Mtu ananitukana

Na Stephen Dik

Imepakiwa - Sunday, November 6  2016 at  12:47

Kwa Mukhtasari

NAAPA mbele ya umma, kuwa mwalimu wa hadhi,
Nina vyeti chungu zima, na vyeo vya usitadhi,

 

Naapa mbele ya umma, kuwa mwalimu wa hadhi,
Nina vyeti chungu zima, na vyeo vya usitadhi,
Nafundisha mambo mema, ndani ya mbingu na ardhi,
Nimepata sifa nyingi, kutoka Pwani na Bara.

Na kuitwa hili jina, eti 'Mwalimu’ Tefano,
Nashindwa kisa na mana, nimebatizwa kwa nini,
Nilibatizwa mchana, hapa ndani ukumbini,
Nikawa nashitumiwa, maneno yaliwakera.

Niliposema ya kwamba, nguvu ni kujiamini,
Namwondolea ushamba, mtu niliyemdhani,
Ndipo ajihisi bomba, mwanaume namba wani,
Na asiwe na mawazo, ya kuenda kwa mganga.

Na wala sikumtukana, kutia moyo machungu,
Nia mbaya hapana, mimi ni mtu wa Mungu,
Ninazidi kukazana, kufunza ulimwengu,
Nguvu zako za kiume, ni wewe hujiamini.

Na mwisho ninaamuru, kuwaaga kishairi,
Na wote kuwashukuru, wasomao mashairi,
Ni fani yenye uhuru, kuongea bila siri,
Na kama nimekosea, hapa nimesema pole.

Mwalimu Stephen Dik
“Mpenda Ushairi”
Ugunja