http://www.swahilihub.com/image/view/-/3492826/medRes/1516916/-/sucrw8z/-/jaha.jpg

 

Maudhui ya Elimu katika Kidagaa Kimemwozea

Kidagaa Kimemwozea

Jalada la riwaya ya Kidagaa Kimemwozea. Picha/HISANI 

Na KEN WASIKE

Imepakiwa - Tuesday, December 20  2016 at  15:34

Kwa Mukhtasari

Elimu ni muhimu sana kwa binadamu. Mwandishi wa riwaya ya Kidagaa Kimemwozea anaonyesha kuwa elimu inayopewa kipaumbele katika jamii ni ile ya darasani; elimu inayopatikana vitabuni.

 

ELIMU ni muhimu sana kwa binadamu. Mwandishi wa riwaya ya Kidagaa Kimemwozea anaonyesha kuwa elimu inayopewa kipaumbele katika jamii ni ile ya darasani; elimu inayopatikana vitabuni.

Hata hivyo, wengi hawatambua kuwa wakati mwingine elimu hii inaweza kuwa ghushi na kwa kujaa upotofu.

Suala la elimu linadhihirika kupitia kwa wahusika mbalimbali, kwa mfano Majisifu anayepelekwa ng’ambo na marehemu babake kusomea ukasisi na kupata shahada.

Mtemi anasoma mpaka darasa la nane.

Madhubuti naye anasomeshwa hadi chuo kikuu huko Urusi kwa pesa walizotozwa wakazi wa Sokomoko ambao ni maskini.

Vilevile Mtemi Nasaba Bora anamsomesha bintiye, Mashaka ambaye anaamua kujiingiza katika mapenzi na kuishia kidato cha tatu.

Mwandishi anadhihirisha kilio chake kuelekea tanzia iliyokumba elimu katika jamii.

Jambo la kwanza linaloangaziwa ni ufaafu wa walimu waliotwikwa jukumu la kuwafundisha wanafunzi madarasani.

Hapa ndipo tumpatapo Fao, rafikiye Amani wa utotoni. Fao, baada ya kupewa jukumu kufundisha katika shule ya Sekondari ya Kinondani kwao Ulitima, anajigeuza paka wa kulinda kitoweo. Paka huyu anashindwa kujizuia kumpenda msichana mmoja mwanafunzi. Hakujithibiti kama impasavyo kila mwalimu bora… (uk. 36)

Licha ya mwandishi kumlaumu yule mwanafunzi aliyedondokewa na Fao kwa “kukanyaga miiba bila viatu na kutegemea hatadungwa hata mwiba mmoja”,  inatarajiwa kuwa mwalimu ndiye anayefaa kuwa kielelezo kizuri kwa mwanafunzi wake. Kitendo cha Fao kinaonyesha namna walimu katika jamii ya Tomoko walivyopotoka kimaadili.

Tanzia nyingine inayokumba elimu katika jamii ni wanafunzi kufanyiwa mtihani na kwenda kusomea taaluma mbalimbali vyuoni. Katika uk. 36, mwandishi anadokeza kuwa Fao hakuwa zuzu darasani aliyeshindwa kuunga moja na moja kupata mbili, ila wazazi wake hawakumwamini sana kimasomo.

Mama yake aliyekuwa mwalimu wa Historia katika shule ya upili na baba yake meneja wa benki mjini Ulitima kabla ya kufanywa Waziri wa Mifugo na Wanyama walitumia nafasi zao katika jamii kumsaidia Fao kupita mtihani kwa kufanyiwa.

Hata baada ya kufanyiwa mtihani na kufaulu kwa ufanifu mkubwa, Fao anapelekwa  kusomea ughaibuni kwa msaada wa serikali uliotengewa watoto wa maskini. Kwa mujibu wa mwandishi, mambo haya yanathibitisha sifa ya Tomoko kuwa taifa la wapwekuzi wa kila kitu, hawajui kubagua cha kuiba. Ni kwa njia hii ndivyo Mtemi Nasaba Bora alivyowatoza Wanasokomoko pesa za kugharamia elimu ya mwanawe, Madhubuti, Urusi katika Chuo Kikuu cha Moscow (uk 118). Tukio hili linazua maswali chungu nzima. Je, Fao alifuzu kwenda kusomea alichoenda kusomea? Je, ataondokea kuwa mwanataaluma wa kweli au wa bandia atakayekuwa harabu kwa nchi ya Tomoko?

Mwalimu Majisifu anachangia katika kuboronga elimu nchini Tomoko. Yeye ni mwalimu wa somo la Kiswahili katika shule ya Upili ya Nasaba Bora. Alipelekwa ng’ambo kusomea ukasisi na aliporejea Tomoko, alifanya kazi kwingi kabla ya kuajiriwa kufunza katika Shule ya Nasaba Bora. Ni dhahiri shahiri kuwa Majisifu hakuwa mwalimu wa kweli kwa vile hajasomea ualimu katika chuo chochote. Fauka ya hayo, Majisifu anakosa kuhudhuria vipindi vya masomo kama impasavyo mwalimu bora. Mashaka anapomletea barua ya mwaliko kwenda Chuo Kikuu cha Mkokotoni kutoa mihadhara kuhusu uandishi wake, anamlalamikia wazi, “Hatujasoma lolote katika somo la Kiswahili karibu muhula mzima… Nasi twakutaka uje utukomboe toka  katika matatizo yetu darasani,” (uk 47)

Elimu katika eneo la Sokomoko inadumazwa na vitendo vya kijamii vyenye matokeo hasi. Mashaka anaishia kukatiza elimu yake baada ya kuachwa na mpenziwe Ben Bella. Lowella anaacha kusoma ili atumbue raha. Yeye ni mpenzi wa chaki wa Nasaba Bora. Kinaya kinatokea kuwa, inatarajiwa kuwa maadam Nasaba Bora ni kiongozi, angehakikisha kuwa Lowella ambaye afaa kuwa bintiye, anaendelea na kisomo chake, badala yake anahusiana naye kimapenzi.

Mwalimu Majisifu anamwajiri Imani, msichana mdogo anayefaa kuwa shuleni. Imani aliamua kukatiza elimu yake kutokana na uchechefu wa karo.

Licha ya mwalimu Majisifu kuchangia matatizo yanayokumba elimu katika eneo la Sokomoko, anamwambia Mashaka kuwa bara la Afrika linataka watu waliosoma sana kulikomboa toka kwenye utumwa wa ujinga, njaa na umasikini. Kauli hii inaondokea kuwa kinyume cha hali halisi riwayani pale ambapo yeye mwenyewe licha ya kusomea ng’ambo, anashindwa kudumu katika ajira mbalimbali azipatazo kutokana na utepetevu.

 

Kuiba mswada

Baya zaidi kushindwa kuhudhuria vipindi vya masomo itakikanavyo na kuiba mswada wa Amani wa Kidagaa Kimemwozea.

Mwandishi anarejelea riwaya ya Tayeb Salih ya Seasons of Migration to the North ambapo mhusika wake mkuu Mustafa Sa’eed ni msomi anayekwenda Uingereza kutoka kwao Sudan. Mustafa Sa’eed anaondokea kuwa mtaalam msomi lakini anashindwa na mtihani wa maisha. (uk 118)

Ili kutatua tatizo linalokumba elimu na kufuta machozi kutokana na tanzia iliyokumba elimu, mwandishi anapendekeza watu wajifunze elimu ya maisha pia.

Anapendekeza kuwa watu wapate elimu. Si elimu ya shahada na stashahada zipatikanazo vyuoni. Elimu ya watu kujielewa wao ni kina nani, walitoka wapi na wanaenda wapi. Elimu ijengayo wasomi wazalendo kama Madhubuti.