http://www.swahilihub.com/image/view/-/3406064/medRes/1168738/-/3t9je1/-/MagufuliRais.jpg

 

RAIS WETU NI MUSA, ALIYETUMWA MISRI

Rais John Magufuli akitoa hotuba

Rais John Magufuli akihutubu awali. Picha/AFP 

Na MWALIMU JACKSON CHACHA FRANCIS

Imepakiwa - Thursday, November 1  2018 at  14:10

Kwa Muhtasari

Na umeme wa kutosha, Tanzania ya viwanda,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

NA Musa ninakuambia, watu wangu wateseka,

Watu wangu wanalia, Misri kuna shabuka,

Kilio nimesikia, watu wangu wasifika,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Najua mateso yao, nashuka kuwaokoa,

Akawarudishe kwao, Misri akawatoa,

Nitawapa nchi yao, ni kubwa tena murua

Nchi itiririkao, maziwa asali pia

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

John Pombe Magufuli, kaleta demokrasia,

Zaonekana dalili, vyama vingi vimejaa,

Ruzuku anafadhili, upinzani kukwamua,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Mfumo wa vyama vingi, Serikali kapokea,

Wabunge pinzani wengi, kazi zao twatambua,

Wafanya shughuli nyingi, Rais azitambua,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Dini zote jama huru, Rais azitambua,

Dini hajawahi dhuru, mchamungu asilia,

Kuabudu ni uhuru, Rais katupatia,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Na haki za binadamu, ni nguzo ya Tanzania,

Na utawala kadumu, utawala wa sheria,

Kajaliwa na kaumu, Magufuli Tanzania,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Ni mwanademokrasia, mzalendo asilia,

Magufuli kachagua, utawala wa sheria,

Ni kiongozi shujaa, Mungu katupa adia

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Ulinzi na Usalama, ni imara Tanzania,

Magufuli kajituma, ulinzi wetu murua,

Kafanya ima fa ima, Jeshi letu kakomboa,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Tanzania inalinda, usalama duniani,

Askali wanatenda, dunia kukomboeni

Na ulinzi ndio tunda, linalozaa amani

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Upande kufungamana, siasa ulimwenguni,

Mabepari twapendana, wajamaa karibuni,

Ninatamka kwa kina, migororo nje na ndani,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Vizuri vya Magharibi, Rais avichukua,   

Nalo so shamba la bibi, Magufuli kazuia,

Yeye chaguo la Rabi, kiongozi Tanzania

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Magharibi Mashariki, Rafiki wa Tanzania,

Tunayotaka ni haki, wasije kutuibia ,

Tanzania sio keki, wageni kujigawia,

 Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri. 

 

Twapenda utandawazi, dunia sasa ni moja,

Biashara ni azizi, tumeujenga umoja,

Na ameujenga uwazi, manufaa tunangoja,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Jama bomba la mafuta, Uganda litatokea,

Magufuli kalileta, hapa kwetu Tanzania,

Na faida tutapata, na kuinua uchumi,

Rais wetu ni Musa,aliyetumwa Misri.

 

Stiegel Gorge, Rais ameamua,

Lijengwe mto Rufiji, Bwawa litatuzalia,

Umeme kwenye vijiji, viwanda kujipatia,

 Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Na umeme wa kutosha, Tanzania ya viwanda,

Na uchumi wa kutisha, jamani tunaupenda,

Jama katufurahisha, Rais tunakupenda,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Kilimo cha manufaa, faida cha tupatia

Na dhamani ametia, mazao ameinua,

Viwanda twasindikia, na nchi za nje kuuzia,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Mazao ghafi hakika, tusiyauze sokoni,

Mazao tunasindika, tuongezee dhamani,

Rais ametamka, tuenzi yake imani,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Tanzanite Mirerani, ukuta kazungushia,

Kaliweka akilini, wazo lake ni murua,

Ameyalinda madini, waporaji wanalia,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Mbuga zetu za wanyama, na ngo’mbe wakavamia

Bila kuona huruma, wanyama walikimbia,

Rais mwenye hekima, Ng’ombe kawaondoa,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Amelinda mazingira, nayo inanyesha mvua,

Mazao yaliyobora, mengi tutajipatia,

Kilimo sasa imara, wakulima furahia,

Rais wetu ni Musa,aliyetumwa Misri.

 

Watalii mbalimbali, watoka ulimwenguni,

Tanzania ni ya pili, vivutio duniani

Watalii mbalimbali, tunawapata wageni,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Ndege saba kanunua, watalii kuwaleta,

Maendeleo ni nia, Magufuli ameleta

Na wapinzani sikia, hamuwezi mkapita,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Barabara nzuri sana, Magufuli amejenga,

Amejenga lami hasa, mikoa ameiunga,

Katumia nyingi pesa, maendeleo kulenga,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Nalo soko la dunia, ni duni vyetu vizaa,

Mabepari kuibia, Magufuli kazuia,

Raslimali Tanzania, watakakutuibia,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Ulaya na Marekani, biashara si murua,

Unyonyaji ni kiini, mabepari kaamua,

Wametutia huzuni, adabu atawatia,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Wavuvi wote haramu, nyavu ndogo na mabomu,

Siku zao zimetimu, jama kutumia sumu,

Wamefanya stakimu, maji yetu waujumu,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Rais ameamua, kulinda samaki wetu,

Samaki sasa wakua, ni raslimali yetu,

Uzito wao murua, ina manufaa tu

Rais wetu ni Musa,aliyetumwa Misri.

 

Elimu sasa ni bure, Magufuli kaamua,

Ni mawazo ya Nyerere, Magufuli katumia,        

Elimu iliyosare, taifa itainua,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Watoto ni wengi sana, wengi kajiandikisha,

Amejenga madarasa, walimu watafundisha,

Ni elimu ya kisasa, elimu inatutosha,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Ukienda mashuleni, vitabu si shida sana,

Katupa matumaini, elimu yetu mwanana,

Na tumepata imani, mchango mkubwa sana,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Maabara amejenga, sayansi kufundishia,

Sayansi ameilenga, hapa kwetu Tanzania,

Viwanda amevilenga, sayansi amenuia,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Madawa ni ya kutosha,huko hospitalini,

Magonjwa  kayaponyesha, sasa tupo afueni,

Twajisikia bashasha, Rais madarakani,

Rais wetu ni Musa,aliyetumwa Misri.

 

Waganga wenye ujuzi, kaajiriwa hakika,

Taaluma zao azizi, jama hatuna mashaka,

Jamani na kila mwezi, magonjwa yanatibika,

Rais wetu ni Musa,aliyetumwa Misri.

 

Jama vitendea kazi, hospitali kajaa,

Na inafanyika kazi, magonjwa kuyatibia,

Twapongeza laazizi, Hisani kutufanyia,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Ndoo katua kichwani, wanawake Tanzania,

Twanywa maji ya bombani, wanawake yamepungua,

Twakuenzi maishani, mazuri kututendea,

Rais wetu ni Musa,aliyetumwa Misri.

 

Nchi sasa ni salama, vyombo vyote vya ulinzi,

Tunafurahia umma, dawamu tutakuenzi,

Jeshi letu ndio mama, limesheheni mapenzi,

Rais wetu ni Musa,aliyetumwa Misri.

 

Mipaka yetu  kalindwa, kwa silaha za kisasa,

Na jeshi letu kaundwa, na wazalendo kabisa,

Rais wetu mpendwa, yeye ni imara hasa,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Kaditama nimefika, Magufuli napongeza,

Kajaliwa na Rabuka, vizuri katuongoza,

Jama mbali tutafika, sote tunakupongeza,

Rais wetu ni Musa, aliyetumwa Misri.

 

Afisaelimu vifaa na Takwimu wa sekondari

Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo.