http://www.swahilihub.com/image/view/-/4812958/medRes/2144939/-/hf7v6jz/-/gamba.jpg

 

KATUWACHA ISAAC GAMBA

Isaac Gamba

Marehemu Isaac Gamba wa Deutsche Welle, Bonn. Picha/HISANI 

Na RAMADHAN ABDALLAH SAVONGE

Imepakiwa - Thursday, October 25  2018 at  07:40

Kwa Muhtasari

Ayi tena ni kingoto, dunia kimetupiga,

Muhifadhi pema pake, ndugu Isaac Gamba.

 

AYI tena ni kingoto, dunia kimetupiga,

Kila bara ni majuto, mauko yametuzonga,

Isaac wetu mtoto, tunalia ameaga,

Muhifadhi pema pake, ndugu Isaac Gamba.

 

Tunamtambua sote, bwana Isaac Gamba,

Kipenzi cha watu wote, kwa khabari akitamba,

Tanzania bara lote, hatunaye ndugu Gamba,

Muhifadhi pema pake, ndugu Isaac Gamba.

 

Alitupasha khabari, za Swahili za dunia,

Saa kumi alasiri, saa saba mtawalia,

Kwa sauti yake nzuri, anga alizipasua,

Muhifadhi pema pake, ndugu Isaac Gamba.

 

Wajerumani walia, kifo chake kawatenda,

Majonzi kawaachia, na upendo wawavunda,

Baruwa ngew'andikia, kuwaaga unakwenda,

Muhifadhi pema pake, ndugu Isaac Gamba.

 

Pengo ameliwachia, Deutsche Welle mwengoyani,

Nafasiye kuzibia, abadani mtihani,

Maisha ni mshumaa, kamwe hukeshi gizani,

Muhifadhi pema pake, ndugu Isaac Gamba.

 

Rabbi tunakuombea, muepushe Gamba moto,

Msamehe lokosea, asiishi kwa majuto,

Mbele ametangulia, kaitika wako wito,

Muhifadhi pema pake, ndugu Isaac Gamba.

 

Ramadhan Abdallah Savonge, 'Malenga Wa Nchi Kavu',

Rununu: 0714408040

Baruabebe: savonge2@gmail.com

Chuo Kikuu SEKU - Kitui, Kenya.