Nabhany alale pema

Na Abdalla Shamte

Imepakiwa - Sunday, March 5  2017 at  15:05

Kwa Mukhtasari

Mauko naomboleza, kiriro napiga kele,
Naomba kubembeleza, zangu dua ziwe kilele,

 

Maombi nayalekeza, kibulani yaleke,
Ba Nabhany yufile, Yarabi na mtuze jaza.

Machozi nabubujika, kilizo naliya kile.
Kimya kisonyamazika, cha nyende na kelele,
Moyoni naungulika, simanzi zinitatile,
U wapi muangaza ule, muwako ushazimika.

Nawaza nikimkubuka, ndu yangu sahibu yule,
Yuki kituwa kitweka, Kiswahili kiteule,
Yuliwafuzu wazuka, tambuzi wakatambule,
Sheikh Nabhany afile, Mufti Swahili mtajika.

Nabhany Musilimu, mavani katangulile,
Afufuliza kuzimu, palo wema nafikile,
Akamuone Hashimu, Muhamadi Mtumile,
Aishi naye milele, daima dumu dawamu.

Wa Matondoni na Lamu, makiwani nawapa pole,
Wadogo na wa makamu, vikongwe na vikongole,
Ni faradhi wanadamu, kifo nacho kimusole,
Nabhany pema alale, namuombea Rahimu.


Abdalla Shamte,
“Mtumwa wa Mungu”
Mwembekuku, Mombasa.