http://www.swahilihub.com/image/view/-/4924772/medRes/2217554/-/d6nsoh/-/rafiki.jpg

 

Udugu si kufanana

Marafiki walioshibana kama ndugu 

Na Shaaban Maulidi

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  15:33

Kwa Muhtasari


 

shaabanmaulidi@gmail.com


Sifuri nayo nambari, angali hawaijali,

Inayo kubwa athari, kwa moja hata kwa mbili, 

Kumbuka pasi sifuri, laki haiwi kamili,

Udugu si kufanana, udugu ni kufaana.

 

Kuzaliwa kwa nasaba, undugu ulo timili,

Mmoja mama na baba, wazazi wenu wawili,
Undugu uso na haba, changanya zako akili,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana.

Undugu huu wa ada, tena unaulazima,
Udugu huu ibada, ufuate hima hima,
Udugu uwe ziada, si kupita wima wima,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana.

Udugu pasi mahaba, mithani yake adui,
Udugu uso kibaba, maana yake sijui,
Udugu ni msalaba, kubeba na hautui,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana.

Hata kama ni wa kambo, kaka au wako dada,
Hata iwe ni wa ng'ambo, undugu hauna kada,
Muhimu msingi jambo, kupeana msaada,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana.

Hata kama ni rafiki, au awe ni jirani,
Kabila la wazanaki, au wa umasaini,
Hata awe muiraki, undugu udumisheni,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana.

Hata kama ni Mkenya, au awe wa Uganda,
Mtusi sijemkanya, hata awe Mnyarwanda,
Mipaka utaipenya, undugu uwe wa kanda,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana.

Akiwa mkatoliki, wewe ni muislamu,
Udugu haibanduki, nyote ni binadamu,
Tofauti mashabiki, chadema na sisiemu,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana.

Daima msitupane, popote mtakapokuwa,
Vizuri msaidiene, mmoja akizidiwa,
Pamoja mkagawane, kidogo mlichopewa,
Udugu si kufanana, udugu ni kufaana.

Undugu wa faida, ule wa kujaliana,
Katika raha na shida, tuweze saidiana,
Undugu jua ibada, ukikata ni laana,
Undugu si kufanana, undugu ni kufaana.

Shaaban Maulidi
Lakabu: Nguo ya kuazima
0763902318/0718526259