WASWAHILI TUPO

Na Rasi Saidi Raphael Mbwana

Imepakiwa - Monday, June 5  2017 at  11:14

Kwa Mukhtasari

SHAIRI la Mswahili, natunga kutoka Tanga,

Niwasalimu wa mbali, Mombasa, Kwale na Vanga,

 

Mnijuzeni hali, nudhumu mkizitunga,

Tupo wengi Waswahili, tulipo twajulikana.

 

Zanzibari  nawasili, mafundi wajua kunga,

Ngazija msiwe tuli, msiche kutunga,

Mtumie Kiswahili, si maneno kuboronga,

Tupo wengi Waswahili tulipo twajulikana.

 

Msopenda Waswahili, na kupita kutupinga,

Mmejawa ufidhuli, na matusi kuyapanga,

Enyi ndumilakuwili, zenu roho za watanga,

Tupo wengi Waswahili, tulipo twajulikana.

 

Wapo tena wao nguli, majagina  na nyakanga,

Wenye sifa tajamali, walofunzwa na wahenga,

Hassani nguli wa kweli, sifa zake zimetanga,

Tupo wengu Waswahili, tulipo twajulikana.

 

Ndugu Mbaruku Ali, Mswahili asoringa,

Mwenye tungo taamuli, anajua kuzitunga,

Zikawaka ja kandili zikatoa wake mwanga

Simba asiye timbwili, mwenda pole kwa kuringa.

 

Hapendi yeye zohali, Mswahili wa Kitanga,

Kamakinika njali, amepikwa na waknga,

Tupo wengi Waswahili, tulipo twajulikana

Hapa nafunga kufuli, Waswahili nimelenga.

 

Rasi Saidi Raphael Mbwana,

Chuo Kikuu Dodoma.