http://www.swahilihub.com/image/view/-/2581258/medRes/916471/-/si07ioz/-/RTPCouple2%25282%2529.jpg

 

MCHAWI AU MUONGO?

Siri ya ndoa

Wanandoa changa. Picha|HISANI 

Na SALEE MSUYA JUMA akiwa MARIKITI, MUTHURWA, NAIROBI

Imepakiwa - Wednesday, April 11  2018 at  06:39

Kwa Muhtasari

Kati ya hawa wawili, nauliza wahisani,

Mchawi au muongo, bora nimuoe nani?

 

KATI ya hawa wawili, nauliza wahisani,
Nataka yenu kauli, hapa nimuoe nani,
Muongo kipilipili, na mchawi bora nani,
Mchawi au muongo, bora nimuoe nani?

Mchawi mshirikina, niambieni jamani,
Au muongo fitina, mzuri hapa ni nani,
Nani nimpende sana, nioe niweke ndani,
Mchawi au muongo, hapa mzuri nani?

Mchawi hana huruma, ukimuudhi nyumbani,
Fitina naye lawama, kila siku majirani,
Majirani walalama, hapa petu mtaani,
Mchawi au muongo, hapa mzuri nani?

Hapa wote walalama, fitina za mtaani,
Na mchawi wanasema, aturogaye ni nani,
Toka jana ni mzima, ameuwawa na nani,
Mchawi au muongo, bora nimuoe nani?

Muongo ndiye fitina, huogopea nyumbani,
Mchawi mshirikina, yote ni yao jueni,
Nipeni mwenye maana, nani nimuweke ndani,
Mchawi au muongo, bora nimuoe nani?

Habari zangu ni hizo, nimeuliza jamani,
Nangojea maagizo, mzuri nioe nani,
Zuri lenu pendekezo, nalingoja wahisani,
Mchawi au muongo, bora nimuoe nani?