http://www.swahilihub.com/image/view/-/4776950/medRes/2117165/-/r0d0h2/-/kazi.jpg

Shairi: Ajira

mtu akitafuta taarifa za ajira kwenye mtandao kupitia kompyuta 

Na Ismail Amiri Nyangasa

Imepakiwa - Tuesday, September 25  2018 at  13:08

Salamu kwangu muhimu, hili ni jambo adhwimu,

Niishikapo kalamu, kuna jambo la muhimu,

Leo hii najihimu, kueleza yalazimu,

Hili janga melichuma, nitalila na wakwetu.

Miaka inasogea, mambo nilotarajia,

Meshindwa kuyafikia, ujuzi wanikimbia,

Ajira metokomea, sijachoka subiria,

Hili janga melichuma, nitalila na wakwetu.

Hakika ninasubiri, zilisemwa zitatoka,

Ni mwaka sasa wa pili, kwa awamu zinatoka,

Siandiki kuhubiri, radhinu ninaitaka,

Hili janga melichuma, nitalila na wakwetu.

Walo wengi wanalia, fani waloisomea,

Hakuna nofurahia, ajira litegemea,

Mkaa mejipalia, maisha mewagemea,

Hili janga melichuma, nitalila na wakwetu.

Wanena tujiajiri, kitumbuliwa hulia,

Hupatwa na kisukari, presha hujipandia,

Wanaomba tafadhali, kwenye viti kubakia,

Hili janga melichuma, nitalila na wakwetu.

Mtaani yangu hadhi, kabisa hujishukia,

Ajira sio faradhi, haielewi jamia,

Na maneno yanoudhi, eti tulijifelia,

Hili janga melichuma, nitalila na wakwetu.

Zilochache zimetoka, na moyo zikatutia,

Wengine zikawafika, ajira mejipatia,

Uzalendo mejivika, na kazi wajifanyia,

Hili janga melichuma, nitalila na wakwetu.

Ismail Amiri Nyangasa (mnyonge kilingeni) Shule ya msingi swafaa (muheza-Tanga) 0658581814