BORA NIKUPE TALAKA

Na IDD NINGA WA TENGERU

Imepakiwa - Monday, December 12  2016 at  07:02

Kwa Muhtasari

Ndoa haina furaha, kila siku kugombana,

Bora nikupe talaka, japokuwa nakupenda.

 

NDOA haina furaha, kila siku kugombana,
Ndoa imejaa karaha, mara zote twalumbana,
Moyo wapata jeraha, kutwa kucha, twazozana,
Bora nikupe talaka, japokuwa nakupenda.

Kila siku najiuliza, kwa nini tulioana,
Ndoa imejawa kiza, na mapenzi yamenuna,
Nani wa kuniliaza,wewe mapenzi hauna,
Bora nikupe talaka, japokuwa nakupenda.

Sina budi sina njia, bora sasa kuachana,
Japokuwa wavutia, mapenzi ni kupendena,
Labda nitafurahia, japo hatutoonana,
Bora nikupe talaka, japokuwa nakupenda.

Moyo umekaa chini, siwezi tena na tena,
Itanishika huzuni, usiku hadi mchana,
Wasalimu wa mjini, wambe tumepigana,
Bora nikupe talaka, japokuwa nakupenda

Talaka yako chukua, kwa heri ya kuonana,
Japo mbingu zachukia, watu wanapoachana,
Roho yangu yaumia, ila nitakwaza sana,
Bora nikupe talaka, japokuwa nakupenda.

Na IDD NINGA WA TENGERU

Shairi limeidhinishwa na Stephen Maina, Mratibu wa Swahilihub

smaina@tz.nationmedia.com