http://www.swahilihub.com/image/view/-/4890032/medRes/2194553/-/xcsjbwz/-/maria.jpg

 

Nadharia kama mwongozo wa uhakiki

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, January 22  2019 at  11:50

Kwa Muhtasari

  • Kwa mujibu wa Wamitila (2003), nadharia ni istilahi inayotumiwa kurejelea kauli au kaida za kijumla zinazotegemezwa kwenye uwazaji fulani

  • Katika kitengo cha uhakiki, nadharia inaweza kuchukuliwa kama mwongozo wa kumsaidia msomaji kufahamu kazi ya sanaa vyema zaidi

 

KATIKA fasiri ya nadharia kwa kutumia mtazamo wa hali ya umoja na wingi, wataalam husika walichukulia nadharia kuwa moja tu.

Dhamira yao ilikuwa kutafuta msimbo wa kibia wa kuchanganulia fasihi. Isitoshe, kwao kazi za sanaa ni minara inayosifika kwa vile imehifadhiwa kimaandishi.

Hata hivyo, fasihi simulizi haikuwa moja kati ya taaluma mashuhuri katika mitaala yao.

Hii ni kwa sababu ilkichukuliwa kama itikadi ya kukiritimba uainisho na usomaji wa fasihi.

Ndiyo sababu wataalamu waliokulia kwa ziwa la Wellek na Warren walipoanza kutembea hasa barani fasihi za kienyeji hazikuwashugulisha asilani ijapokuwa zilikuwa zimeimarika vya kutosha katika vyuo vikuu vya Kimagharibi.

Nadharia za uhakiki ni kama njia nyingi teule za kuzungumzia ujuzi wa kifasihi, zimo mashindanoni na zinazoshinda kidesturi ndizo huhesabiwa kuwa teule zaidi kadamnasi ya nyinginezo.

Nadharia zinazoshinda kwa kurejelewa mara kwa mara na kutumiwa si lazima ziwe sahihi na kuhudumia wanajamii wote kwa mafanikio.

Hivyo basi kwa sasa nadharia ni nyingi na hutumika kutegemea mahitaji mbalimbali  na vikundi anuai vya wanajamii.

Nadharia kama mwongozo wa kuhakiki

Katika kitengo hiki, nadharia inaweza kuchukuliwa kama mwongozo wa kumsaidia msomaji kufahamu kazi ya sanaa vyema zaidi.

Nadharia ni mkataba usiokuwa rasmi kati ya msomaji na mtunzi. Mhakiki kama msomaji anapoyaweka mawazo ya mtunzi katika utaratibu mahsusi ili yaweze kutathminika pasi kuweka masharti maalum, basi nadharia yake itakuwa kama mwongozo.

Kwa mfano katika ushairi wa Kiswahili, wahariri na wahakiki mathalani Shihabuddin Chiraghdin na Abdilatif Abdalla wanazungumzia vitanzu vya mashairi kimaudhui bila kuonyesha mipaka yake mahsusi. Idadi ya vitanzu inategemea masuala yanayoendelea kuibuka.

Katika utangulizi wake wa Malenga wa Mvita (1970), tungo zilizosanifiwa na Juma Bhalo, Chiraghdin hazungumzii muundo wa ushairi.

Suala la muundo ni kaida na halimshughulishi asilani.

Alipouandika utangulizi wake, muundo tengemano wa shairi kama alivyofahamu hakukuwa umeshurutishwa wala kuvurugwa na yeyote.

Alilirejelea tu pale alipowajibika kuwaonya na pengine kuwaelekeza washairi chipukizi wa kizazi kipya.

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo:

Wamitila, W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus.

Wa Thiong'o, Ngugi (1998). Penpoints Gunpoints and Dreams. Oxford: Clarendon.

Wellek Rene & Austin Warren ( 1986). Theory of Literature. Harmondworth: Penguin.

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com