http://www.swahilihub.com/image/view/-/3032504/medRes/1227769/-/oycpdt/-/kamata.jpg

 

CHOZI LA KARNE

Kiungambali

Kiungambali cha runinga. Picha/HISANI 

Na RICHARD BONIFACE KUMYOLA

Imepakiwa - Wednesday, April 11  2018 at  12:14

Kwa Muhtasari

Akilia na alia, mtoto kambeba mtoto,

Ukweli niufahamu, nani hapa ni salama?

 

FAMILIA silaumu, hata wewe u salama,

Ila sikitii sumu, mezani nikapahama,

Nitabaki nayo hamu, kuujua kwa tehama,

Ukweli niufahamu, nani hapa ni salama?

 

Kazaliwa huyu Siti, kumwita mama wa kesho,

Nyumba yao ya makuti, jembe lamtoa jasho,

Akaanza kutafiti, shule ajibiwa kesho,

Ukweli niufahamu, nani hapa ni salama?

 

Miaka kafika kenda, rafiki yake Mwamvua,

Sokoni kutwa kaenda, John akamjua,

Na mama akampenda, atakacho kanunua,

Ukweli niufahamu, nani hapa ni salama?

 

Na usiku watoweka, warudi kumeshakucha,

Siri sirini kaiweka, mama yake kaificha,

Umekaa kwa mkeka, wazipaka bure kucha,

Ukweli niufahamu, nani hapa ni salama?

 

Siku aliyo ingoja, yafika kama upepo,

Rafiki hajengi hoja, litupa na lake kopo,

Shingo yake kama moja, yupo ni kama hayupo,

Akijaribu jikongoja, analitoa tapiko,

Ukweli niufahamu, nani hapa ni salama?

 

Ndoto yake yapotea, analia kwa uchungu,

Njiani kapotelea, kichwa pigwa kwa lungu,

Mtoto kamkojolea, mtoto kizunguzungu,

Ukweli niufahamu, nani hapa ni salama?

 

Akilia na alia, mtoto kambeba mtoto,

Jamii yasimulia, ujana maji ya moto,

Hawajui ajutia, angekuwa kwa kidato,

Ukweli niufahamu, nani hapa ni salama?

 

Malezi sasa digiti, kisimbuzi rahisishe,

Maadili hayapiti, wazazi ni mishemishe,

Wakirudi kwenye viti, na runinga waiwashe,

Ukweli niufahamu nani hapa ni salama?

 

Kilio hiki kwa nani, alie tumsikie,

Ikawe vita vitani, shimoni tumfungie,

Kumbe sote taabani, maarifa kimbilie,

Ukweli naufahamu, hayupo hapa salama.

 

Mtunzi: Richard Boniface Kumyola +255763988244