Nguli katutoka

Na Gwandiko Erneo

Imepakiwa - Sunday, March 5  2017 at  15:11

Kwa Mukhtasari

Waswahili twahuzuni, kuondokewa Mwalimu,
Tungo zake kifuani, tutazilinda zidumu,

Nabhany si kifani, kwa tungo zake muhimu,
Nguli wetu katutoka, tunalia walimwengu.

Tunalia walimwengu, nguli wetu kututoka,
Akuhifadhi ye Mungu, huna kosa ulotoka,
Twaumia kwa machungu, mhadhiri kututoka,
Nguli wetu katutoka, tunalia walimwengu.

Kiswahili ulienzi, walimwengu twalijua,
Waswahili wanagenzi, kwako fani kujulia,
Ulizisana na tenzi, bahari kutung’ania,
Nguli wetu katutoka, tunalia walimwengu.

Kiswahili kimekua, duniani kukijua,
Hapa kwetu Tanzania, Nabhany twatambua,
Kumbi za kishairia, kwako twakurejelea,
Nguli wetu katutoka, tunalia walimwengu.

Salamu wote wafiwa, zamu kwanza Wanakenya,
Aliwapeni fatawa, Tungoni aliwakanya,
Kwa lugha Kiswahiliwa, fumbateni nawatonya,
Nguli wetu katutoka, tunalia walimwengu.

Gwandiko Erneo,
Tanzania.