Mkabala wa kisintaksia katika kuainisha ngeli za nomino

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, April 18  2017 at  14:54

Kwa Mukhtasari

UAINISHAJI wa ngeli kwa kutumia mkabala au mtazamo wa kisintaksia ni mpana mno. Hii ni kwa sababu ya kuzalishwa kwa uwakilishaji wa nomino nyingi zaidi katika sarufi ya lugha.

 

Kwa kiasi kikubwa, itashuhudiwa kwamba udhaifu na upungufu mwingi uliopo katika mfumo au mtindo wa kuainisha ngeli za Kiswahili kimofolojia unaondolewa na pengo hilo kuzibika.

Katika kuainisha ngeli za nomino ama kimofolojia au kisintaksia, wanasarufi wametumia viambishi kuwakilisha nomino katika ngeli zao.

Kisintaksia, kila ngeli ina kipatanishi chake ambacho huambishwa kwenye nafasi ya kwanza ya kitenzi na (au) kivumishi wakati nomino yoyote inatumika katika nafasi ya kiima.

Mfano:

1(a) Mti mkubwa umeanguka (Umoja)

  (b) Miti mikubwa imeanguka (Wingi)

2(a) Kilichopotea ni kizuri mno (Umoja)

  (b) Vilivyopotea ni vizuri mno (Wingi)

Katika sentensi za (1), kiambishi cha ngeli ya nomino ‘mti’ katika kitenzi –meanguka ni ‘U’katika Umoja na ‘I’ katika Wingi.

Katika sentensi za (2), kiambishi cha ngeli katika kitenzi –lichopotea na –livyopotea ni ‘KI’ na ‘VI’ katika Umoja na Wingi mtawalia, kadri idhihirikavyo katika kiwakilishi cha nomino.

Vivyo hivyo, katika sentensi hizo, kiambishi cha ngeli katika kivumishi –zuri ni ‘KI’ katika Umoja na ‘VI’ katika Wingi.

Kisintaksia, ina maana kwamba ngeli ya nomino ‘mti’ ni U-I-, ilhali nomino inayowakilishwa katika sentenzi ya 2(b) imo katika ngeli ya KI-VI- kiujozi.

Hivyo, ngeli ni utaratibu wa taaluma ya kisarufi ya lugha katika kupanga aina za majina au nomino.

Kapinga (1983) anaeleza kuwa neno ‘ngeli’ limechukuliwa kutoka kwa lugha ya Kihaya (Tanzania) lenye maana ya ‘aina ya kitu’.

Kwa kutumia mantiki yatokanayo na maelezo haya, ngeli inaweza kufafanuliwa kuwa ‘kundi la nomino za aina moja’.

Ngeli zinaweza kuainishwa kwa vigezo vya kimofolojia (maumbo ya maneno), kisintaksia (upatanisho au uwiano wa kisarufi) au kisemantiki (kimaana).

Kuna wanasarufi wengi walioainisha ngeli za Kiswahili kimofolojia. Baadhi yao ni ni Krapf (1850), Steere (1875), Meinhoff (1910), Ashton (1944), Palome (1961), Loogman (1965), Guthrie (1967) na Zawawi (1979).