Tufungapo Ramadhani

 

Imepakiwa - Monday, June 11  2018 at  16:29

 

Kufunga yataka nia, na ikhlaswi ya ndani,

Nashuruti kutimia, pamoja na arkani,

Yataka kujizuwia, na makatazo fulani,

Saumu ina undani, mungaswali nakufunga.

 

Funga katika sheria, nipana yake maani,

Kule kujizuwilia, na vipengele fulani,

Ibada ilo na Ria, huishilia dhambini,

Wema wake huuoni, mungaswali nakufunga.

 

Kithirisha ukarimu, kwa ndugu na majirani,

Uweze kuwakirimu, yatima na maskini,

Ufute yako athamu, na madhambi ya zamani,

Uime kuwa twaani, kwa kuswali na kufunga.

 

Kwa sababu ya swaumu, ametwambia amini,

Wenye kufunga timamu, wataingia janani,

Kwamlango  maalumu, jina lake ni Rayyani,

Kwahima tukazaneni, kwakuswali na kufunga.

 

Jambo lakusengenyana, na urongo kumbukeni,

Napia kutukanana, wakati wa ramadhani,

Dhambize ni kubwa sana, yatupasa tuacheni,

Mema tukithirisheni, tuswalipo nakufunga.

 

Umetukuzwa kwamno, mwezi mwema Ramadhani

Tupunguzeni maneno, ya upuzi na utanii, 

Ili tunali mavuno, mengi yasonakifani,

Kwashime tusimameni, kwakuswali nakufunga.

 

Ndio mwezi wamavuno, kwa waliyo waumini,

Naneema nyingi mno, zitokazo kwa manani,

Tupunguzeni maneno, ya uchafu midomoni,

Kutwa kucha ibadani, yakuswali nakifunga,

Bab Shali, Malenga wa Bajunini, Nairobi