http://www.swahilihub.com/image/view/-/4699868/medRes/2070748/-/7hjww1/-/maveve.jpg

 

TABU ZA KUJITAKIA

Muguka

Maafisa wa kudumisha sheria na kanuni katika kaunti ya Mombasa waharibu kibanda cha kuuzia muguka Agosti 6, 2018, eneo la Tononoka. Picha/WACHIRA MWANGI 

Na ABU JAFARI HUBA

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  14:36

Kwa Muhtasari

Nimewaona walao, walaji wa mairungi,

Tabu ya kujitakia, mtu haambiwi pole.

 

NIMEWAONA walao, walaji wa mairungi,

Yamekwisha meno yao, yameshang’oka kwa wingi,

Hawaoni shida hiyo, walaji wa mairungi,

Tabu ya kujitakia, mtu haambiwi pole.

Ni ukweli shida hiyo, ya meno kwa ni nyingi,

Na hata mabibi zao, wapendao mairungi,

Wengi wao meno yao, yamebadilika rangi,

Tabu ya kujitakia, mtu haambiwi pole.

Ni wengi niwajuwao, walo marafiki zangu,

Wameacha kazi zao, pamwe na jirani zangu,

Wakilala watu hao, kuamka ni mizungu,

Tabu ya kujitakia, mtu haambiwi pole.

Kuna mingine rahisi, inayoitwa migoka,

Hiyo hawali wakwasi, wenye pesa watajika,

Ina ulevi wa kasi, mikali sana migoka,

Tabu ya kujitakia, mtu haambiwi pole.

Wengi wao vibogoyo, miraa wanaitwanga,

Mlaji haini hayo, pesa anazibananga,

Mdomoni hamna meno, kama mtoto mchanga,

Tabu ya kujitakia, mtu haambiwi pole.

Kwaheri watafunaji, migoka na mairungi,

Sijui yenu faraji, ya kuyala mairungi,

Ni mapesa ufujaji, mnazifuja kwa wingi,

Tabu ya kujitakia, mtu haambiwi pole.

ABU JAFARI HUBA

Pumwani, Nairobi