MOLA WAENDE SALAMA WAENDAO MAKA

Sherehe za Eid al-Adha

Waumini wa Dini ya Kiislamu katika uwanja wa Kaunti ya Mombasa wakati wa swala ya Eid al-Adha maarufu kama Idi ya Kuchinja Septemba 24, 2015. Picha/KEVIN ODIT 

Na MWANDISHI WETU

Imepakiwa - Friday, September 9  2016 at  12:50

Kwa Mukhtasari

Rabi Mola Rahamani, mwenye kuombwa Manani,

Mola waende salama, wandao kuhiji Maka.

 

RABI Mola Rahamani, mwenye kuombwa Manani,
Wale wenye na imani, nguzo hii kutamani,
Wazidishe matumaini, moyo uwe na Imani,
Mola waende salama, wandao kuhiji Maka.

Waondolee mashaka, tabu za yao safari,
Wende wakahiji maka, kwa salama na buheri,
Hija ikimalizika, wasipatwe na hatari.
Mola waende salama, wendao kuhiji Maka,

Wakamalizie hamu, mambo yaende vizuri,
Warudi kwa tabasamu, shughuli ziwe shuari,
Wamemalioza saumu, Mola wote wasitiri,
Mola waende salama, wendao kuhiji Maka.

Na sisi ambao kwamba, Hija hii hatupati,
Tunakuomba na kwamba, unaokuja wakati,
Nasi tuende kuomba, Kwa muda na kwa wakati,
Mola waende salama, wendao kuhiji Maka.

Wendao wende salama, waume na kina mama,
Ibada hii ni njema, tena mno nguzo njema,
Mungu akikukirima, ifanye kuwa lazima,
Mola waende salama, wendao kuhiji Maka.

Ibada yake Mwenyenzi, moja ya nguzo azizi,
Na ambaye hujiwezi, kuitimiza huwezi,
Inshala Mola muwezi, Takuwezesha muwezi,
Mola waende salama, wendao kuhiji Maka.

Hija kubwa yetu nguzo, baada ya Ramadhani,
Ikiwa pesa unazo, nazo kuacha nyumbani,
Na pia nguvu unazo, si mgonjwa asilani,
Mola waende salama, wendao kuhiji Maka.