http://www.swahilihub.com/image/view/-/2758636/medRes/1040993/-/hpl66o/-/nyonyesha.jpg

 

MWANANGU

Mwanamke amnyonyesha mtoto

Mwanamke amnyonyesha mtoto. Picha/MAKTABA 

Na JUMAA HASSAN 'TARISHI WA MANGA' akiwa AMBONI, TANGA

Imepakiwa - Thursday, March 8  2018 at  09:52

Kwa Muhtasari

Mgongoni ana mwana
Bado kupo na kulima.

 

KWANZA ninanyenyekea
Kwa Mungu anaelea
Kisha nawasalimia

Natumai msalama.

Mwajiuliza ni nani
Nilo hapa uwanjani
Pia nimeleta nini

Jambo lilojaa ne'ma.

Mimi ndie Tanzania
Taifa m'lokulia
Leo nina moja nia

Kuwafunda kihekima.

Kuna wanangu wapendwa
Naona wapindwapindwa
Kisha nao wakashindwa

Kupambania hujuma.

Nyumbani ninawaona
Kazi zimesongamana
Mgongoni ana mwana
Bado kupo na kulima.

Waliopo ndanindani
Hujifungua njiani
Mama na alotumboni
Kifo kinawaandama.

Leba atakayefika
Huduma zimechujuka
Mama anadhalilika
Lini haya yatakoma.

Tena wapo wasichana
Mwezi wanapouona
Taulo huwa hawana
Bei imezidi kima.

Unyanyasaji wa ngono
Bosi katega mgono
Na waume waso meno
Vitoto wanavichoma.

Vipi na hili balaa
Mwana shule anafaa
Baba'ke akakataa
Wa kike hendi kusoma.

Nimewafaa makazi
Aridhi iliyo wazi
Ila hili moja shazi
Mbona mnalisukuma?

Yule yupo utawani
Hauzi hata ukuni
Biashara iso duni
Khadija hakuchutama.

Namuona anakopa
Nashauri m'ngempa
Au riba kutolipa
Afane kiumbe mama.

Nisikilize mwanangu
Kujiondoa kiwingu
Yakutoke na machungu
Upambane himahima.

Zikatae tamaduni
Zinofanya uwe duni
Kukatwa visu kwanini
Mke anatokwa ngama.

Kama wakikupuuza
Na shule kukutaza
Dawa ni kujiapiza
Kidete ukasimama.

Katu msifarakane
Bali msaidiane
Na mikono mshikane
Kama pepo mtavuma.

Mwanangu usibweteke
Pambana usidhurike
Uelimishe utoke
Umma wa akia mama.

Mwana wangu wakiume
Mwenzio usimuume
Msaidie ademe
Mpande wote kilima.

Tamati nawakumbusha
Mama kumshajiisha
Mwisho najikurubisha
Kwa Mola wetu Karima.

Mtunzi: Jumaa Hassan Heshima
(Tarishi Wa Malenga)
Amboni, Tanga.
+255714638277