http://www.swahilihub.com/image/view/-/2652180/medRes/965687/-/10kh988/-/BDLNairobi0207EF.jpg

 

NAIROBI

Jiji la Nairobi

Sehemu ya jiji la Nairobi kwenye picha iliyopigwa Julai 2, 2014. Picha/SALATON NJAU 

Na OMAI ABDALLA NG’ANZI wa Eastleigh Section II, Nairobi

Imepakiwa - Tuesday, June 5  2018 at  09:23

Kwa Muhtasari

Mji wetu unanuka, sijui niseme nini,

Nairobi inanuka, ni chafu sana mjini.

 

MJI wetu unanuka, sijui niseme nini,
Raia tunashituka, hatujui mambo gani,
Mji umejaa taka, popote barabarani,
Nairobi inanuka, ni chafu sana mjini.

Wale tulioandika, usafi hapa mjini,
Wa kuzoa takataka, pawe pasafi mjini,
Wote wameshatoweka, hatuwaoni kazini,
Nairobi inanuka, ni chafu sana mjini.

Mwisho wa mwezi kifika, wamejaa ofisini,
Mshahara wanataka, na kazi hatuioni,
Na kama wasiposhika, wanakwenda mgomoni,
Nairobi inanuka, ni chafu sana mjini.

Zimejaa takataka, harufu mbaya mjini,
Maradhi yanatufika, kipundupindu milini,
Hayo ni yetu mashaka, atatuokoa nani,
Nairobi inanuka, ni chafu sana mjini.

Wale mnaohusika, viongozi kauntini,
Oneni haya mashaka, mtayamaliza lini,
Mji wetu unanuka, katikati ya tauni,
Nairobi inanuka, ni chafu sana mjini.

OMAI ABDALLA NG’ANZI wa Eastleigh Section II, Nairobi