Wimbo wa Taifa

Na BEATUS KUSAGA, UDSM

Imepakiwa - Friday, November 24  2017 at  12:07

Kwa Muhtasari

Albino wapata tabu, twasema tuna amani,

Huu wimbo wa taifa, dhumuni lake ni nini?

NA sasa ipo sababu, ya kusema hadharani,

Tumeikosa adabu, hekima na umakini,

Migomo ya matabibu, na ugomvi wa kidini,

Huu wimbo wa taifa, dhumuni lake ni nini?        

Hakuna ustaarabu, tujiulize kwa nini,

Hatufati taratibu, sheria ni mikononi,

Sitopenda kuwa bubu, ukweli ndo nawapeni,

Huu wimbo wa taifa, dhumuni lake ni nini?

Mabibi hata mababu, hofu kwao moyoni,

Yapi yanayowasibu, kwa wekundu machoni,

Wanapigiwa hesabu, wapotezwe duniani,

Huu wimbo wa taifa, dhumuni lake ni nini?

Kipi kinachowasibu, ulinzi serikalini,

Albino wapata tabu, twasema tuna amani,

Munaikosa thawabu, kwa mbaya zenu imani,           

Huu wimbo wa taifa, dhumuni lake ni nini?

Huwa napata ghadhabu, fisadi mahakamani,

Kwao siyo maajabu, hata kwa makosa gani,

Hutoka bila tabu, thubutu aseme nani,

Huu wimbo wa taifa, dhumuni lake ni nini?

Chachu yangu ni wajibu, viongozi tambueni,

Msitufanyie ghubu, kilimo sisitizeni,

Mnajuana Waarabu, kwa vilemba vichwani,

Huu wimbo wGrace Mugabe. File: AFPa taifa, dhumuni lake ni nini?

Walimu nao ghadhabu, madai yao kapuni,    

Wapeni basi jawabu, elimu pande thamani,      

Msijidai mabubu, jukumu hili la nani,

Huu wimbo wa taifa, dhumuni lake ni nini?     

Imekuwa aghalabu, vijana wa mitaani,

Kuendeleza ulabu, elimu yao kapuni,

Nini kama si ajabu, na kupoteza thamani,

Huu wimbo wa taifa, dhumuni lake ni nini?

Mbona mnatusulubu, madini yako nyumbani,

Hamuishiwi sababu, eti nchi masikini,            

Acheni hizo taarabu, na wizi wa hadharani,

Huu wimbo wa taifa dhumuni lake ni nini?

Hebu tuweni karibu, tukwepe umasikini,

Kwa Mungu pia tutubu, tuyaogope madeni,

Nani atakayejibu swali nawaulizeni,

Huu wimbo wa taifa, dhumuni lake ni nini?

Nikipata majaribu, werevu niteteeni,

Someni sana vitabu, mengi mtayajueni,

Fasihi haina tabu, inaweka hadharani,

Huu wimbo wa taifa, dhumuni lake ni nini?

Beatus Kusaga, UDSM