http://www.swahilihub.com/image/view/-/4778758/medRes/2122569/-/11tnok5/-/umati.jpg

 

Shairi: Yatima

Wafanyakazi wa umati wakiwa na watoto yatima pamoja na walezi wa watoto yatima katika kituo cha watoto yatima Kurasini. Picha kwa Hisani ya Kituo cha Vijana,UMATI-TEMEKE  

Na Samson Alfred Shilla

Imepakiwa - Wednesday, September 26  2018 at  15:11

 

Hakuomba aje huku, sulubu kuzipokea,

Hesabuze chukuchuku, giza alipotokea,

Mbeleya pana ukungu, safari historia,

Haya tumwachie Mungu, hatimaye yatokea.

 

Wanadamu kumtenga, huzuni imetawala,

Maswaibu yamemsonga, kasi mpaka Mkangala,

Msemo mbele songa, msaadawe kwa sala,

Haya tumwachie Mungu, hatimaye yatokea.

 

Alipofika kafika, hatua moja muongo,

Tumaini amekata, matokeo ya msongo,

Simulizi amechoka, fununu tamu kamongo,

Haya tumwachie Mungu, hatimaye yatokea.

 

Amefuka furukuta, msaada kutafuta,

Njia finyu ya kupita, afanyalo ni kujuta,

Shidaze nyingi sakata, taifa lafukunyuka,

Haya tumwachie Mungu, hatimaye yatokea.

 

Familia ndio nguzo, msitupe hili fungu,

Nduguze ni nduguzo, bebeni hili jukumu,

Mpunguzeni msuto, kuiepuka hukumu,

Haya tumwachie Mungu, hatimaye yatokea.

 

Chozi lake ni ishara, maji yamemfikia,

Tusikubali hasara, mkono tunamshika,

Tushikane kwa mitara, majirani mashirika,

Haya tumwachie Mungu, hatimaye yatokea.

 

Janga acha mfukuto, Serikali kasikia,

Wadau msipite mkato, Yatima kumchangia,

Elimu ni ufunguo, kando tuweke pazia,

Haya tumwachie Mungu, hatimaye yatokea.

 

 Samson Alfred Shilla, 0682700930, Itigi, Singida.