Mwanamume si ndevu

Wachumba

Wachumba wakiwa wamejawa na furaha. Picha/HISANI 

Na Iddi Ninga wa Tengeru

Imepakiwa - Tuesday, November 29  2016 at  12:56

Kwa Mukhtasari

Moja ni uvumilivu na kutokata tamaa,

Ili mbele kula mbivu, na kuacha kuzubaa,

Kujilinda na uvivu, na kuiaha zinaa,

Uanaume si ndevu, ni matendo na tabia.

 

Mbili wala si mchoyo, kwa kile alichopata,

Hata kama kiboyo, hushinda akitafuta,

Siyo mpinga mboyoyo, na mkiya akifyata

Uanaume si ndevu, ni matendo na tabia.

 

Tatu mwingi wa upole, tena aliye jasiri,

Asopiga makelele, alojawa na usiri,

Daima msonga mbele, kikammanda jemedari,

Uanaume si ndevu, ni matendo na tabia.

 

Siyo mkurupukaji, japokuwa hutokea,

Hajifanyi mjuaji, kwa kile asolijua,

Tena yeye mkanyaji, baya akishuhudia ,

Uanaume si ndevu, ni matendo na tabia.

 

Basi kuwa mchamungu, usipate sifa hizi,

Tafuta chini uvungu, mwanaume siyo mwizi,

Wa kale tangu na tangu, katika hiki kizazi,

Uanaume si ndevu, ni matendo na tabia.

Na Iddi Ninga wa Tengeru