Mkabala wa kitaksonomia katika uainishaji wa lugha kiisimu

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Sunday, April 23   2017 at  19:22

Kwa Mukhtasari

KWA mujibu wa Massamba (2010) na (2011), akimrejelea Fudge (1973), uanishaji ni ugawaji wa kitu kivipandevipande.

 

Kwa mantiki hiyo basi, Fonolojia Ainishi ni ile ambayo inajishughulisha na uainishaji wa sauti kwa kuzingatia sifa zake bainifu.

Nadharia hii ya Fonolojia Ainishi iliasisiwa na wanazuoni, Nicholas Trubetzkoy, Edward Sapir na Leonard Bloomfield. Walifanya kazi ambazo zilifungua ukurasa mpya katika uchanganuzi wa lugha kiisimu.

Wataalamu hawa walichochea wanafonolojia wengi kujishughulisha zaidi na masuala yaliyokuwa yanahusu uchanganuzi wa kifonimu.

Wanazuoni kama vile Bloch, Hockett, Harris na Chao walitumia muda wao mrefu wakijaribu kuzielewa taratibu na njia za kuchunguza na kufanya majaribio kuhusu mifumo mbalimbali ya lugha. 

Wengi wa wasomi hawa wa Isimu walifuata nyayo za watangulizi wao ingawa walitofautiana kwa kiasi kikubwa katika baadhi ya masuala kuhusu uchunguzi wa lugha kisayansi.

 

MISINGI

Wataamu hawa walijaribu walivyoweza ili kuonyesha jinsi uwakilishi wa kiwango cha kifonimiki (kifonolojia) na ule wa kiwango cha kifonetiki ungeweza kufanywa.

Walitafuta njia ambazo kama zingefuatwa barabara, zingewawezesha kuubaini mfumo wa kifonimu wa lugha yoyote ile pasi na kuingiza hisia, maoni au fikra za mchanganuzi anayehusika.

 Ili kuonyesha wazi tofauti zilizopo kati ya kile walichokiita uwakilishi wa kifonimiki na uwakilishi wa kifonetiki, wanamuundo walionelea kuwa ilikuwa vyema:

(a) Kueleza wazi maana waliyokuwa nayo walipotumia istilahi za fonimu na foni. 

Kwa hivyo wanamuundo hawa walizingatia zaidi kanuni zilizotakikana katika kuhusisha taarifa za kifonimiki na zile za kifonetiki. Ili kufikia kiwango hiki, walilazimika kuingiza masuala ya kisarufi.

Walilazimika pia kubadilisha utaratibu wao kidogo: waanze kwa kiwango cha kifonetiki na kwenda hatua kwa hatua hadi kwenye kiwango cha kisarufi.

(b) Katika ufafanuzi wa kimuundo, uchanganuzi makini na wa hatua kwa hatua wa data za kiisimu lilikuwa jambo muhimu sana. Utaratibu ukawa ule wa ugawanyaji maumbo kivipandevipande na kuyaainisha kwa kuanza na data za mfumo wa lugha husika. 

Kwa hivyo, wanamuundo hawa wakauita mkabala huu wa uainishaji wa kiisimu, mkabala wa kitaksonomia, kwa sababu ulikuwa mwelekeo ambao ulifuata mbinu za kitaksonomia.

 MIKABALA YA UANISHAJI

a)  Kuvibainisha vipandesauti katika lugha fulani; yaani fonimu na alofoni zake.

b)  Kutumia sifa bainifu kuzifafanua na kuzitofautisha fonimu na alofoni hizo.

Kwa mujibu wa David E. Massamba katika kitabu chake Misingi ya Fonolojia (2006), uchanganuzi wa kitaksonomia ni uchanganuzi ambao hufuata mkabala wa ufafanuzi wa masuala ya lugha unaozingatia kanuni na taratibu za uainishaji yaani uwekaji katika makundi mbalimbali yenye sifa zinazofanana na ufafanuzi wa vitu, maumbo au vipengele vyovyote vile. 

Kwa hivyo, wanamuundo walijikita katika utaratibu wa uainishaji uliokuwa umekitwa katika ugawanyaji wa maumbo kivipandevipande. Yaani, kuchagua neno moja na kuligawanya kivipandevipande kwa kuzingatia muundo wa kifonolojia au kimofolojia.

Kwa mfano maneno:   Mtu →  {m}+{tu}

                                    Upendo → {u}+{pend}+{o}

Maneno haya mawili yamepambanuliwa kwa kuzingatia maumbo ya kimofimu. 

Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa uainishaji huu haukufanywa tu kiholela ila ulifanywa kwa kuzingatia utaratibu wa kimofimu. Wanamuundo waliishia katika kuligawa neno tu. 

Hata hivyo, kama itakavyobainika baadaye, wanafonolojia zalishi walitoa sababu ilipoonekana kuwa lazima kufafanua hali fulani.

Hivyo, maneno yaya haya kifonolojia yanaweza kuainishwa kama ifuatavyo:

Mtu  → /m/+ /t/ + /u/ yaani lina fonimu tatu

Upendo  → /u/ + /p/ + /e/ + /nd/ + /o/  yaani lina fonimu tano.