http://www.swahilihub.com/image/view/-/3822690/medRes/1570316/-/8lum99z/-/himo.jpg

NAKUJA KUOA KENYA

Holili

Magari ya mizigo yakiwa Holili hapo njiapanda kuelekea Taveta nchini Kenya. Picha/MTANDAO 

Na IDD NINGA akiwa Arusha, Tanzania

Imepakiwa - Tuesday, May 8  2018 at  12:11

Kwa Muhtasari

Acha niseme ukweli, nitue huu mzigo,

Nakuja kuoa Kenya, Wabongo wamenishinda.

ACHA niseme ukweli, nitue huu mzigo,

Naenda kuoa mbali, huku nakupa kisogo,

Nawabwaga chini chalk, nashusha yangu mapigo,

Nakuja kuoa Kenya, Wabongo wamenishinda.

Huku wengi omba omba, wanapenda kutuchuna,

Wanapenda omba omba, kwa hilo ninawachana,

Japokuwa wapo bomba, ila upendo hakuna,

Nakuja kuoa Kenya, Wabongo wamenishinda.

Wabongo waringa sana, wataka mahari kubwa,

Wanapenda vilivyonona, kuku baga na ubwabwa,

Kwa mahari washindana, shindwa wakwone jibwa,

Nakuja kuoa Kenya, Wabongo wamenishinda.

Wanaweza kutajia, mahari mamilioni,

Kama wanatukomoa, twajifanya hatuoni,

Kenya nakuja kuoa, mke nimpe thamani,

Nakuja kuoa Kenya, Wabongo wamenishinda.

Hawana penzi la kweli, huku wanawaza pesa,

Jitie we ujahili, uone watakutesa,

Nakuja kuoa mbali, bila jicho kupepesa,

Nakuja kuoa Kenya, Wabongo wamenishinda.

Sura zao za dukani, tena ghali waziuza,

Najitoa mashakani, sitaki mauza uza,

Wajiona wa thamani, na utu waupuuza,

Nakuja kuoa Kenya, Wabongo wamenishinda.

Nimechagua wakenya, wanaojua kulea,

Namanga ninaipenya, Nairobi nasogea,

Watanga ninawaonya, wameshaji haribia,

Nakuja kuoa Kenya, Wabongo wamenishinda.

Bongo wanaringa ringa, na midomo wabenua,

Nakipuliza kipenga, ili kesho waje kua,

Wametupa ya wahenga, yuropa wamechukua,

Nakuja kuoa Kenya, Wabongo wamenishinda.

IDD NINGA, Arusha, +255624010160

iddyallyninga@gmail.com