UTENZI KWA WASIOJIWEZA

Na HAMIS KUNDAI

Imepakiwa - Monday, October 24  2016 at  15:57

Kwa Muhtasari

Wazee wameridhika

Wazima wavutiya

 

BAADA ya Mapinduzi yalifanyika mambo mengi ya kimaendeleo kama ilivyoelezwa katika beti zilizotangulia.

Hata hivyo kumekuwa na juhudi za kuhudumia watu wenye maisha magumu kama yatima, wazee na walemavu. Endelea kusoma:

 1. Wazee wasojiweza
  Serikali ikawaza
  Bora kuwatengenezea
  Majumba kuwajengeya.

 2. Watoto walo yatima
  Waso baba na mama
  Imetenda jambo jema
  Serikali kuwalea.

 3. Kila aso uwezo
  Hupata kibembelezo
  Kwa fedha zilizo mzo
  Maisha kufurahiya.

 4. Pesa hizo kila mwezi
  Hupewa bila ajizi
  Walipia matumizi
  Kwa wanachohitajiya.

 5. Msaada kila kabila
  Watu hupewa hela
  Hupata bila madhila
  Nao hufurahiya.

 6. Raia wote wa radhi
  Kupata yao faradhi
  Utu wao una hadhi
  Heshima imerejea.

 7. Mwiko tena hawaombi
  Majiani hawatambi
  Jambo hilo kwao dhambi
  Na sasa wametuliya.

 8. Si usiku si mchana
  Naapa hutawaona
  Kwani wao waungwana
  Neema imewangiya.

 9. Wazee wameridhika
  Kwa kupata yao faka
  Miili imekarambuka
  Wazima wanavutiya.

 10. Mtambo wa televisheni
  Umejengwa visiwani
  Seti zimo majumbani
  Watu wanajionea.

 11. Umejengwa kwa gharama
  Kutumia kwa kusoma
  Masomo yenye neema
  Tija yatatuleteya.

 12. Taaluma ya siasa
  Tutachambua kurasa
  Ili tuwe na hamasa
  Ya nchi kujijengeya.

 13. Itasomesha sayansi
  Wana wapate kupasi
  Tena upesi upesi
  Ajizi kuwondokeya.

 14. Tahifadhi mila yetu
  Silika za babu zetu
  Tudhibiti utu wetu
  Na mema kujifanyiya.

 15. Pia itafurahisha
  Vipindi vya kuchekesha
  Watu kuwaburudisha
  Roho zipate tuliya.

 16. Kiwanda cha kuhifadhiya
  Matunda yetu baadhi
  Kitajengwa kutukidhi
  Mali yetu kuwekeya.

 17. Zitahifadhiwa embe
  Kwenye mikebe zirembwe
  Tuzitowelee sembe
  Kwa ladha inovutiya.

 18. Machungwa na mananasi
  Hata piya mafenesi
  Yatawekwa kwa nafasi
  Makoponi kuingiya.

 19. Samaki watovuliwa
  Tutawafanyia dawa
  Na vibatini kutiwa
  Waache kutuozeya.

 20. Samaki tasafirisha
  Baada ya kukaushwa
  Watu watatamanishwa
  Nje kujinunuliya.

 21. Na vijiwanda vidogo
  Navyo vitatupa nogo
  Biskuti za mihigo
  Vitatutengenezeya.

 22. Tutatengeneza mafuta
  Siyo ya kukukereta
  Uhondo tutaupata
  Kwa vyakula kupikiya.

 23. Piya mafuta ya nywele
  Siyo yale ya uwele
  Hutoa hata upele
  Kichwani yakiingia.

 24. Sabuni za kuogeya
  Na piya za kufuliya
  Na hata za kuosheya
  Zote tutajipatiya.

 25. Viwanda hivyo vidogo
  Mambo yake si madogo
  Ni viwanda vya mikogo
  Faida kutuleteya.

 26. Meli kutoka Japani
  Na sasa kiwandani
  Yamalizwa usukani
  Karibu tatufikiya.

 27. Meli tuloinunuwa
  Makusudio ni kuwa
  Watu itawachukuwa
  Wao na mizigo piya.

 28. Meli hiyo kubwa sana
  Kwa urefu na upana
  Watu hawatobanana
  Kwa nafasi taingiya.

 29. Haitakuwa na zogo
  Kwa nafasi ya mizigo
  Hata yakiwa magogo
  Melini yataingiya.

 30. Nafasi ya kulaliya
  Ipo bila ya udhiya
  Vitanda vimeeneya
  Vururu wajipatiya.

 31. Mizigo takaa mbali
  Haichanganywi asili
  Itatengwa kweli kweli
  Mbali na abiriya.

 32. Safari ilo ya raha
  Iliyojaa buraha
  Safi isiyo karaha
  Huku meli yaeleya.

 33. Na televisheni ndani
  Kama mmo majumbani
  Lipi la kukughasini
  Kwa raha mwajioneya.

 34. Uovu kila namna
  Nchini haupo tena
  Watu wote wapendana
  Imani imeeneya.

 35. Zimeondoka fitina
  Za watu kuchukiana
  Na wengine kusutana
  Yote yameshapoteya.

 36. Zimeondoka hasama
  Na hata pia lawama
  Imerejea heshima
  Nyoyo zote metuliya.

 37. Uchafu umeondoka
  Kulewa na kutapika
  Wapi! Umemalizika
  Ibada metanguliya.

 38. Ulevi hautakiwi
  Tende katu huuziwi
  Hata dawa hupewi
  Watu wameikimbiya.

 39. Na bangi yenye madhara
  Ati huitwa sigara
  Imepigwa kipapara
  Haipo imepoteya.

 40. Bangi watu hawavuti
  Majiani na buyuti
  Kwani ina tasiliti
  Mtu wazimu hungiya.

 41. Wameona maradhiye
  Hasa hasa hatimaye
  Huyaponza maishaye
  Mtu hata hujifiya.

 42. Bangi hukupa kichaa
  Na mwisho ukapumbaa
  Kwa wazimu kukujaa
  Maishayo kupoteya.

 43. Na hata hiyo kasumba
  Ikivutwa na mitemba
  Sasa imepigwa kamba
  Visiwani mepoteya.


  Na Hamis Kundai

  Tanzania, Afrika Mashariki

  Imepitiwa na kuidhinishwa na Stephen Maina