tena hayuko, Omar babu hayuko,

Shaha akatutokeko, dunina kaiagako,

Roho yake Marjani, Ilazwe pema peponi.

 

Uga tunahangaiko, kustahimili mauko,

Mwalimu nasi hayuko, michangoye metokeko,

Rabana ulikueko, sasa nakuhisi uko,

Roho yake Marjani, ilazwe pema peponi,

 

Mtima una vurugiko, ni mazito maondoko,

Nayakumbuka matamko, alie nifundisheko,

Nitoe zangu mihemko, japo tunapo lumbako,

Roho yake Marjani, ilazwe pema peponi.

 

Nakisitisha kimako, chozi nikalifuteko,

Omar kutokuwako, kwa fani hii nipiko,

Jalia uso yumbako, wajua zote chimbuko,

Roho yake Marjani, ilazwe pema peponi.

 

 

FOCUS KAWA MWANDEMBO,

'Kombora Kombeoni',

Wundanyi-Taita.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

 

 

MSIBA ULOTUFIKA

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na EDISON WANGA

Imepakiwa - Thursday, January 22  2015 at  11:46

Kwa Muhtasari

Hatuwezi kususia, kifo ni tangu wa tangu,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

YA Illahi Jalalia, Muumba wa nchi na mbingu,

Kwa yaliyotufikia, kukubali ni uchungu,

Hatuwezi kususia, kifo ni tangu wa tangu,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Mtimani naumia, msiba ulotufika,

Siwezi kujizuia, mat'ozi kutiririka,

Umeenda pasi nia, ja mwizi ukatoroka,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Ulivyonisaidia, nakumbuka ndugu Babu,

Yeyote hukubagua, 'limfunza taratibu,

Siwezi kusingizia, uliyotenda sahibu,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marjani.

 

Kwa asilimia mia, ni wengi walikupenda,

Wataukosa wasia, kwa huzuni wakishinda,

'Lokuwa ukitetea, Kiswahili ushakwenda,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Umeacha familia, mke na wana wadogo,

Wote wanakulilia, umewapa kipigo,

Babu umewakimbia, haupo tena kigogo,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Omari Babu sikia, ulikokwenda ahera,

Nitafwata zako njia, mtazamo na taswira,

Haikuwa yangu nia, kifo kije kukupora,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Natamati nikilia, mkono unatetema,

Edi nikifikiria, ulonitendea wema,

Simanzi menizidia, kwanilemea kuhema,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marjani.

 

EDISON WANGA,

Son Bin Edi,

Mwana wa Mambasa.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

 

 

AMETUAGA OMAR BABU

Kariakor, Nairobi

Marafiki na ndugu zake mwandishi Omar Babu wakiwa wamebeba maiti yake kuelekea makaburi ya Kariakor, Nairobi Januari 21 2015. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na JAMES MUTWIRI WANJAGI

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  19:42

Kwa Muhtasari

Alo msomi aali, gonjwa kamfanya tuli,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

KIFO Babu mekabili, kamtwaa kikatili!

Abu Marjan ukweli, katunga kidijitali,

Kighafula ja ajali, ye kafa pasipo swali,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Alo msomi aali, gonjwa kamfanya tuli,

Kamwe aso uzohali, kasomeya uzamili,

Alolonga kulihali, jambo lugha kajadili,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Katangaza kiwa mbali, sauti tamu dalili,

Mshairi kwelikweli, shairi jadi shughuli,

Lugha mustakabali, kapenda kama asali,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Jamani gani kauli, kuibwa Nguli kamili?

Mtunzi kote mahali, twaomboleza halali,

Jukwaani mbalimbali, akaghani si kalili,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Akawa Mcheshi kali, kuandika hakufeli,

Kubuni yake amali, kukazana kakubali,

Aliyapinga madhili, malenga aso bahili,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Ujerumani mahali, kapambana ja fahali,

Kaonyesha kiakili, tungoze ziso mithili,

Waama kajua ngeli, kaeneza Kiswahili,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Katu hakuchoka mwili, ubunifu alijali,

Jagina kwetu twakuli, amfadhili Jalali,

Mwandishi tutaamali, hongera asitahili,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Ninawaomba kibali, utunzi nt’ie kufuli,

Kapata tele medali, tungo zake afadhali,

Kiswahili lo jabali, galacha kote angali,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

JAMES MUTWIRI WANJAGI,

'Malenga Msifika'

 Chuka-Tharaka Nithi.

 

 

AII! BOB OKOTH TENA?

Bob Okoth

Bw Bob Okoth. Picha/HISANI  

Na LUDOVICK MBOGHOLI

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  19:30

Kwa Muhtasari

Mhariri mtajika, wa zama Taifa Leo,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Kifo cha Bob Okoth, nacho kilinisakama,

Kilinishukisha hadhi, mwili ukanitetema,

Nilidhani ni hadithi, gazeti niliposoma,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Kwa hakika kifo chake, moyoni kiliniuma,

Nilijihisi mpweke, kama kipande cha nyama,

Kidogo tu nianguke, sikwona mbele na nyuma,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Mbogholi nilishtuka, moyo ukanenda mbio,

Mhariri mtajika, wa zama Taifa Leo,

Ghafula katuondoka, hatuoni mwelekeo,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Nnakumbuka miaka, ilopita zama zake,

Hakujali matabaka, wala mume au mke,

Sote tulichanganyika, waandishi chini yake,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Bwana Bob mhariri, nyaka hizo zilopita,

Alipenda washairi, na wanamaoni hata,

Wanasalamu mahiri, pamoja na maripota,

Namlia bwana Bob , kumbe hayu nasi tena!

 

Bob alikuwa gwiji, kipenzi cha wote hata,

Alienzi wasomaji, wanachama wa WAKITA,

Akawa ni msemaji, wa kuzima vutavuta,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Enzi ya Hamisi Keya, mwenyekiti wa WAKITA,

Bob alikuwa geya, chama kukivutavuta,

Kiweze kuendeleya, Taifa Leo kumeta,

Namlia bwana Bob , kumbe hayu nasi tena!

 

Namkumbuka Opundo, mwanamaoni wa zama,

Alikizusha vishindo, akiwa ndani ya chama,

Bob akasema bado, WAKITA itasimama,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Walofata nyayo zake, ushauri walopawa,

Waume na wanawake, walokuwa na vipawa,

Leo hii teketeke, ni mabingwa wamekuwa,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Hapano nipumzike, kwa kufika kaditama,

Siandiki nitosheke, alazwe peponi pema,

Kwasababu kifo chake, Bob sote chatuuma!

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

LUDOVICK MBOGHOLI

'Al-Ustadh-Luqman Ngariba-Mlumbi'

Taveta-Bura / Ndogo.

 

 

ILLAHI TUHIFADHIE

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na ALAMIN SIWA SOMO

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  19:21

Kwa Muhtasari

Alikuwa ni mteshi, sikizani niwambie.

Amehama Ulimwengu, Omar katuondokea.

 

KADARA Mghani wangu, nakuomba nighanie,
Shairi la ndugi yangu, lighani nilisikie,
Ijapo nina utungu yabidi nivumilie,
Amehama Ulimwengu, Omar katuondokea.

 

Alikuwa ni mteshi, sikizani niwambie,
Hakupenda ya ubishi, upole ndio kazie,
Kamtwaa mwenye Arshi, Illahi Muumba yeye,
Kweli maisha ni moshi, ni nani atabakia.

 

Tulikuwa marafiki, ninaweleza mujue,
Katika kitabu hiki, kitachotoka badae,
Nawambia muswadiki, Somo nimetunga nae,
Amemtwaa Razaki, Illahi Mola Jalia.

 

Sina hamu ya kutunga, na kiu inishishie,
Kwa kuwa wetu Malenga, hivi sasa siko nae,
Illahi Muumba anga, twaomba tuhifadhie,
Kwa pepo zenye na kunga, Upate tuingizia.

 

Zatosha beti kidogo, heri hapa niishie,
Mithili pande la gogo, msiba umetungie,
In Sha Allah wake mzigo, kwa kuliani apawe,
Ili awe na vigogo, Swahaba na Tumwa Nabia.

 

Illahi ninakuomba, naomba nikubalie,
Uumfanyie wembamba, kaburini na badae,
Meupe kuliko pamba, kwa maisha yake yawe,
Na kaburi liwe nyumba, ya pepo ya kuvutia.

ALAMIN SIWA SOMO

'Malenga wa Mombasa'
Chuo Kikuu cha Kenyatta

Mombasa. 

 

 

BURIANI MARIJANI

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na GITAA HERMAN ANGWENYI

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  19:11

Kwa Muhtasari

Mangi ulinifundisha, Lugha ngeli na mitungo,

Buriani marijani, Mola kakulaze pema!

 

UMETUFIKA msiba, watunzi tunatetema,

Mauko yamemuiba, ndu' yangu ninalalama,

Katangulia kwa baba, ni wapi tutaegema,

Buriani Marijani, Mola kakulaze pema!

 

Mangi ulinifundisha, lugha ngeli na mitungo,

Kifo umekaribisha, tutakosa viambajengo,

Japo menitamausha, hutotoka langu bongo,

Buriani Marijani, Mola kakulaze pema!

 

Tanzia nikapokea, mwanzo sikuziamini,

Ja kitoto nikalia, nikimlani shetwani,

Moyo zikaniatua, dawamu umo kitwani,

Buriani Marijani, Mola kakulaze pema!

 

Watunzi ulikubali, toka bara pia pwani!

Katu huna mushekili, Mola kutunze peponi,

Vitabu vya Kiswahili, na tungozo tazighani,

Buriani Marijani, Mola kakulaze pema!

 

Limenilemea tozi, kwendeleya numeshindwa,

Manipiku michirizi, mtima umeshapondwa,

Omar Abu mwuguzi, uliko juwa wapendwa,

Buriani Marijani, Mola kakulaze pema!

GITAA HERMAN ANGWENYI

 'Mlawandovi Malenga'

Migombani- Nyancha.

 

 

KWAHERI OMAR BABU

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na MWALIMU STEPHEN DIK

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  19:04

Kwa Muhtasari

Kwanza ni mwanzaji, mwisho ni kwa muishaji,

Kwaheri Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

KWANZA ni mwanzaji, mwisho ni kwa muishaji,

Kifo chako ewe gwiji, kwa kweli sikutaraji,

Kilio kwa mtungaji, wa mijini na vijiji,

Kwaheri Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

La sivyo tunakumbuka, wosia ulotuacha,

Lidunde libingirike, jikombora limechacha,

Litupwe na lisiwake, likeshe usiku kucha,

Lala pema Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

Mlo hai sisahau, umoja wetu ndo' nguvu,

Mtu awe akijua, maisha ni kama povu,

Miaka nayo ni ua, mwili wetu ni majivu,

Milele Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

Naandika ukurasa, napiga nduru kichizi,

Naenda nikipapasa, maneno sizungumzi,

Ni Marjan kwa sasa, amaliza matembezi,

Nenda hima Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

Om shanti wa shanti, kaditama wa tamati,

Ole wako we mauti, ningakuvua makoti,

Ondoka kwetu mauti, sura mbaya we mauti,

Ohh nalia Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

MWALIMU STEPHEN DIK,

'Mpenda Ushairi',

Siaya.

 

 

KIFO SOTOA FIDIA!

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na PHIBBIAN MUTHAMA

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  18:46

Kwa Muhtasari

Ni hisia sauti, yake Abu Marijani,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

 

ACHUKUWA kilazima, yeyote amemnyamaa,

Mchangamfu azima, na mwili kumlemaa,

Kwa jeuri na dhuluma, ukatili mekujaa,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

 

Miajali zafanyika, timizie zako mbovu,

Mindwele kali yashika, wasafi waso ovu,

Wako umedhihirika, unapokonya kwa nguvu,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

 

Kwetu watupa daraja, ukisifiye mauti,

Hasa kunapo faraja, wenda chini kwa magoti,

Wona bahati ya luja, tunapochimba mafuti,

Ole wako wachukuwa paso naya kaisari.

 

Kifo huoni huruma! Kichukuwa na wakongwe,

Nyoyoni unatuvama, sowacha dogo vilembwe,

Waja mbele, pia nyuma, haidhuru ndo mizengwe,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

Laiti ungalijuwa, usingalifanya jauri,

Lakini  kesho tajuwa, ya Mola tekwa dhahiri,

Kwako njiya wapitiwa, nasi tungo la shairi,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

 

Kifo nakueleza, kwa wangu utungoni,

Mwawazi takugeuza, tuweke sini maishani,

Asilani wone kiza, tukiwa paradisoni,

Ole wako wachukuwa, pasi naya kaisari.

 

Ni hisia sauti, yake Abu Marijani,

Yalotupata mauti, Jumanne ishirini,

Mgumu hunu wakati, tuwepushiye Manani,

Ole wako wachukuwa, paso naya kaisari.

PHIBBIAN MUTHAMA

'Malenga Mlezi'

 

 

MOLA AMLAZE PEMA!

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na BISMARCK KIMANGA

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  18:36

Kwa Muhtasari

Ninasoma gazetini, hayupo tena Omari,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

NINASOMA gazetini, hayupo tena Omari,

Mwenye tungo za makini, nzito na zenye urari,

Daima mwenye hisani, asiyependa kiburi,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

Ndugu yangu Marijani, ameifunga safari,

Kasifika kwa yakini, mkufunzi mashuhuri,

Mwenye nyingi samahani, sumile pia kaburi,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

Nashindwa kuamini, nimebaki ghururi,

Kanilea kwenye fani, na kunipa ushauri,

Meondoka duniani, Babu asopenda shari,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

Chuoni na vitabuni, fasihi ikanawiri,

Kama  ‘Ndoa ya Samani’, ‘Heri Subira’ nakiri,

‘Kala Tufaa’ jamani, nayo mengi mashairi,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

Metangulia njiani, amekwenda kwa Qahari,

Hayumo tena kundini, imemmeza kaburi,

Ametuacha mwendani, kaenda pasi kwaheri,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

Umekatika uneni, meniisha sitari,

Nalia ndani kwa ndani, zahuzunisha habari,

Kalamu naweka chini, machozi kama bahari,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

BISMARCK KIMANGA

'Malenga Mwadilifu'

Rongai -Nakuru.

 

 

MSILILIE MARIJANI

Kariakor, Nairobi

Marafiki na ndugu zake mwandishi Omar Babu wakiwa wamebeba maiti yake kuelekea makaburi ya Kariakor, Nairobi Januari 21 2015. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na MAIYO BIN MAIYO

Imepakiwa - Thursday, January 22  2015 at  14:25

Kwa Muhtasari

Tukiuliza kwa nini, atayejibu ni nani?

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

AMETUACHA Marijani, so rahisi kuamini,

Hakupunga buriani, atuweke tayarini,

Tukiuliza kwa nini, atayejibu ni nani?

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Kudura zake Manani, hainani walakini,

Na ijapo ni huzuni, nawaomba kubalini,

Na ninyi tafakarini, hatima yenu ni lini?

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Alinena darasani, marehemu Marijani,

Akafunza ukumbini, hapa petu gazetini,

Kunga zake maishani, ziwe funzo mwafulani,

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Keshafika ukingoni, napo mwisho aushini,

Katu siseme haneni, akiwapo kaburini,

Alondika vitabuni, yanasema na wendani,

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Kazuru ughaibuni, mswahili uzunguni,

Katamba Ujerumani, sikwambii Marekani,

Akafundisha vyuoni, Fasihile kama nini,

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Roho zenu lilieni, ufufuo u njiani,

Waingiao mbinguni, ni wenye haki yamini,

Jisaili mtimani, taingia pande gani,

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Nimetimiza kanuni, za kuzijenga mizani,

Na laziada sinani, naondoka kwa huzuni,

Makiwa enyi wapwani, na wenye lugha barani,

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

MAIYO BIN MAIYO

'Malenga Wa Kiplombe'

Chuo Kikuu cha Baraton.

 

 

 

KIFO KIMEATUWA MIOYO

Kariakor, Nairobi

Marafiki na ndugu zake mwandishi Omar Babu wakiwa wamebeba maiti yake kuelekea makaburi ya Kariakor, Nairobi Januari 21 2015. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na RICHARD  MAOSI

Imepakiwa - Wednesday, January 21  2015 at  17:25

Kwa Muhtasari

“Mti mkuu kugwaa, viyoyo tu mashakani,

Kifo cha Omar Babu, kimeatua mioyo.”

 

AMEKWENDA kaburini, baba yetu wa fasihi,

Keshazima zake mboni, mekuja kutanabahi,

Kujiunga mavumbini, muwandishi wa tarihi,

Kifo cha Omar Babu, kimeatuwa mioyo.

 

Mti mkuu kugwaa, viyoyo tu mashakani,

Yamebakia mawaa, kulizana maskani,

Shehe wetu hukufaa, kuondoka duniani,

Kifo cha Omar Babu, kimeatua mioyo.

 

Yamemteka mauti, mshairi wa nudhuma,

Ale shika madhubuti, kiwa mesimama wima,

Leo hayupo hayati, imetuvaa nakama,

Kifo cha Omar Babu, kimeatua mioyo.

 

Mchangizi hatunasi, mekuwa mwalimu wangu,

Meuona ufanisi, Ulaya mekuwa tangu,

Waima sio kukisi, yametufika machungu,

Kifo cha Omari Babu, kimeatua mioyo.

 

Mwalimu nenda salama, pumzikoni makiwa,

Tunaukwea mlima, huko sote tutakuwa,

Mana haina ulama, mauti yanapotuwa,

Kifo cha Omari Babu, kimeatua mioyo.

 

Hazina ulonifunza, sitowacha kuishika,

Yote uliyoyakinza, utabaki kutajika,

Wasanii ulitunza, na vitabu kuandika,

Kifo cha Omari Babu, kimeatua mioyo.

 

Ndani ya Damu Nyeusi, ndoa yako ya samani,

Mikusanyiko sisisi, mathalani ni diwani,

Heri subira sikosi, ulivosema mneni,

Kifo cha Omar Babu, kimeatua mioyo.

 

RICHARD  MAOSI

"Amiri Kidedea"

Rovy Girls High School,

Nakuru.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

 

 

MTUNZI OMAR BABU

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na JUMA NAMLOLA

Imepakiwa - Wednesday, January 21  2015 at  10:58

Kwa Muhtasari

Kazi yake Rahamani, kwa Omari ‘metimia,

Tumuage kwa heshima, mtunzi Omari Babu.

 

WASHAIRI pulikani, huzuni imeningia,

‘Menipotea uneni, Namlola ninalia,

Kazi yake Rahamani, kwa Omari ‘metimia,

Tumuage kwa heshima, mtunzi Omari Babu.

 

Tulijuana zamani, mashairi kichangia,

Tukawa sote kazini, Nation akifanyia,

Hadi kenda Jerumani, lugha kuipalilia,

Tumuage kwa heshima, mtunzi Omari Babu.

 

Na vitabu madukani, ukenda kuulizia,

Hutakosa japo thani, alivyotuandikia,

Mimi naye kwenye fani, pamoja tumechangia,

Tumuage kwa heshima, mtunzi Omari Babu.

 

Beti zenu gazetini, Jumamosi nategea,

Mkono wa buriani, tupate kumpungia,

Sote tumo safarini, yeye ametangulia,

Tumuage kwa heshima, mtunzi Omari Babu.

 

JUMA NAMLOLA,

"Hakimu wa Mashairi"

S.L.P 49010 - 00100

Nairobi, Kenya

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

AMEONDOKA MHENGA

Kariakor, Nairobi

Marafiki na ndugu zake mwandishi Omar Babu wakiwa wamebeba maiti yake kuelekea makaburi ya Kariakor, Nairobi Januari 21 2015. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na NUHU ZUBEIR BAKARI

Imepakiwa - Wednesday, January 21  2015 at  18:02

Kwa Muhtasari

Umetuwacha mhenga, akusetiri Jalali,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani.

 

TUMEPOTEZA Swahiba, muandishi mashuhuri,

Mtu na zake haiba, mtunzi wa mashairi,

Umetufika msiba, mwenzetu Babu Omar,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Umetangulia sweba, amekuita Kahari,

Tunalia kwa msiba, metuwacha Jemedari,

Tunakuvika vikuba, ili ikufike zari,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Tungo ulizozitunga, na riwaya tumbitumbi,

Ziliibua kinganga, kwenye za watunzi kumbi,

Meenda ngali mchanga, tutaku-misi walumbi,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Michango uliyochanga, kwa lugha ya Kiswahili,

Metoa nuru na mwanga, katika janibu hili,

Umetuwacha mhenga, akusetiri Jalali,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Uende hadi peponi, aliko mtume wetu,

Katika mabustani, ya mitende na misitu,

Akufae Rahmani, Mungu muumbaji wetu,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Kaka umetangulia, bado ungali kijana,

Umeiwacha dunia, meenda kwa Marjana,

Leo tunaomba dua, iwe ni yako hazina,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Hapa mefika hatwima, nakamilisha kutunga,

Ulale mahala pema, ewe Omar mhenga,

Kifo kwetu ni lazima, mja hawezi kupinga,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

NUHU ZUBEIR BAKARI

“Al-Ustadh Pasua”

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

 

 

KIFO CHA MARIJANI PIGO

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na NYAMWARO O'NYAGEMI

Imepakiwa - Wednesday, January 21  2015 at  09:27

Kwa Muhtasari

Angengoja ziraili, Marijani awe babu,
Akitutiya makali, Kiswahili Kiarabu,
Kifo chake shaha 'Abu, ni mjeledi mkali!

 

KIFO umetukatili, kutwaa Omar Babu,
Mwalimu wetu wa kweli, maswali yetu kujibu,
Kwangu kanitowa mbali, nikiwa mbumbumbu bubu,
Kifo cha Omari Babu, ni pigo kwa Kiswahili,

Ni pigo kwa kiswahili, kifo cha Omar Babu,
Angengoja ziraili, Marijani awe babu,
Akitutiya makali, Kiswahili Kiarabu,
Kifo chake shaha 'Abu, ni mjeledi mkali!

Ni mjeledi mkali, kifo cha Omar Babu,
Litungia hoja kali, kanifanya mraibu,
Misamiati asali, ni ushairi wa Abu,
Lingoja tungo za Babu, Jumamosi jumapili!

Jumamosi Jumapili, lingoja tungo za Babu,
Taifa Leo faili, zake ni tele za Abu,
Omar mtajamali, leo kifo kamsibu,
Muandishi wa vitabu, mtuzwa kwao na mbali!

Mtuzwa kwao na mbali, uandishi wa vitabu,
Mwaka wa elfu mbili, ni mwanahabari 'Abu,
Ujerumani ni mbali, huko katangaza Babu
Saratani kakusibu, kakulaza sipitali!

Kakulaza sipitali, saratani kakusibu,
Si mara moya si mbili, linambiya shehe 'Abu,
Tumbo lauma vikali, wapokezwa matibabu,
Kumbe waondoka Babu, vipi tutalikubali?

Vipi tutalikubali, kuondoka kwako Babu?
Mjane wana wawili, kifo kimewaghusubu,
Nawasihi sende mbali, nayo jamii ya 'Abu,
Yanitoka ndiya mbili, matozi nalia Babu!

NYAMWARO O'NYAGEMI
"Malenga wamigombani"
Verce Ndumberi High-Kiambu.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

PENGO KUBWA LITABAKI

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na KIMANI WA MBOGO

Imepakiwa - Wednesday, January 21  2015 at  12:21

Kwa Muhtasari

La mno limetukia, katukumba ukumbini,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

 

HUMU tu wapita njia, kesho haijulikani,
Majonzi limetutia, likatanda la huzuni,
La mno limetukia, katukumba ukumbini,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Imetuchukua muda, jambo hili kukubali,
Tumefikwa nayo shida, wapenzi wa Kiswahili,
Twakumbuka zako mada, lugha ulivyoijali,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Pakubwa ulichangia, bidii zako mwalimu,
Pengo umetuwachia, pote ulipohudumu,
Kwa mengi umepitia, ughaibuni na humu,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Ulinifunza kutunga, fani nikaibaini,
Lugha hukuiboronga, ulivyokuwa makini,
Kusarifu ulilenga, lugha ulivyotamani,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Vitabu uliandika, kumbukumbu itakuwa,
Vitabaki kusomeka, daima kuenziwa,
Upesi umetoweka, mauti kukuchukuwa,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Sana ulinyenyekea, na bora hukujiona,
Wengi ulitembelea, urafiki ukafana,
Sifa zilivyoenea, zilifika kila kona,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Ilikujaa hekima, njema hiyo kufaana,
Pafaapo ulisema, wingi wa busara tena,
Nitaukumbuka wema, mazuri yako kwa kina,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Kifo ni adui kweli, hunyakua walo wema,
Tupendao hukabili, wazuri waliovuma,
Kifo hugeuza hali, yalo mema yakakoma,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

 

KIMANI wa MBOGO

Mwanagenzi Mtafiti

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

BURIANI ABU

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na ISMAIL BAKARI

Imepakiwa - Thursday, January 22  2015 at  13:08

Kwa Muhtasari

Alikuwa maridhia, si mtu mwenye kuringa,

Na asingeshabikia, lugha ukiiboronga

 

KILIO tunacholia, kimetanda kwenye anga,

Wengi mmeshasikia, kilotufika kisanga,

Abu ametukimbia, sasa tunalegalega,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Si rahisi kwitikia, kukubali hili janga,

Hasa ukizingatia, juzi tukiwa twalonga,

Kwenda kumsalimia, Omar kumwengaenga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Hayo yameshatukia, hakuna wakuyapinga,

Na kazi yake jalia, si ya mavangamavanga,

Msizue yakuzua, maneno kuungaunga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Mwalimu mulimjua, ni bingwa wa umalenga,

Vipindi alichangia, kwa radio na runinga,

Wengi vikawaingia, kuwatoa ushambenga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Vitabu katwandikia, vyenye tungo zenye kunga,

Na vya Kiswahili pia, riwaya zenye muanga,

Vyote vimesaidia, kuongoza vijulanga,
Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Alikuwa maridhia, si mtu mwenye kuringa,
Hakupenda kupapia, mambo yasiyomlenga,

Na asingeshabikia, lugha ukiiboronga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Nataka kuwahusia, kina manju na malenga,

Japo ameshakimbia, hatupo naye mkunga,

Fuateni zake njia, na ninyi muwe wahenga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Maswahiba na insia, jamaa na wamachinga,

Mwaombwa kuvumilia, wala sio kujitenga,

Poleni twawatumia, tena bila kujivunga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Maneno yaniishia, sina tena la kubonga,

Kilobaki kumwombea, ndugu yetu na malenga,

Mola kutakabalia, dua zetu kutopinga,
Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

ISMAIL BAKARI

(Swila Mchiriza Sumu)

NAIROBI.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

 

 

MLAZE PEMA BABU

Kariakor, Nairobi

Marafiki na ndugu zake mwandishi Omar Babu wakiwa wamebeba maiti yake kuelekea makaburi ya Kariakor, Nairobi Januari 21 2015. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na FOCUS KAWA MWANDEMBO

Imepakiwa - Thursday, January 22  2015 at  12:00

Kwa Muhtasari

Shaha akatutokeko, dunina kaiagako,

Roho yake Marjani, Ilazwe pema peponi.

 

LIMEFIKA tamauko, pamoja nalo  payuko,

Hanasi tena hayuko, Omar babu hayuko,

Shaha akatutokeko, dunina kaiagako,

Roho yake Marjani, Ilazwe pema peponi.

 

Uga tunahangaiko, kustahimili mauko,

Mwalimu nasi hayuko, michangoye metokeko,

Rabana ulikueko, sasa nakuhisi uko,

Roho yake Marjani, ilazwe pema peponi,

 

Mtima una vurugiko, ni mazito maondoko,

Nayakumbuka matamko, alie nifundisheko,

Nitoe zangu mihemko, japo tunapo lumbako,

Roho yake Marjani, ilazwe pema peponi.

 

Nakisitisha kimako, chozi nikalifuteko,

Omar kutokuwako, kwa fani hii nipiko,

Jalia uso yumbako, wajua zote chimbuko,

Roho yake Marjani, ilazwe pema peponi.

 

 

FOCUS KAWA MWANDEMBO,

'Kombora Kombeoni',

Wundanyi-Taita.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

 

 

MSIBA ULOTUFIKA

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na EDISON WANGA

Imepakiwa - Thursday, January 22  2015 at  11:46

Kwa Muhtasari

Hatuwezi kususia, kifo ni tangu wa tangu,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

YA Illahi Jalalia, Muumba wa nchi na mbingu,

Kwa yaliyotufikia, kukubali ni uchungu,

Hatuwezi kususia, kifo ni tangu wa tangu,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Mtimani naumia, msiba ulotufika,

Siwezi kujizuia, mat'ozi kutiririka,

Umeenda pasi nia, ja mwizi ukatoroka,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Ulivyonisaidia, nakumbuka ndugu Babu,

Yeyote hukubagua, 'limfunza taratibu,

Siwezi kusingizia, uliyotenda sahibu,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marjani.

 

Kwa asilimia mia, ni wengi walikupenda,

Wataukosa wasia, kwa huzuni wakishinda,

'Lokuwa ukitetea, Kiswahili ushakwenda,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Umeacha familia, mke na wana wadogo,

Wote wanakulilia, umewapa kipigo,

Babu umewakimbia, haupo tena kigogo,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Omari Babu sikia, ulikokwenda ahera,

Nitafwata zako njia, mtazamo na taswira,

Haikuwa yangu nia, kifo kije kukupora,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Natamati nikilia, mkono unatetema,

Edi nikifikiria, ulonitendea wema,

Simanzi menizidia, kwanilemea kuhema,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marjani.

 

EDISON WANGA,

Son Bin Edi,

Mwana wa Mambasa.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

 

 

BURIANI MARIJANI

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na BENSON NYALE

Imepakiwa - Thursday, January 22  2015 at  11:19

Kwa Muhtasari

Kifo chako Marijani, wengi tumeshitukiya,

Kule kwetu ukumbini, kilio umetwachiya

 

BARA hadi visiwani, habari tulipokeya,

Kwa huzuni mioyoni, mwendani kuondokeya,

Kattu hatujaamini, Abu umetanguliya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Kulla pahala huzuni, sute tunaluliliya,

Kifo chako Marijani, wengi tumeshitukiya,

Kule kwetu ukumbini, kilio umetwachiya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Utasaliya nyoyoni, japo umetanguliya,

Ndugu Abu Marijani,mangi katufunuliya,

Kote makongamanoni, lugha uliichangiya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Soteni tumo ndiani, kwa Mola tatarejeya,

Tuishipo duniani, imani twashikiliya,

Si kwetu ulimwenguni, vumbini tunarejeya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Ninautungu moyoni, nashindwa kuvumiliya,

Katutoka Marijani, mwalimu wa kwaminiya,

Mweledi wa hino fani, sote tulitumaniya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Kalale pema peponi, Abu umetanguliya,

Wino wako vitabuni, daima utasaliya,

Naswi twendapo dukani, wanetu twanunuliya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Kuna pengo ukumbini, nani tashuhulikiya,

Tu makiwa wana fani, tumebakiya kuliya,

Meondoka Marijani, kilio katwachiya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Mlezi we Marijani, salama twakutakiya,

Ulazwapo kaburini, Mola tunakuombeya,

Amekuita Manani, nawe ukaitikiya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Litufaa Marijani, hilo ninashuhudiya,

Sio hapa ukumbini, chipukizi 'lituleya,

Mshairi we mwendani, welekezi litupeya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

BENSON NYALE

"Sauti ya Mbali"

Nakuru.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

 

 

WAGANGA MNA NINI!

Mganga ajaribu kufufua

Mganga Samuel Kanundu (akiwa na nguo nyekundu) awahutubia wanahabari katika kijiji cha Mwazaro, Shimoni Januari 09, 2015 akiwa katika shughuli ya kujaribu kufufua Dominic Kyalo aliyefariki Oktoba 2013. Picha|FAROUK MWABEGE  

Na NYAMWARO O'NYAGEMI

Imepakiwa - Tuesday, January 13  2015 at  16:12

Kwa Muhtasari

Enzi ya utandawazi, kwa wengine tandawizi,

Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

 

WAGANGA wa mitishamba, Afrika mashariki,

Itaneni kwenye chemba, na gumzo mshiriki,

Sio la watu kuchimba, ni nyie kujihakiki,

Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

 

Nimechunguza kwa muda, madai ya ndugu Duba,
Shehe Abduba Dida, yakini mchungu mwiba,
Waganga wengi ni shida, au imani ndo haba?
Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

 

Lilikuja zee lile, maarufu la Loliondo,
Mbelekile Mwashavile, mganga mwenye huondo,
Waja kanywa dawa ile, kafaulu lake windo,
Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

 

Enzi ya utandawazi, kwa wengine tandawizi,
Matangazo kote wazi, hipo ndwele hamuwezi,
Mmepotosha kizazi, kikongwe na chipukizi,
Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

 

Wengine ni wanajimu, ya kesho kuyabashiri,
Kumbe ni kupika sumu, matapeli wajeuri,
Hawachagui msimu, lengo wawe matajiri,
Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

 

Wajitanua vifua, nguvu kufufua wafu,
Kulisimamisha jua, kwa uwezo mtukufu,
Hatuachwi kupumua, wamepora maelfu,
Twambie nani mkweli, na nani ni mtapeli!

Zangu saba zimetosha, beti natia kufuli,
Ama kweli mnatisha, wasoamini Jalali,
Komesha zenu tamasha, mche Mungu tafadhali,
Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

NYAMWARO O'NYAGEMI

“Malenga wa Migombani”

Kiambu Mjini

 

 

KATI YA SURA NA TABIA

Wachumba

Wachumba wakiwa wamejawa na furaha. Picha/FOTOSEARCH 

Na BENSON NYALE "SAUTI YA MBALI"

Imepakiwa - Thursday, December 11  2014 at  16:55

Kwa Muhtasari

Nawauza n'anueni, weledi wa haya mambo, Kati ya sura, twabiya, ni ipi huja ya kwanza?

 

Nawauza n'anueni, weledi wa haya mambo,
Mwenzenu niko gizani, sielewi hili jambo,
Ingawa ninatamani, naogopa kwenda kombo,
Kati ya sura, twabiya, ni ipi huja ya kwanza?

Watu hupenda twabiya, japo huwa ya sirini,
Vipi wapende tabiya, ilhali hayonekani?
Sivyo livyo tarajiya, bado ningali gizani,
Kati ya sura, twabiya, ni ipi huja ya kwanza?

Siishi kutafakuri, bado niko pale pale,
Jambo hili nafikiri, niwaendee wavyele,
Wakanipe ushauri, maozi wanifumbule,
Kati ya sura, twabiya,ni ipi huja ya kwanza?

Kabla nende kwa wavyele, nawauliza wajuzi,
Mkishindwa nendembele, niweze kuyua wazi,
Ni ipi huja kimbele, s'elewi mie wayuzi,
Kati ya sura, twabiya, ni ipi huja ya kwanza?

Tamati nahitimisha, shairi kuliandika,
Kalamu ninaishusha, nudhumu meandikika,
Pumzi ninazishusha, sauti imepazika, Kati ya sura, twabiya,ni ipi huja ya kwanza?

BENSON NYALE
"Sauti ya Mbali"
Nakuru.

Tuma mchango wako kwa: swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

MANDERA KULIKONI

Mamia Mandera wakimbilia pahala salama

Raia wasio wa asili ya Kisomali wakusanyika katika uwanja wa ndege wa Mandera Novemba 25, 2014 wakihofia kurudi makwao baada ya basi kushambuliwa na watu 28 kuuawa. Picha/MANASE OTSIALO 

Na JAMES MUTWIRI

Imepakiwa - Saturday, December 6  2014 at  17:47

Kwa Muhtasari

Mandera ya waziwazi, mikosi na mavamizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera tujue juzi, do! Yalotanda machozi,

Mandera wahedi mwezi, vifo mekita mizizi,

Mandera ya waziwazi, mikosi na mavamizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera ushambulizi, Jumamosi angamizi!

Mandera lojibarizi, kwa basi ndo uvamizi,

Mandera ndo ombolezi, kafa belele walezi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera i matembezi, waama siyo mapozi,

Mandera i bumbuazi, kafa wachapaji kazi,

Mandera nyi wasikizi, ni majonzi siku hizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera hatujiwezi, dunia hi vinywa wazi,

Mandera i unyakuzi, wa roho mi sinyamazi,

Mandera kuntu tatizi, mezuka janga tukizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera la uchukuzi, basi katekwa uwazi,

Mandera ndo ukatizi, wa aushi ndo telezi,

Mandera walo wajuzi, kauliwa kichokozi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera nyi viongozi, mwiletee ukombozi,

Mandera yalo wokozi, tendwe pasi ubaguzi,

Mandera twomba tulizi, ndo usalama tetezi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

JAMES MUTWIRI WANJAGI,

“Malenga Msifika”,

CHUKA, Tharaka Nithi

 

Tuma mchango wako kwa: swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

UBAKAJI USHINDWE

Na JAMES MUTWIRI

Imepakiwa - Saturday, December 6  2014 at  17:47

Kwa Muhtasari

Rijali liso utu chembe, kiusena lawazuga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

MEAMUWA nisifumbe, kitendawili kutega,

Ninene wazi ujumbe, fahamu kinaganaga,

Ndo nazatiti kabambe, kuyataja bila woga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Nina vigoli wakembe, kuwatilia ja boga,

Rijali liso utu chembe, kiusena lawazuga,

Kalilazimisha jembe, kondeni kulivuruga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Waso hiari viumbe, nduli tundalo kumega!

Wali tosa maembe, ndanimo kuwakoroga,

Vipi kero situkumbe, geuzwa karaha uga?

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Shani watoma halumbe, kutesa waliofuga!

Wawadaka wawarambe, maeneo yalo viga,

Kuso mianya wachimbe, wakidai ni shuga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Vigoli tele niambe, mebakwa kawa mzoga,

Maradhi yasio tembe, najisiwa mekanyaga,

Majuto mesali kumbe! Dunia teke wapiga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Tuwapatie uvimbe, wajulikane chambega,

Tuwatie ja vikombe, baada ya kuwatoga,

Juujuu tuwasombe, hadi jela kuwachega,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Kike sigeuze ng’ombe, kiimla kuwasaga,

Sheria kali itambe, wadhalimu kuwatega,

Ikatekate ja wembe, wapate kugugayuga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Hili la kichwa tuvimbe, lisendelee kutaga,

Ubakaji tusiimbe, tupige kondo wakwiga,

Mkawini tumuombe, ya shwari ya omega,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Malenga niso uzembe, wasikizi nawaaga,

Mepuliza hii pembe, ujumbengu meuaga,

Kiumbe kike tupambe, ili wapate kunoga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

JAMES MUTWIRI WANJAGI,

“Malenga Msifika”,

 CHUKA - Tharaka Nithi

 

Tuma mchango wako kwa: swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

KIMAKONDE SI KINGINDO

Na WILSON NDUNG’U

Imepakiwa - Saturday, December 6  2014 at  17:47

Kwa Muhtasari

Timazi ya lugha gwanda, ata kuiweka kando,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

 

TIMAZI ya lugha gwanda, ata kuiweka kando,

Jinsi unavyo enenda, wazi hufwati mkondo,

Jina na tungo si chanda, na pete ufunge fundo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

 

Umepiga parapanda, bilashi kuanza kondo,

Silaha za kujilinda, zako ni fimbo na nyundo,

Hutapata ukomanda, kwa vidondo na vishindo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

 

Lafudhi hipigwi randa, Mwangi haneni ja Fondo,

Msiu si mnyarwanda, ndimi zao zina pindo,

Kiswahili cha Uganda, si kile cha Loliondo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

 

Wanenavyo Mijikenda, wa Ganze hata kinondo,

Wagiriama wa nyanda, uluyani Kavirondo,

Pamoja na Waholanda, wanatofauti rundo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

 

Lahaja kumi na kenda, zapitana kimuundo,

Washairi wa Mpanda, tofauti na Waendo,

Ada zao zimetanda, kwa ndimi na midundo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

 

Kiswahili ni matunda, ya bantu wenye pendo,

Waishi katika kanda, Afirika ya utando,

Mambasa hadi Ruanda, wamo siwaweke kando,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

 

Uko kwenye njia panda, hujakuwa mzalendo,

Lugha yenu hujalinda, kwa silaha za kishindo,

Umeazima magwanda, ya Waswahili mitindo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

 

Wangindo wameshatanda, kisauni kwa mgando,

Kujifunza wamedinda, lugha yao ya kingindo,

Mwaka rudi mwaka nenda, hawabadilishi mwendo,

Kamakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

WILSON NDUNG’U MUCHAI,

"Mjoli wa Shekinah",

Kitale

Tuma mchango wako kwa: swahilihub@ke.nationmedia.com 

 

 

TUKISIFIE KISWAHILI

Na EDWARD LOKIDOR

Imepakiwa - Saturday, December 6  2014 at  17:47

Kwa Muhtasari

Ngalawa ninaabiri, Kiswahili kusifia,

Sitokoma kome kome, kusifia Kiswahili.

 

NGALAWA ninaabiri, Kiswahili kusifia,

Kinazidi kushamiri, taifani chaenea,

Kwa yakini ninakiri, duniani yasambaa,

Sitokoma kome kome, kusifia Kiswahili.

 

Sitokoma kome kome,kusifia Kiswahili,

Tazidi kuwa mtume, kutetea Kiswahili,

Nitakifanye kivume, kieneze yetu mali,

Sitakionea soni, daima takitukuza.

 

Sitakionea soni, daima takitukuza,

Nitakisema chuoni, hata watu kinibeza,

Tahutubu hadharani,  Kiswahili kukikweza,

Nyimbo pia tazitunga,zinogeze Kiswahili.

 

Nyimbo pia tazitunga, zinogeze Kiswahili,

Maneno tayafinyanga, jumbe ipate fasili,

Sarufi sitovurunga, waloweka Waswahili,

Wasanii chipukizi,tukuzeni Kiswahili.

 

Wasanii chipukizi, tukuzeni Kiswahili,

Mtaweka kumbukizi, kitumia Kiswahili,

Tuige wetu wazazi, waloimba Kiswahili,

Wanamuziki wa sasa, tumieni Kiswahili.

 

EDWARD LOKIDOR,

''Balozi wa Kiswahili’’,

Nairobi

 

Tuma mchango wako kwa: swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

MASKINI WA NIDHAMU

Na SIMON ITEGI

Imepakiwa - Saturday, December 6  2014 at  17:48

Kwa Muhtasari

Vazi lako ukipima, viungovyo lisetiri,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

NATUMAI msalama, salimini bila shari,

Hu utungo nautuma,  ya moyo ninakiri,

Natumai mtasoma, muelewe shwarishwari,

Maskini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

Moyo wangu waterema, kuwaona mwakariri,

Kama samba mwalalama, kijigonga kwa vidari,

Na kidete mwasimama, haki zenu kudhihiri,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

Vazi lako ukipima, viungovyo lisetiri,

Usianze kulifuma, bila kimo kubashiri,

Sio jambo la hekima, maumboyo kuhakiri,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea

 

Mila zetu kuzitema, hilo sio jambo zuri,.

Kunga zetu za gharama, kupuuza sio heri,

Ni utumwa huo jama, ustarabu kughairi,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

Tudumishe na heshima, kwa wadogo wa kiumri,

Tujitunge kina mama, wasiige na vigori,

Hili swala linauma, nanitungu kishubiri,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

Yashangaza naungama, wenzanguni mafahari,

Kunivua ni dhuluma, vilevile uayari,

Nambie kitaaluma , nelekeze nishauri,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

Tamatini ninakoma, hilo swala mfikiri,

Moyo wangu wazizima, kwa utungu sio siri,

Hadharani ninasema, ulimwengu ni safari,

Masikini wa nidhamu,limwengu mekuzoea.

SIMON ITEGI NYAMBURA,

Chuo Kikuu cha Laikipia

Tuma mchango wako kwa: swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

TUSIFU KISWAHILI

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na EDWARD LOKIDOR - 'BALOZI WA KISWAHILI'

Imepakiwa - Wednesday, December 3  2014 at  18:06

Kwa Muhtasari

Ngalawa ninaabiri, Kiswahili kusifia,
Kinazidi kushamiri, taifani chaenea,

Sitokoma kome kome, kusifia Kiswahili.

 

NGALAWA ninaabiri, Kiswahili kusifia,
Kinazidi kushamiri, taifani chaenea,
Kwa yakini ninakiri, duniani yasambaa,
Sitokoma kome kome, kusifia Kiswahili.

Sitokoma kome kome, kusifia Kiswahili,
Tazidi kuwa mtume, kutetea Kiswahili,
Nitakifanye kivume, kieneze yetu mali,
Sitakionea soni, daima takitukuza.

Sitakionea soni, daima takitukuza,
Nitakisema chuoni, hata watu kinibeza,
Tahutubu hadharani, Kiswahili kukikweza,
Nyimbo pia tazitunga, zinogeze Kiswahili.

Nyimbo pia tazitunga, zinogeze Kiswahili,
Maneno tayafinyanga, jumbe ipate fasili,
Sarufi sitovurunga, waloweka Waswahili,
Wasanii chipukizi, tukuzeni Kiswahili.

Wasanii chipukizi, tukuzeni Kiswahili,
Mtaweka kumbukizi, kitumia Kiswahili,
Tuige wetu wazazi, waloimba Kiswahili,
Wanamuziki wa sasa, tumieni Kiswahili.


EDWARD LOKIDOR,
'BALOZI WA KISWAHILI'
NAIROBI.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

TUJIFUNZE KISWAHILI

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na SWALEH SUHEILl ABEID (SAUTI YA HAKI)

Imepakiwa - Wednesday, December 3  2014 at  18:10

Kwa Muhtasari

Neno moja liliyoko, la tafauti maani
Nami pia tabaini, niongeze yaliyoko

 

Shukurani zije kwako, ewe Nsura Hassan
Kwa kutoa hoja zako, ulotuma kilingeni
Neno moja liliyoko, la tafauti maani
Nami pia tabaini, niongeze yaliyoko

PAA ni ya kuruka angani, ya kupaa kama nyuni
PAA ni la masikani, lavimbwa sivuje ndani
PAA ni ya hayawani, kama mbuzi wa mwetuni
PAA nyengine baini, para samaki karoni

UNGA ni kushikanisha, pabovu pawe pazima
UNGA ni wa kujilisha, wa ngano au wa sima
UNGA ni ya kupatanisha, ukashikamana uma
UNGA nyengine nonesha, kama iko utasema.

PANGA ni ya lile panga, la kufyekea nyasini
PANGA ni ya ile panga , yenye ndonga mzimuni
PANGA ni kule kupanga, kuweka sawa swafuni
PANGA nyengine ni panga, kudanganya na kukhini

MBUZI ni ya hayawani, zizini twawashungia
MBUZI ni ya mapishini, ni ya nazi twakunia
MBUZI mwitu mjuweni, msituni atokea
MBUZI nyengine siyoni, kama iko nionyeni
UWA ni ya lile uwa, la kuchanuka mtini
UWA ni kwenda kuuwa, mja afe duniyani
UWA ni boma hutiwa, au ukuta nyumbani
UWA nyengine tambuwa, kama iko ibaini

KATA ni ya kuyachota, kwa kata maji uteke
KATA ni kukatakata, hadi m’ti uanguke
KATA ni ya kuukata, ukuruba ukatike
KATA nyengine kukata, kiuno kitibwirike

TAA ni ya kumulika, tukaoneya kizani
TAA ni ya makhuluka, samaki wa baharini
TAA taa kushikika, kuhangaika ndweleni
TAA nyengine nataka, kama iko ileteni

FUA ni ya kuzifuwa, kisha nguo ziswafika,
FUA ni chombo kufuwa, kama pete ipendeke
FUA ni nazi kufuwa, hadi kumbi limbambuke
FUA nyengine tambuwa, kama iko itajike

TANGA ni kutangatanga, kubeheneka mjini
TANGA ni roho kutanga, mtu hawi na makini
TANGA ni ya lile tanga, la jahazi baharini
TANGA nyengine kuchanga, pesa zifae chamani
TUNGA ni kule kutunga, kwa usaha wa jipuni
TUNGA ni ya kujitunga, ukae tahadharini
TUNGA ni kule kutunga, mbuzi walishe nyasini
TUNGA nyengine kutunga, kishada cha asimini

TUNGA ni ya kuvitunga, vina viwe na mezani
TUNGA ni ya kuutunga, unga mule tungiyoni
TUNGA ni ya kuvitunga, vitinyango kijitini
TUNGA nyengine kutunga, Insha kule shuleni

Swaleh Suheil Abeid
(Sauti Ya Haki)
Dubai – U.A.E.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

MANDERA KULIKONI?

Mamia Mandera wakimbilia pahala salama

Raia wasio wa asili ya Kisomali wakusanyika katika uwanja wa ndege wa Mandera Novemba 25, 2014 wakihofia kurudi makwao baada ya basi kushambuliwa na watu 28 kuuawa. Picha/MANASE OTSIALO 

Na JAMES MUTWIRI

Imepakiwa - Thursday, November 27  2014 at  14:18

Kwa Muhtasari

Mandera twomba tulizi, ndo usalama tetezi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

MANDERA tujue juzi, do! Yalotanda machozi,

Mandera wahedi mwezi, vifo mekita mizizi,

Mandera ya waziwazi, mikosi na mavamizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera ushambulizi, Jumamosi angamizi!

Mandera lojibarizi, kwa basi ndo uvamizi,

Mandera ndo ombolezi, kafa belele walezi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera i matembezi, waama siyo mapozi,

Mandera i bumbuazi, kafa wachapaji kazi,

Mandera nyi wasikizi, ni majonzi siku hizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera hatujiwezi, dunia hi vinywa wazi,

Mandera i unyakuzi, wa roho mi sinyamazi,

Mandera kuntu tatizi, mezuka janga tukizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera la uchukuzi, basi katekwa uwazi,

Mandera ndo ukatizi, wa aushi ndo telezi,

Mandera walo wajuzi, kauliwa kichokozi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera pate geuzi, iweze kuwa pendezi,

Mandera uzungumzi, uwe amani tambuzi,

Mandera hatwipuuzi, kuwekwe  uangalizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera nyi viongozi, mwiletee ukombozi,

Mandera yalo wokozi, tendwe pasi ubaguzi,

Mandera twomba tulizi, ndo usalama tetezi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

JAMES MUTWIRI WANJAGI,

“Malenga Msifika,”

 Chuka-Tharaka Nithi.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

TUMECHOKA KUFA

Mamia Mandera wakimbilia pahala salama

Raia wasio wa asili ya Kisomali wakusanyika katika uwanja wa ndege wa Mandera Novemba 25, 2014 wakihofia kurudi makwao baada ya basi kushambuliwa na watu 28 kuuawa. Picha/MANASE OTSIALO 

Na LUDOVICK MBOGHOLI

Imepakiwa - Friday, December 5  2014 at  16:13

Kwa Muhtasari

Kila siku visavisa, roho zinadekadeka

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

SASA tumechoka kufa, na miili kuizika

Twafa bila taarifa, ya maradhi kutushika

Kila kuchao maafa, ya ugaidi kuzuka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Kila siku visavisa, roho zinadekadeka

Hatutulii kabisa, twafa huku tukizika

Ndipo napiga kamsa, kufa sasa tumechoka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Kiongozi wa taifa, Uhuru Kenyatta kaka

Nakwambia huku kufa, kipumbavu tumechoka

Kama kufa ndio sifa, basi tumekinaika!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Tumechoka kufa sasa, UhuRuto wahibaka

Hata kwenye makanisa, mabomu yanalipuka

Na misikitini visa, vingi mno vinazuka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Kufa sisi tumechoka, twafa kama takataka

Twauliwa kama nyoka, kwa risasi na mashoka

Hakuna wa kuponyoka, twambe amenusurika!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Ovyo ovyo twauliwa, na doria wanashika

Wanajeshi wetu hawa, na polisi kadhalika

Waona tukiuawa, huku twafanywa mateka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Mimi naona ajabu, helikopta zazunguka

Mandera zikijaribu, ati amani kuweka

Na huku Al-Shababu, nao kasi wanashika!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Kuuawa kikatili, wananchi tumechoka

Huku tuna serikali, tuloipa mamlaka

Tena ni ya dijitali, vijana walochipuka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Narudia mauaji, ya Mandera tumechoka

Tunaona wachinjaji, wa vipanga na vishoka

Wakija kwenye vijiji, kuchinja na kutoroka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Na sio tuu Mandera, hata Pwani wamefika

Na maeneo ya bara, nako wameshazunguka

Magaidi na wakora, na wahuni kadhalika!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

 

 

TUSIFU KISWAHILI

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na EDWARD LOKIDOR - 'BALOZI WA KISWAHILI'

Imepakiwa - Wednesday, December 3  2014 at  18:06

Kwa Muhtasari

Ngalawa ninaabiri, Kiswahili kusifia,
Kinazidi kushamiri, taifani chaenea,

Sitokoma kome kome, kusifia Kiswahili.

 

NGALAWA ninaabiri, Kiswahili kusifia,
Kinazidi kushamiri, taifani chaenea,
Kwa yakini ninakiri, duniani yasambaa,
Sitokoma kome kome, kusifia Kiswahili.

Sitokoma kome kome, kusifia Kiswahili,
Tazidi kuwa mtume, kutetea Kiswahili,
Nitakifanye kivume, kieneze yetu mali,
Sitakionea soni, daima takitukuza.

Sitakionea soni, daima takitukuza,
Nitakisema chuoni, hata watu kinibeza,
Tahutubu hadharani, Kiswahili kukikweza,
Nyimbo pia tazitunga, zinogeze Kiswahili.

Nyimbo pia tazitunga, zinogeze Kiswahili,
Maneno tayafinyanga, jumbe ipate fasili,
Sarufi sitovurunga, waloweka Waswahili,
Wasanii chipukizi, tukuzeni Kiswahili.

Wasanii chipukizi, tukuzeni Kiswahili,
Mtaweka kumbukizi, kitumia Kiswahili,
Tuige wetu wazazi, waloimba Kiswahili,
Wanamuziki wa sasa, tumieni Kiswahili.


EDWARD LOKIDOR,
'BALOZI WA KISWAHILI'
NAIROBI.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

TUJIFUNZE KISWAHILI

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na SWALEH SUHEILl ABEID (SAUTI YA HAKI)

Imepakiwa - Wednesday, December 3  2014 at  18:10

Kwa Muhtasari

Neno moja liliyoko, la tafauti maani
Nami pia tabaini, niongeze yaliyoko

 

Shukurani zije kwako, ewe Nsura Hassan
Kwa kutoa hoja zako, ulotuma kilingeni
Neno moja liliyoko, la tafauti maani
Nami pia tabaini, niongeze yaliyoko

PAA ni ya kuruka angani, ya kupaa kama nyuni
PAA ni la masikani, lavimbwa sivuje ndani
PAA ni ya hayawani, kama mbuzi wa mwetuni
PAA nyengine baini, para samaki karoni

UNGA ni kushikanisha, pabovu pawe pazima
UNGA ni wa kujilisha, wa ngano au wa sima
UNGA ni ya kupatanisha, ukashikamana uma
UNGA nyengine nonesha, kama iko utasema.

PANGA ni ya lile panga, la kufyekea nyasini
PANGA ni ya ile panga , yenye ndonga mzimuni
PANGA ni kule kupanga, kuweka sawa swafuni
PANGA nyengine ni panga, kudanganya na kukhini

MBUZI ni ya hayawani, zizini twawashungia
MBUZI ni ya mapishini, ni ya nazi twakunia
MBUZI mwitu mjuweni, msituni atokea
MBUZI nyengine siyoni, kama iko nionyeni
UWA ni ya lile uwa, la kuchanuka mtini
UWA ni kwenda kuuwa, mja afe duniyani
UWA ni boma hutiwa, au ukuta nyumbani
UWA nyengine tambuwa, kama iko ibaini

KATA ni ya kuyachota, kwa kata maji uteke
KATA ni kukatakata, hadi m’ti uanguke
KATA ni ya kuukata, ukuruba ukatike
KATA nyengine kukata, kiuno kitibwirike

TAA ni ya kumulika, tukaoneya kizani
TAA ni ya makhuluka, samaki wa baharini
TAA taa kushikika, kuhangaika ndweleni
TAA nyengine nataka, kama iko ileteni

FUA ni ya kuzifuwa, kisha nguo ziswafika,
FUA ni chombo kufuwa, kama pete ipendeke
FUA ni nazi kufuwa, hadi kumbi limbambuke
FUA nyengine tambuwa, kama iko itajike

TANGA ni kutangatanga, kubeheneka mjini
TANGA ni roho kutanga, mtu hawi na makini
TANGA ni ya lile tanga, la jahazi baharini
TANGA nyengine kuchanga, pesa zifae chamani
TUNGA ni kule kutunga, kwa usaha wa jipuni
TUNGA ni ya kujitunga, ukae tahadharini
TUNGA ni kule kutunga, mbuzi walishe nyasini
TUNGA nyengine kutunga, kishada cha asimini

TUNGA ni ya kuvitunga, vina viwe na mezani
TUNGA ni ya kuutunga, unga mule tungiyoni
TUNGA ni ya kuvitunga, vitinyango kijitini
TUNGA nyengine kutunga, Insha kule shuleni

Swaleh Suheil Abeid
(Sauti Ya Haki)
Dubai – U.A.E.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

TUJILINDE TULINDANE

Mamia Mandera wakimbilia pahala salama

Raia wasio wa asili ya Kisomali wakusanyika katika uwanja wa ndege wa Mandera Novemba 25, 2014 wakihofia kurudi makwao baada ya basi kushambuliwa na watu 28 kuuawa. Picha/MANASE OTSIALO 

Na FRANKLIN MUKEMBU

Imepakiwa - Thursday, November 27  2014 at  14:25

Kwa Muhtasari

Tuepukeni lawama, Kimaiyo Lenku pia,

Raia watajituma, waseme yanotokea.

 

NAMWELEKEA karima, risala zangu kutoa,

Kishairi ninasema, mizani napangilia,

Tukio linaniuma, Mandera lilotokea,

Tujilinde tulindane, usalama kudumisha,

Naukashifu unyama, ulokumba abiria,

Wa kidini uhasama, hauna manufaa,

Wavuruga usalama, kuua waso hatia,

Tujilinde tulindanem usalama kudumisha,

Polisi  wanajituma, wanaishika doria,

Watupokeza huduma, hakika wajitolea,

Tuwapeni na heshima, popote wakitujia,

Tujilinde tulindane, usalama kudumisha,

Tuepukeni lawama, Kimaiyo Lenku pia,

Raia watajituma, waseme yanotokea,

Kauli mbiu kituma, haraka tasaidia,

Tujilinde tulindane, usalama kudumisha,

Eneo hatari koma, kinga ni bora sikia,

Majanga sije yachuma, tawa vema kuzuia,

Palilia usalama, amani itaenea,

Tujilinde tulindane, usalama kudumisha,

Beti saba ninakoma, zimenizidi hisia,

Nabaki kushika tama, kumbukumbu tabakia,

Moyoni linaniuma, kahari tatujalia,

Tujilinde tulindane, usalama kudumisha,

FRANKLIN MUKEMBU

Mawimbi Ya Nchi Kavu

Kajuki-Nithi

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

MANDERA KULIKONI?

Mamia Mandera wakimbilia pahala salama

Raia wasio wa asili ya Kisomali wakusanyika katika uwanja wa ndege wa Mandera Novemba 25, 2014 wakihofia kurudi makwao baada ya basi kushambuliwa na watu 28 kuuawa. Picha/MANASE OTSIALO 

Na JAMES MUTWIRI

Imepakiwa - Thursday, November 27  2014 at  14:18

Kwa Muhtasari

Mandera twomba tulizi, ndo usalama tetezi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

MANDERA tujue juzi, do! Yalotanda machozi,

Mandera wahedi mwezi, vifo mekita mizizi,

Mandera ya waziwazi, mikosi na mavamizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera ushambulizi, Jumamosi angamizi!

Mandera lojibarizi, kwa basi ndo uvamizi,

Mandera ndo ombolezi, kafa belele walezi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera i matembezi, waama siyo mapozi,

Mandera i bumbuazi, kafa wachapaji kazi,

Mandera nyi wasikizi, ni majonzi siku hizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera hatujiwezi, dunia hi vinywa wazi,

Mandera i unyakuzi, wa roho mi sinyamazi,

Mandera kuntu tatizi, mezuka janga tukizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera la uchukuzi, basi katekwa uwazi,

Mandera ndo ukatizi, wa aushi ndo telezi,

Mandera walo wajuzi, kauliwa kichokozi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera pate geuzi, iweze kuwa pendezi,

Mandera uzungumzi, uwe amani tambuzi,

Mandera hatwipuuzi, kuwekwe  uangalizi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

Mandera nyi viongozi, mwiletee ukombozi,

Mandera yalo wokozi, tendwe pasi ubaguzi,

Mandera twomba tulizi, ndo usalama tetezi,

Mandera twomba azizi, utusikie Mwenyezi!

 

JAMES MUTWIRI WANJAGI,

“Malenga Msifika,”

 Chuka-Tharaka Nithi.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

MAGAZETI KUFUNGIA NYAMA

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Imepakiwa - Thursday, November 27  2014 at  14:29

Kwa Muhtasari

Kwa kero ninainama, kuyikashifu dosari,
Siyafungieni nyama, magazeti hifadhini!

 

NAJA na mengi mashaka, edita nipe nafasi,
Msin'ole kibaraka, mwingi wa mingi mikosi,
Watunzi tulipofika, tutakosa wafuasi,
Siyafungieni nyama, magazeti hifadhini!

Malenga tunajituma, kuyatunga mashairi ,
Vipi watuvuta nyuma,hawayasomi kwa ari,
Kwa kero ninainama, kuyikashifu dosari,
Siyafungieni nyama, magazeti hifadhini!

Buchari nalenda juzi, nyama nikainunue,
Sikuyamini maozi, ukweli niwelezee ,
Ikawa nzuri mbawazi, hali na muitambue,
Siyafungieni nyama, magazeti hifadhini!

' Sokomoko' nikaona, mzigo likafungiwa,
Kisha nikanza gombana, mpaka doa nikatiwa,
Jamani enyi wangwana,yasome muwe muruwa,
Siyafungieni nyama, magazeti hifadhini!

Kiwa hukwenda skuli, hifadhia hvitukuu,
Waje soma wawe nguli, wasije vuntika guu,
Wajaposoma madili, wapate busara kuu ,
Siyafungieni nyama , magazeti hifadhini!

Kuna mangi yakufana, mbali hiyi mitungo,
Heti tungachanjiana, pasi kuyapa mgongo,
Yatafaidi vijana, na walo pinda migongo,
Siyafungieni nyama, magazeti hifadhini!

Nawaaga kwaherini, ndiyo yaliyonileta,
Washairi hongereni, kweli walezi wazo matata,
Edita nashukuruni, Taifa kumetameta,
Siyafungieni nyama, magazeti hifadhini!

GITAA HEMAN ANGWENYI
'Mla wa ndovi malenga'
Migombani-Nyancha.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

KIFO CHA OTIENO KAJWANG

Otieno Kajwang'

Bw Otieno Kajwang' alipokuwa akifuatilia miradi ya ujenzi wa barabara katika mji wa Kikuyu, Kaunti ya Kiambu Novemba 18, 2014 mwendo wa saa saba. Alifariki usiku. Picha/ANNE MACHARIA 

Na LUDOVICK MBOGHOLI

Imepakiwa - Wednesday, November 19  2014 at  15:23

Kwa Muhtasari

Daima alisimama, kutetea walegevu

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

KIFO cha mwanasiasa, bwana Kajwang Otieno

Ni pigo kuu kwa sasa  twalia twasaga meno

Hakika tutamkosa, katika yetu maono

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Mola amlaze pema, huyu wetu kiongozi

Alosimama daima, akawa mpingamizi

Wa dhuluma na hujuma, mfano wa ulanguzi

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Alikemea daima, siasa za kipumbavu

Hakutaka uhasama, wa chuki, hila na wivu

Daima alisimama, kutetea walegevu

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Hivi moyo waniuma, nikikumbuka maneno

Aloteta akisema, kwamba ‘bado mapambano’

Wimbo wake ulovuma, ‘mapambano mapambano!’

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Wakenya kinatuchoma, kifo chake pigo kuu

Kisiasa kawa chuma, hakutia makuruu

Wakinzao kawazima, kama moshi wa kifuu

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Nasema poleni sana, poleni mliofiwa

Hasa mkewe na wana, na marafiki wafiwa

Na Raila pole sana, kifo kimekuumbuwa

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Ndio hali ya dunia, muda ukimalizika

Lazima unajifia, kwani Mungu kakutaka

Huishi kuendelea, lazima utaondoka!

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Kaditamati Mbogholi, mwisho wa shairi hili

Mliofiwa kwa kweli, nafahamu hamlali

Hata na kula hamli, huzuni imesaili

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

LUDOVICK MBOGHOLI

Al-Ustadh-Luqman

Ngariba – Mlumbi

Taveta – Bura / Ndogo

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

VISKETI VYA KUBANA

Minisketi

Wanawake wakiwa wamevalia nguo fupi, ambazo hazipaswi kuvaliwa katika maeneo rasmi ikiwamo ofisini. Picha/MAKTABA 

Na LUDOVICK MBOGHOLI

Imepakiwa - Wednesday, November 19  2014 at  14:50

Kwa Muhtasari

Wavaaje rinda duni, tena rinda la kubana

Lioneshalo mwilini, viungo vya siri pana

Kama huo si uhuni, tuuitaje kwa jina?

 

KAMA mwavaa vaeni, nguo ndefu tena pana

Sio kuvaa vimini, visketi vya kubana

Tuwaone hadharani, jinsi mlivyo jazana!

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

 

Hiyo ni tabia gani, mwawafundisha vijana

Ujinga wa uzunguni, mwatuletea bayana

Halafu mwataka nini, walifanye wavulana?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

 

Unapovaa vimini, na kamisi za kichina

Na sidiria chuchuni, na chupi ya ndani huna

Unatarajia nini, ukipita kwa kijana?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

 

Kuvuliwa hadharani, tena mchana mchana

Kiguo cha kishetani, kwangu ubaya hakuna

Maana uhayawani, nadhani umekubana!

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

 

Wavaaje rinda duni, tena rinda la kubana

Lioneshalo mwilini, viungo vya siri pana

Kama huo si uhuni, tuuitaje kwa jina?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

 

Mwaenda barabarani, ati mnaandamana

Mwampinga Maanani, kwa kuvalia vimina?

Nambieni hiyo nini, kama hiyo si laana?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

 

Havifiki magotini, visketi vya kubana

Vyaishia mapajani, karibu na hiyo ‘zana’!

Nyinyi ni viumbe gani, wala adabu hamna?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

 

Nguo hizo nguo gani, fupi kisha za kubana

Wala huokoti chini, kilichoanguka tena

Huinami mapajani, zimebana raha huna!

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

 

Na hicho chako kimini, dada yangu msichana

Kwani kina hadhi gani, kama siyo ya laana

Wamtamanisha nani, kama sio wavulana?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

 

Nusu uchi hadharani, watembea twakuona

Wala haya hauoni, na mnyama wafanana

Unamvutia nani, kama si hao vijana?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

 

 

 

KINA DADA WAKO HURU

Minisketi

Wanawake wakiwa wamevalia nguo fupi, ambazo hazipaswi kuvaliwa katika maeneo rasmi ikiwamo ofisini. Picha/MAKTABA 

Na EKADELI LOKIDOR

Imepakiwa - Monday, November 17  2014 at  15:07

Kwa Muhtasari

Jamani si ustarabu, ghashi kumdhalilisha,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

 

MWANGWANA yu huria, apendavyo kuvalia,

Si haki kumzomea, mja alivyovalia,

Matusi kumrushia, ghashi asiye hatia,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

 

Jamani si ustarabu, ghashi kumdhalilisha,

Ni jambo isojibu, banati kumdunisha,

Sio tena adabu, rindao kuteremsha,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

 

Wanawake wana hadhi, yafaa kuwastahi,

Mavazi yao kiudhi, kwa upole wanasahi,

Ni bora kuwanyaadhi, wavalie kisitahi,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

 

Wakati imefikeni, wanaume tustarabike,

Sheria tufuateni, daima tuwajibike,

Tuwache uhayawani, wanawake watukuke,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

 

Wakenya tukumbukeni, heshima kitu adhimu,

Maadili tushikeni, ustarabu pate timu,

Tubaidi walakini, kotekote kistakimu,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

 

EDWARD EKADELI LOKIDOR,

'Balozi wa Kiswahili'

NAIROBI.

 Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

DUNIANI KUNA WAJA

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na SYLVESTER SIDDI KIROBOTO

Imepakiwa - Wednesday, November 12  2014 at  19:40

Kwa Muhtasari

Mengi nimeangalia, moyoni nikaumia,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

 

KULIA huku kulia, kuna sababu kulia,
Leo nitawaambia, huzuni yanonitia,
Mengi nimeangalia, moyoni nikaumia,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Hapa katika dunia, mambo nimeshuhudia,
Kuna ya kufikiria, mtu ukamlilia,
Kunao wanoumia, na vibaya kusikia,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Nanzia hubani mle, ndimo mwenye dhiki tele,
Nimeionja Mpole, japo si sasa ni kale,
Leo kuna wateule, mapenzini wachochole,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Wangine wamefiliwa, na wenzi wao ghafula,
Uchungu waloachiwa, anaoujuwa Mola,
Hufika wakazidiwa, kaburini wakalala,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Wapo wasiojaliwa, watoto wao kupata,
Mifano wakapigiwa, hasa wakiwa wakata,
Kaburini wakitiwa, hakuna wa kuwaita,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Pia kunao fukara, wajaribucho hakiwi,
Huwakimbia ajira, wakiomba hawapewi,
Fungu lao kuzurura, kesho yao hawajuwi,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Wapo mwisho walofika, wakalaumu Rabuka,
Kosani wakamuweka, kwa kudhani ahusika,
Imani hutiwa shaka, na dini wakaitoka,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Tena kuna wenye pesa, walo tajiri kabisa,
Nao dunia yatesa, furaha wakaikosa,
Ila nui hii sasa, afadhali japo tasa,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Moliwa leo nalia, nyuso huzuni zatia,
Naumia kwangalia, mayatima wakilia,
Wajane wajinamia, bwana wakikumbukia,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Sijui mimi sijui, yote hayo sielewi,
Mie siumbi siui, na lolote siamuwi,
Bila uchungu sizui, mkosa hisia siwi,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Rahima nakusaili, imani zetu kumbuka,
Hali zetu zibadili, kukushukuru twataka,
Si kuwa hautujali, lakini twatamauka,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Ilivyo huko mbinguni, timiza na duniani,
Kwa hekima na imani, tuongoze alamini,
Tuepushe ya sharini, tusiingie dhikini,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Kama enzi ya safina, utunusuru Rabana,
Utuponye al’amina, aali wa swahibina,
Uyaone hayo inna, amina Rabb’l amina, ,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Sylvester Siddi Kiroboto
“Kimpole”
Duka la Mihalake (kwa Dhima ya Karima),
Eldoret Mjini

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

MAZINGIRA TUYATUNZE

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na WAMBUGU YUSUF

Imepakiwa - Wednesday, November 12  2014 at  19:40

Kwa Muhtasari

Tafakuri naileta, iwe chanzo cha karamu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

 

UFANISI na ukata, asilize mwafahamu,
Kukosa pia kupata, kipimo chake ni hamu,
Tafakuri naileta, iwe chanzo cha karamu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Ni ilani kwa wakata, nanyi mnaojikimu,
Mtakuja kula mwata, mazingira kihujumu,
Tunajitia utata, tunaishi kwenye sumu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Tukumbuke kuikata, miti ni kujihukumu,
Maafa tunayaleta, kwa vizazi takadamu,
Masika kutoyapata, mazao yawe adimu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Chemichemi kuzipata, ndu’angu lipo jukumu,
Shiriki pasi kusita, isije kutugharimu,
Kwa ghaidhi ninateta, nipulikeni adamu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Usafi kote kunata, ndiyo silika timamu,
Umbijani tukipita, wahakiki tabasamu,
Wanyama macho wavuta, wanatutia hamumu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Laazizi nawasuta, mambo haya ni muhimu,
Masaibu yatang’ata, tukikosa utalamu,
Tuondokee kujuta, tusende bure kuzimu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Sikio toeni nta, msije kujidhulumu,
Piganeni hivi vita, vya mazingira adhimu,
Tuwe mtungi na kata, maisha yawe matamu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

WAMBUGU YUSUF,
Malenga wa mlimani.
Thika.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

MIHADARATI ACHENI

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na "ZIMWI LIKUJUALO" - ABUBAKAR FAKHI

Imepakiwa - Wednesday, November 12  2014 at  19:36

Kwa Muhtasari

Haya ninayoyanena, si mambo ya kutania

Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni

 

BISMILLAHI ya Jabbari, Mola uliye Azizi,
Nakuomba yenye kheri, na baraka kwenye kazi,
Isinifike ya shari, na yote ya pingamizi,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Haya ninayoyanena, si mambo ya kutania,
Ni kitu nilichoona, katika hini dunia,
Wala sitopingana, na kaumu wenye nia,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Mihadarati hakika, humdhuru mtumizi,
Na katika pata shika, kama wenye usingizi,
Humfanya kuteseka, na mwishowe huwa mwizi,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Ulevi na misokoto, ugoro na ya uvundo,
Huwapoteza watoto, kwa afiya na matendo,
Na kuacha kama ndoto, uchomao uzalendo,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Jambo la kuhuzunisha, ni kuona mtegemewa,
Akiwa anawakisha, na kupuliza kwa hewa,
Ugoro na hiyo shisha, kwake zikiwa ni sawa,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Hasa kiwa msichana, alo na hino tabia,
Huwa ni hasara sana, kwa walimwengu jamia,
Hata pia mvulana, wote jangani hungia,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Kuhusika ulevini, ni hatari ya maisha,
Mitaani na shuleni, takuwa waogopesha,
Hata walio moyoni, kwako utahangaisha,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Ugomvi hujitokeza, pindi akizitumia,
Kuwapiganisha wenza, kwake hilo ni sawia,
Hakika inachukiza, hilo kwangu ni hatia,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Sijakuwa wa kukoma, ila wino unaisha,
Kueleza ya kuchoma, moyoni hayajaisha,
Huku muda wayoyoma, na pumzi nikishusha,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Beti kumi zimefika, nafupisha yangu mada,
Ni mambo yaso na shaka, yalosababisha shida,
Nawaombea Rabbuka, kuwapa yenye saada,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

"ZIMWI LIKUJUALO"
ABUBAKAR FAKHI

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

TUJIFUNZE KISWAHILI

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na NSURA HASSAN GAKURYA

Imepakiwa - Wednesday, November 12  2014 at  19:46

Kwa Muhtasari

Paa sehemu ya nyumba, jengo linapo simama,
Paa mfume kigumba, nawe ukapate nyama,

 

KATA viwe viwili, vipande vitu kugawa,
Kata upate sahali, mzigo katika kitwa,
Kata kiucho kikali, upate maji ya kunwa,
Kuna kata ilo mbali, ambayo sijaisema.

Paa sehemu ya nyumba, jengo linapo simama,
Paa mfume kigumba, nawe ukapate nyama,
Paa ni kusema kwamba, paa ni vile kinyama,
Paa zote nimeamba, ni gani sijaisema?

Teka maji kisimani, uende kuoshea nyanya,
Teka mateka vitani, bila huruma kufanya,
Teka ulo furahani, nikuone wako mwanya,
Teka ni hizo jamani, hizo ndizo nazojua.

Kaa hapano mwenzangu,uneleze ya masiku,
Kaa hupika majungu,ni moto huku na huku,
Kaa mnyama mchungu,huenda maliza kuku,
Kaa nyingine wahibu,niambiya niijuwe.

Taa samaki mtamu, aishiye baharini,
Taa ni chombo muhimu, washa usiwe gizani,
Taa dunia ni ngumu, hangaika mitaani,
Taa mimi sifahamu, nyengineyo sifahamu

Panda mbegu ardhini, ili upate chakula,
Panda ya mti jamani, ulotanda kwa uwala,
Panda haraka mtini, simba asije kuwala,
Panda silaha shambani, iloachana kuwili.

Tama ni kama kusema, napiga tama la maji,
Tama usishike tama, kishika raha haiji,
Tama namaliza jama, na wala usinihoji,
Tama nayo kaditama, kiniita mimi siji.

NSURA HASSAN GAKURYA
Mombasa, Tiwi

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

MOLA WALAZE PEMA

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na EKADELI LOKIDOR

Imepakiwa - Monday, November 10  2014 at  14:22

Kwa Muhtasari

Machungu yatulemea, shufaa metutoweka,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

 

POLISI mlofariki, wakenya twawaombea,

Heshima mnastahiki, muwanga kujitolea,

Kazini likuwa nyuki, katu hamkuzembea,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

 

Simanzi imetuvaa, mauti yalipofika,

Furaha metukimbia, mebaki kusononeka,

Machungu yatulemea, shufaa metutoweka,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

 

Polisi mloumia, afueni twawakia,

Mola awape shufaa, matatibu kipokea,

Katu sikate tamaa, kazini mkirejea,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

 

Wakati sasa mefika, polisi kuwafidia,

Tuwapeni madaraka, polisi walobobea,

Polisi tatamauka, tusipowapa ridhaa,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

 

Polisi tuwape silaha, majangili siwapiku,

Mafunzo yawe silaha, watumie kila siku,

Ya Kapedo si mzaha, Lokidor sina chuku,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

  

EDWARD EKADELI LOKIDOR,

'Balozi wa Kiswahili'

NAIROBI.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

HONGERA GOR MAHIA

Mashabiki wa Gor Mahia

Mashabiki wa Gor Mahia wakishabikia timu hiyo awali. Picha/MAKTABA 

Na EKADELI LOKIDOR

Imepakiwa - Monday, November 10  2014 at  13:58

Kwa Muhtasari

Kwa hakika mekazana, hamnani wa kukana,

Hongera Gor mahia, ligi kuu kunyakua.

 

KWA mara nyingine tena, Gor mahia mefana,

Nyingi timu mmechana, kileleni kubanana,

Kwa hakika mekazana, hamnani wa kukana,

Hongera Gor mahia, ligi kuu kunyakua.

 

Kidete mmesimama, yenu taji kutetea,

Ulingoni kajituma, Ushuru kawapandua,

Tatu goli mkafuma, ushindi kajipatia,

Hongera Gor mahia, ligi kuu kunyakua

 

Heko Sserunkuma, mengi mabao mefunga,

Eric kiki kavuma, mosi bao kaifunga,

Ushuru kashika tama, lipojitoa muwanga,

Hongera Gor mahia, ligi kuu kunyakua.

 

Mashabiki shukurani, wastarabu mekuwani,

Litulia ulingoni,  rabsha kaepukani,

Amani ikasheheni, uga kawa salimini.

Hongera Gor mahia, ligi kuu kunyakua.

 

Gor ninawapa shime, endeleni kubobea,

Kome kome sikome, yenu kombe kutetea,

Ugani muwe umeme, upeoni kubakia.

Hongera Gora mahia, ligi kuu kunyakua.

 

EDWARD EKADELI LOKIDOR,

'balozi wa Kiswahili'

Nairobi.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

Bodaboda zatuponda

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na FRANKLIN MUKEMBU

Imepakiwa - Wednesday, November 5  2014 at  16:56

Kwa Muhtasari

Kila mara yatendeka, wananchi waumia,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari

 

Nimejawa na kumaka,kadhia nasimulia,
Shairi naliandika, kujuza yalotokea,
Kila mara yatendeka, wananchi waumia,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Mapema tukidamuka, kazini kuelekea,
Bodaboda zatumika, upesi zatudumia,
Madhari zina haraka, ndiani kutokawia,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Haraka hina baraka, ajali zinatokea,
Abiria wadhurika, vibaya wanaumia,
Hela nyingi zatumika, kutibu waloumia,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Wendeshaji twawataka, mafunzo kuhudhuria,
Vyeti ghushi mukisaka, ujuzi tawondokea,
Ufisadi tukiepuka, tajiriba tawafaa,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Barabara vema shika, ishara nazo tumia,
Matutani mukifika, mwendo wako pungua,
Hatimaye utafika, ajali hitotokea,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Vituoni mukifika, abiria kadiria,
Lukuki ukiitaka, matatani tajitia,
Trafiki watakusaka, majanga tajichumia,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Kaditama nimefika, dereva mewahusia,
Nidhamu yahitajika, barasite kitumia,
Maafa yatosikika, raia tahudumia,
Boda boda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


FRANKLIN MUKEMBU
Mawimbi Ya Nchi Kavu
Kajuki-Nithi

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

Injili yenye vitimbi

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na Ben Gichaba

Imepakiwa - Wednesday, November 5  2014 at  16:56

Kwa Muhtasari

Vinatendwa bila haya, leyo wamepatikana
Injili hii ni ipi?,mchungaji awa fisi

 

WAUMINI tunaliya, kwa yale tuloyaona,
Jicho pevu angaliya, vitimbi tukaviona,
Vinatendwa bila haya, leyo wamepatikana,
Injili hii ni ipi, mchungaji awa fisi


Kondoo wake mewala, kitoweo kuwafanya,
Pesa zao yuazila, akidai kuwaponya,
Tumia jinake Mola, wafuasi kunyanganya,
Injili hii ni ipi, mchungaji awa fisi


Miujiza hii feki, kuhadaa waumini
Mola unamdhihaki, kutapeli waumini
'Kanyari' u mnafiki, kakuingia shetani
Injili hii ni ipi, mchungaji awa fisi


Jamani potasiamu, wawapaka waumini,
Eti ndo watoe damu, ndiposa wakuamini,
Wahadaa wanadamu, pesa zao wathamini,
Injili hii ni ipi, mchungaji awa fisi


u mkora kama popo, 'Kanyari' mepatikana,
wale pia waliyopo, jueni kimeumana,
Mjinga erevukapo, matata tapatikana,
Injili hii ni ipi, mchungaji awa fisi


Ndugu zangu waumini, mechezewa shere sisi,
Tuendapo kanisani, tusijeliwa na fisi,
Jamani tuwe makini, tumkane ibilisi,
Injili hii ni ipi, mchungaji awa fisi


Meandikwa bibilia, waziwazi twaisoma,
Ishara zitatujia, maandikoni twasoma,
Manabii tatujia, kidai kutenda wema,
Injiji hii ni ipi?, mchungaji awa fisi


Kaditama ninafika, mhariri kazi kwako,
Yangu nimeyaandika, iliyobaki ni yako,
Wewe bingwa mtajika, uhariri kazi yako,
Injili hii ni ipi, mchungaji awa fisi

BEN GICHABA

Chuo kikuu cha Kenyatta

Nairobi

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

Mkosa si mwana

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na SOUDY PODOS (TALL G

Imepakiwa - Wednesday, November 5  2014 at  16:51

Kwa Muhtasari

Mkono utaniunga, na kuitia saini
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

 

NIMWEJITOA mhanga, kuwambia wenye kani,
Fika hata kwa mganga, na ramli kubaini,
Mkono utaniunga, na kuitia saini,
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi,

Ni mengi anayotenda, na wengi wanamsema,
Ayatenda yenye inda, yasio leta salama,
Ni wengi wanamuinda, ayatendayo si mema,
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

ziwe nyingi tendekeza, akitakacho chukua
Hutaki kumchukiza, na mwana silie ngowa
Atakuja kukukweza, ujute na kuzaliwa
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

Humkanyi akosapo, eti ni mwana mdogo
Kumi na tano alipo, asema nawe kwa kogo
Hajaupata mchapo, wala utamu wa hogo
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

Akitumwa hatumiki, alisemalo ni basi
Nenda kanunue hiki, dukani kwa Almasi
Atakujibu sitaki, isiyo na wasiwasi
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

Alitakalo hufanya, lafaradhi au suna
Ukimuonya la njia, takupa jibu la kina
Tamaka kwa kusikia, jibu alilolinena
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

Jina lake Athumani, na mkofu ushingoni
Rangi zimo vidoleni, na kidani kifuani
Nywele kachoma kichwani, na nshi ameauni
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

Jina lake Mariamu, tamati ni kituoni
Si halali si haramu, atendayo si yakini
Baa nyumba ya kudumu, anayo kesha mjini
Usimlaumu mwana ,makosa niye mzazi

SOUDY PODOS (TALL GUY)
DUKUDUKU LA ROHONI
BIN SUDI FARM
GANDA MALINDI

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

Mnafiki ni mfitini

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na NYAMWARO wa NYAGEMI

Imepakiwa - Wednesday, November 5  2014 at  16:55

Kwa Muhtasari

Wangi wao ni ja nyuki, na ukiwo mizingani

Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!

 

SIINGIYI kwa mikiki, nisikize kwa makini,
Kujua mwastahiki, nililetalo mezani,
Iwapo humakiniki, tego litakutegeni,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Tafakari uhafiki, wadhamuwo maishani,
Si kwamba huwakumbuki, kutokea uchangani,
Wako tele marafiki, walokutiya tabani,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Wangi wao ni ja nyuki, na ukiwo mizingani,
Semo halisahuliki, li tamu toka kinwani,
Na uchungu husemeki, kututiya hatiani,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Mabaya wanashabiki, japo sio hadharani,
Kisiri wanashiriki, kukuongoza gizani,
Kutangaza taharuki, wao ndio namba wani,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Husababisha hilaki, kwa wangi waso makini,
Chambua utasadiki, akhi ni majoka kijani,
Nyasini hatambuliki, mwendo wa chini kwa chini,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Mangi hayafikiriki, usidhani ni matani,
Mawi wanayashiriki, kikulacho ki nguoni,
Songombwingo wazandiki, fanya kuwatambueni,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na na mfitini!


Mbona hawaeleweki, nyendo za kihunihuni,
Wafuge hawafugiki, hayawani wa nyikani,
Pika sumu hawachoki, za kondoo kavaeni,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Nawaaga halaiki, lumbo natamatishani,
Wajuweni wazandiki, wanafiki wafitini,
Si eti nawashitaki, bali tupate makini,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


NYAMWARO wa NYAGEMI
'Malenga wamigombani'
Verce Ndumberi High-Kiambu.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

Msaada upelekwe Turkana

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na  R. KIZUKA

Imepakiwa - Wednesday, November 5  2014 at  16:52

Kwa Muhtasari

Wahisani nalia tena,kisikieni kilio

hali mbaya Turkana,ni maafa Nakurio

 

WAHISANI nalia tena,kisikieni kilio
Na hayakuanza jana,yataka mazingatio
Japo mie ni kijana,kubali wangu ujio
Hali mbaya Turkana,ni maafa Nakurio

Chakula kukosekana,yatangazia redio
Walia baba na nina,kufiliwa na wanao
Wengi makao hawana,waondoka wazazio
Hali mbaya Turkana,ni maafa Nakurio

Ukame mezidi sana,na hasa huko Kerio
Maafa yako bayana,hakuna alo salio
Machozi ya Turkana,nani hasiki vilio
Hali mbaya Turkana,ni maafa Nakurio

Viongozi hili sana,wajinga ndo waliwao?
Vifo vya waturkana,nani hasiki vilio
Hali mbaya Turkana,ni maafa Nakurio

BW. R. KIZUKA
SHULE YA MSINGI YA TOM MBOYA
MOMBASA.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

Mashabiki tulieni

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na Edward Ekadeli Lokidor,

Imepakiwa - Wednesday, November 5  2014 at  16:49

Kwa Muhtasari

Mashabiki nawaomba, wasitarabu tuweni

Mashabiki tulieni, zetu timu zikicheza

 

MASHABIKI nawaomba, wasitarabu tuweni,
Kwa udi na uvumba, tuepuke purukushani,
Timu takosa kubamba, rabsha kizuani,
Mashabiki tulieni, zetu timu zikicheza.

Fujo hino ni hatari, yaletani yalo soni,
Timu yetu taadhiri, kilipa kubwa faini
Wachezaji takosa ari, kikatazwa ulingoni,
Mashabiki tulieni, zetu timu zikicheza.

Tuloona machakosi, kwa hakika yaudhi,
Vurugu lipohalisi, uga kapoteza hadhi,
Time mepata nuksi, hawapati tena radhi,
Mashabiki tulieni, zetu timu zikicheza.

Vurumai si kambumbu, mashabiki sikizeni,
Kimpiga wako umbu, wajitia walakini,
Tusiwe bumbubumbu, waso katu na makini,
Mashabiki tulieni, zetu timu zikicheza.

Twapenda Gor mahia, timu bora taifani,
Kwenye soka mebobea, daima mu kileleni,
Mashabiki sikia, siitie walakini,
Mashabiki tulieni, zetu timu zikicheza

Sirikali yetu timu, sitokoma kusifu,
Mawe hino ni mabomu, yaribu yake wasifu,
Gor takosa muhimu, vurugu kiwa sufufu,
Mashabiki tulieni, zetu timu zikicheza.

Edward Ekadeli Lokidor,
'Balozi wa Kiswahili'
Nairobi

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com