http://www.swahilihub.com/image/view/-/2823674/medRes/1083815/-/2qe4ll/-/BDSpyCamera1706r.jpg

KESHO WAJA LINI?

Saa.

Saa. Picha/MAKTABA 

Na NAMALA SAMSON

Imepakiwa - Tuesday, May 8  2018 at  10:40

Kwa Muhtasari

Nataka na ndoa njema, nioe mke mzuri,

Hivi kesho waja lini? nami nikuishi vema!

KUNA jambo nitasema, kuleta nzuri habari,

Ingawa kama mapema, tuli ‘silete athari,

Nikaja shindwa hema, kwa kuvujisha habari,

Hivi kesho waja lini? nami nikuishi vema!

Najiuliza daima, kuona kesho dhahiri,

Shamba nataka lima, ila wadudu ta’thiri,

Ngoma zianze rindima, mipango jawa shubiri,

Hivi kesho waja lini? nami nikuishi vema!

Kuyafikiria mema, mipango jaza bahari,

Wema huzaa wema, mpaka kwisha dahari,

Nisije lichoma hema, kwa motowe kibatari,

Hivi kesho waja lini? nami nikuishi vema!

Nataka na ndoa njema, nioe mke mzuri,

Nimvishe chanda chema, watoto waje wazuri,

Na malezi yawe vema, wawe mfano mzuri,

Hivi kesho waja lini? nami nikuishi vema!

Kesho we huna huruma? maisha yawa kamari,

Sie daima ‘jituma, kwenye jangwa na bahari,

Saa siku hadi juma, twapita nyingi hatari,

Hivi kesho waja lini? nami nikuishi vema!

Kesho umenidanganya, nikapanga na mipango,

Na ndoto kuninyang’anya, ukanijaza msongo,

Kujificha kama panya, kwa kuzidi longolongo,

Hivi kesho waja lini? nami nikuishi vema!

Tabia ya kuyeyuka, ‘mekushtukia kesho,

Kalendani wasomeka, kama siku ya sipesho,

Leo ‘kishatimilika, kesho iwe marejesho,

Hivi kesho waja lini? nami nikuishi vema!

NAMALA SAMSON,

+255716748674,        naamala.samson@brac.net