Mtindo katika lugha ya mawasiliano ya wanajamii

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, April 18  2017 at  15:00

Kwa Mukhtasari

LUGHA imeweza kutumiwa kuleta mabadiliko na huwa na athari chanya na hasi katika jamii kutegemea na watumizi lugha, yaani msemaji na msemewa.

 

Katika athari chanya, lugha yaweza kutumiwa kuwaunganisha watu na pia kukomesha uhasama. Hata hivyo, lugha yaweza kuwa na athari hasi hasa ikiwa itatumiwa kuleta uhasama au kusababisha utengano baina ya mtu na mtu, jamii na jamii nyingine au hatamakundi ya kijamii.

Lugha huweza kuathiri mtazamo na tabia ya mtu. Yote hutegemea namna lugha inatumiwa ili kuleta athari inayokusudiwa.

Watu hutambua kikundi chao cha kijamii kutegemea misimbo au aina ya lugha wanayotumia.

Matumizi ya lugha kwa njia fulani ndio huwafungamanisha watu wa kikundi fulani pamoja na kuwatambulisha. Lugha ya maafisa wa polisi kwa mmfano, huweza pia kubainishwa na kutumiwa kuwatambulisha.

Maafisa wa polisi ndio kiungo muhimu katika kulinda na kudumisha usalama wa nchi. Kutokana na uhalisi wa kazi yao, maafisa wa polisi huhusiana na watu wa matabaka mbalimbali na walio na vyeo tofautitofauti katika nyanja mbalimbali.

Katika kutekeleza majukumu yao, maafisa wa polisi hutumia lugha kuwasiliana na ‘wateja’ wao.
Maafisa wa polisi hutumia lugha kwa namna inayowatambulisha wao kama kikundi maalumu ambacho kinaweza kutambuliwa kutokana na sajili yao.

Kikundi hiki cha maafisa wa polisi kinaweza kutambuliwa na watu wengine kutokana na lugha wanayoitumia.

Kama wasemavyo Linda na Wareing,(1999: 143), kikundi fulani hutambuliwa kama kikundi cha kijamii na watu wengine kutokana na matumizi yao ya lugha na tabia nyingine za kiisimu kama vile katika
kutunga sentensi zao. Haya ndio mambo ambayo huwaongoza wanajamii wengine kukitambua kikundi cha kijamii.

Matumizi ya lugha ya maafisa wa polisi ni ya kipekee na hii huwatofautisha na makundi mengine.
Lugha ni chombo muhimu cha mawasiliano katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali. Kikundi chochote kile huwa na namna yao ya pekee ya kutumia lugha na hii hutofautisha kikundi na
kingine.

Habwe na wengine (2010: 71) wanasema kuwa “…………ili kukidhi haja ya mawasiliano, makundi ya kijamii huibua mitindo na istilahi zao zinazowawezesha kurejelea shughuli za kundi husika.”

Hii inaashiria kuwa kila kikundi katika nyanja mbalimbali huwa na mtindo wake wa kutumia lugha kwa namna ambayo itawawezesha kuafikia malengo yao ya kazi.

Maafisa wa polisi kama kikundi cha kijamii pia huwa na mitindo na istilahi zao ambazo huwawezesha kutekeleza majukumu yao.

 
Kwa mujibu wa Fishman (1968: 3) jamii ni ya muhimu kuliko lugha na kwa hivyo anasema kuwa jamii ndio hutuwezesha kupata muktadha ambao unaweza kutusaidia katika kutazama aina ya lugha inayotumiwa.

Kama asemavyo Bernstein (1971: 61), tofauti za kiisimu za matumizi ya lugha ya kikundi fulani hutokea katika mazingira halisi ya kijamii na
vyeo vya makundi mbalimbali huweza kubainishwa na usemi wao. Ni rahisi kuchunguza sajili ya maafisa wa polisi wanapokuwa katika kituo cha polisi kwa kuwa hayo ndio mazingira yanayowatambulisha na ndio muktadha wao halisi.

Fishman (1968: 139) akimnukuu Halliday: uchunguzi wa muktadha wa mazungumzo hutuelekeza katika uchanganuzi wa hali na matumizi ya lugha.

Pride (1971: 25) anasema kuwa, mawanda ya matumizi ya lugha huelezwa kama hali ambapo matumizi ya aina fulani ya lugha hutumiwa na kikundi mahsusi na hii husaidia katika utambulisho wa kikundi hicho cha kiisimu na kwa njia ya kijamii.

Hii inaashiria kuwa kikundi fulani cha watu huweza kuainishwa kijamii na kiisimu.

Naye Hirst (1986) anasema kuwa namna watu hutumia lugha husababishwa na mambo mawili: wao kama watu binafsi au wao kama wanajamii.

Hii ina maana kuwa, lugha wanayotumia katika mazungumzo huchangia katika kujitambua na pia lugha yao ni chombo cha kudhihirisha kikundi hicho husika’(TY).

Kutokana na maelezo ya wataalamu hawa, ni wazi kuwa kila kikundi katika nyanja mbalimbali huwa na namna yao ya kuwasiliana. Hii huwatambulisha watu wa kikundi hicho.

Muundo wa kitabaka huathiri elimu na kazi za watu na kisha kuwapa wanajamii husika mahusiano fulani ambayo hutambulisha tabaka lao ambalo huwa tofauti na matabaka mengine.

Wanajamii katika kikundi fulani hutumia lugha kwa njia ya kipekee
wanapoingiliana ili kutambuliwa katika kikundi hicho. Hii inadhihirisha kwamba unaweza kuzungumza kama wanakikundi hicho na hivyo kuwa mwanakikundi.

Nchini Kenya kwa mfano, kuna chukulizi kuwa lugha ya maafisa wa polisi husheheni kuchanganya ndimi, sauti yao hudhihirisha mamlaka, wana misimbo yao ambayo huitumia katika mawasiliano.

Msimbo ni sehemu ya lugha na ni utaratibu wa kutoa mawasiliano (Iribemwangi na Mukhwana, 2011: 45). Wanaendelea kusema kuwa: Kwenye msimbo finyu, wazungumzaji huweza kutumia ujuzi na tajriba zao za pamoja na uelewa wa pamoja kusemea kile wanachotaka kuongea au kusema. Aina hii ya msimbo huunda upamoja ambao hufanya watu wanaotumia lugha kuhisi kuwa ni wa kundi fulani moja.

Kama mkakati wa mawasiliano, maafisa wa polisi kwa mfano hutumia msimbo finyu kama njia ya kuonyesha umoja na kutenga makundi mengine hasa wanapozungumzia masuala yanayohusu usalama wa nchi.

Pia hutumia msimbo pana wanapowasiliana na wateja wao. Kwa mfano, msimbo hutumika sana pale wanapozungumza kwa kutumia redio zao za mkononi.