http://www.swahilihub.com/image/view/-/4706282/medRes/1253131/-/am86qp/-/DN2KsmCEMETRY2211ac%25286%2529.jpg

 

MJA HUFA KWA AHADI

Makaburi

Mavani. Picha/MAKTABA 

Na SALIM HUSSEIN NG'ANZI

Imepakiwa - Monday, September 10  2018 at  12:21

Kwa Muhtasari

Hafi mja asilani, siku isipowadia,

Mja hufa kwa ahadi, iloandikwa na Mola.

 

HAFI mja asilani, siku isipowadia

Hadi apange Manani, ndipo mja kujifia,

Ukidondoka ujani, ndipo waaga dunia,

Mja hufa kwa ahadi, iloandikwa na Mola.

 

Mja ana yake saa, duniani kutoweka,

Saa iliyo fadhaa, Maulana kaweka,

Mara yajapo fajaa si lazima kuzeeka,

Mja hufa kwa ahadi, iloandikwa na Mola.

 

Muda usipokutimu, aga dunia huwezi,

Hata upatwe wazimu, paka apange Mwenyezi,

Hii ghaibu elimu, na haina mtetezi,

Mja hufa kwa ahadi, iloandikwa na Mola.

 

Mja hawezi fariki, asipopenda Wadudi,

Ugongwe kwa pikipiki, unywe sumu makusudi,

 Asipoweka tiki, na kuishi huna budi,

Mja hufa kwa ahadi, ilo andikwa na Mola.

 

Gari lako lipinduke, korongoni pitiize,

Ghorofani uanguke, bichwa lako libamize,

Gari lako limeguke, guu lako liumize,

Mja hufa kwa ahadi, iloandikwa na Mola.

 

Waweza pigwa risasi, panga waweza charangwa,

Waweza gongwa na basi, chunguni weza kaangwa,

Kifo hakina nafasi, kama muda hujapangwa

Mja hufa kwa ahadi, iloandikwa na Mola.

 

Kitanzini jitundike, mtini kamba pachika,

Acha kamba ilike, hatimaye kukatika

Hadi ahadi ifike, ndipo tuweze kuzika,

Mja hufa kwa ahadi, iloandikwa na Mola.

 

Siku yako ikifika, yawa mepesi mauti,

Hata mtu kakushika, au kupigwa kibuti,

Hata jogoo kuwika, ikakuuwa sauti,

Mja hufa kwa ahadi, iloandikwa na Mola.

Salim Hussein Ng’anzi (Jemadari)

Simu: +255719 867 477 AU 0626  884 160.