http://www.swahilihub.com/image/view/-/4344458/medRes/1909594/-/aq7ajlz/-/zozana.jpg

 

KUMPA ASIYEKUPA

Wapenzi

Uchungu wa mapenzi hakuna asiyejua. Picha/HISANI 

Na KINYANJUI MURITHI NJUGUNA akiwa PUMWANI, NAIROBI

Imepakiwa - Wednesday, April 11  2018 at  06:39

Kwa Muhtasari

Kumpa asiyekupa, sawa sawa na kutupa,

Kumpa asiyekupa, ni kama uliyetupa.

 

KUMPA asiyekupa, sawa sawa na kutupa,
Penzi langu nimetupa, bure katili kumpa,
Zarina umenitupa, nabaki kutapatapa,
Kumpa asiyekupa, ni kama uliyetupa.

Penzi niliyempata, penzi langu nikampa,
Alinipeleka puta, sababu hakunilipa,
Tabu sana nikapata, sitapenda ninaapa,
Kumpa asiyekupa, sawa sawa na kutupa.

Zarina ameniacha, sijui nifanye nini,
Silali usiku kucha, usingizi siuoni,
Na kila kunapokucha, hali yangu taabani,
Kumpa asiyekupa, hiyo ni kama kutupa.

Nilivyompenda sana, mwengine simtamani,
Hali yangu naiona, nitatoka duniani,
Fanya huruma Zarina, unionee imani,
Kumpa asiyekupa, ni kama uliyetupa.

Shida hazisemekani, kumpa asiyekupa,
Hilo tokea zamani, ujue umeshatupa,
Nimeyaona jamani, na Zarina hakunipa,
Kumpa asiyekupa, hiyo sawa na kutupa.

Mpeanao toeni, mimi yameshanifika,
Sasa hali taabani, kakataa ushirika,
Wenye kutoa toeni, mwisho ni kukasirika,
Kumpa asiyekupa, sawasawa na kutupa.