http://www.swahilihub.com/image/view/-/1413928/medRes/363940/-/atkp83/-/Dn2Khatmiraa5.jpg

 

MIRAA KWA WANAWAKE, PUMWANI

miraa

Mmea wa miraa ukiwa shambani. Picha/MAKTABA 

Na LEONARD MWANGI NDERITU

Imepakiwa - Tuesday, September 13  2016 at  10:12

Kwa Mukhtasari

Miraa kwa wanawake, Pumwani imekithiri,

Miraa kwa wanawake, mimi sioni vizuri.

 

MIRAA kwa wanawake, Pumwani imekithiri,
Njoo uone ucheke, jambo hili sio siri,
Heshima ya wanawake, mno wamekithiri,
Miraa kwa wanawake, mimi sioni vizuri.

Wamekuwa hawalali, kuitafuta migoka,
Hawanitii shughuli, rahisi ukiwataka,
Bora umpe asali, ya majani ya mugoka,
Miraa kwa wanawake, mimi sioni vizuri.

Haya ninayotamka, ni ukweli si utani,
Njoo kama unataka, ujione machoni,
Pumwani ukishafika, utapatwa na huzuni,
Miraa kwa wanawake, mimi naona huzuni.

Wageni wanapofika, hapo kwao mtaani,
Bwana utahuzunika, haya nayo mambo gani,
Wameza bila kuchoka, Miraa barabarani,
Miraa kwa wnawake, aibu hapa Pumwani.

Kazi ni kuzunguka, hawakai majumbani
Na waume kadhalika, sijui niseme nini
Kazi yao kina kaka, hulala kutwa nyumbani
Miraa kwa wanawake, mimi sioni vizuri

Mabibi na kina kaka, nawaaga kwaherini
Pumwani nimeondoka, nimerudi mashambani
Hayo niliyotamka, nimeyaona machoni
Miraa kwa wanawake, si mizuri asilani.

Leonard Mwangi Nderitu
Nyeri Endarasha.