http://www.swahilihub.com/image/view/-/4549648/medRes/1965486/-/gsuy4v/-/maganda.jpg

KARANGA ZA MAGANDA

Njugu karanga zenye maganda

Naulizia karanga, karanga zenye maganda. Picha/HISANI 

Na SHAABAN MAULID akiwa Tabora, Tanzania

Imepakiwa - Monday, May 7  2018 at  16:48

Kwa Muhtasari

Naulizia karanga, karanga zenye maganda,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

NAULIZIA karanga, karanga zenye maganda,

Hata kama za Iringa, Burundi hata Uganda,

Hata ziwe na mchanga, hizo ndizo nazipenda,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

Ziwe zimetoka shamba, sizitaki za mfuko,

Hata kama za Iramba, nazifata huko huko,

Ikiwa za Wanyiramba, kwangu hizo zina soko,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

Za maganda ndizo safi, tena zinazo utamu,

Haziliwi na walafi, kuzipata ni vigumu,

Ni za pekee herufi, ni halali si haramu,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

Mbolea hazijatiwa, hakuna alozigusa,

Tena zimebarikiwa, na mzee wa kanisa,

Dua zimeshaombewa, zimepita madrasa,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

Wala hajatua nzi, hazijarambwa na mende,

Wala hajatua panzi, niacheni nizipende,

Karanga zenye ulinzi, zaidi ya peremende,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

Nataka zilizo mbichi, zisiwe za kukaangwa,

Zenye ladha parachichi, si ladha ya machungwa,

Zitoke yoyote nchi, lakini isiwe jangwani,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

Za maganda ndizo tamu, ladha yake ya asili,

Kuzila siyo haramu, kwa Mungu hizi halali,

Hazina ladha ya ndimu, ladha yake ni asali,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

Mbichi bila ya mchuzi, katu haziwezi oza,

Zaidi hata ya ndizi, utamu mepitiliza,

Hazifanani na nazi, kwenye mboga zinakoza,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

Moyoni napata hamu, nikizila nanenepa,

Zinazoongeza damu, kusafisha na mishipa,

Tena zaondoa sumu, kuipa nyama mifupa,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

Tena zisiwe bidhaa, kufanyiwa biashara,

Za kula ndiyo zafaa, tena zenye ubora,

Zakumenywa nakataa, hizo kwangu ni hasara,

Karanga zenye maganda, sitaki zilizomenywa.

Shaaban Maulid,  Tabora Tanzania.

+255718526159 / +255763902318