Namkumbuka Mwalimu

Na Ignas Joachimu Komba

Imepakiwa - Monday, October 24  2016 at  14:42

Kwa Mukhtasari

Leo siku imetimu, kumkumbuka Mwalimu,

Naifahamisha kaumu, hili tukio muhimu,

 

Leo siku imetimu, kumkumbuka Mwalimu,

Naifahamisha kaumu, hili tukio muhimu,

Ili wapate fahamu, na mafunzo ya kudumu,

Leo imenilazimu, kumkumbuka Mwalimu.

 

Hakupeda kudhulumu, na katu si mhujumu,

Alikuwa mtaalamu, tena wetu mhudumu,

Leo imenilazimu kumkumbuka Mwalimu.

 

Apendaye ukarimu, mgeni humkirimu,

Fikira zake zidumu, huyu mtu muhimu,

Usiawe na udumu, kwa ajili ya kaumu,

Leo imenilazimu, kumkumbuka Mwalimu.

 

Ninamwomba rahimu, aisaidie kaumu,

Kutimiza majukumu, tuzungushe gurudumu

Maisha tuyaataimu, upendo kwetu udumu,

Leo imenilazimu, kumkumbuka Mwalimu  

 

 

Tusijepata waazimukutotaka ya Mwalimu

Na nchi kuihujumu, tukose wa kulaumu,

Wajanja kututaimu, tukibaki humuhumu,

Leo imenillazimu, kumkumbuka Mwalimu.

 

Alituasa Mwalimu, sharia kuziheshimu,

Ili kweli tudumu, tusipatwe na hukumu,

Na daima tufahamu, ya halali na haramu.

Leo imenilazimu, kumkumbuka Mwalimu

 

Mjamaa mfahamu,Juliasi etu mwalimu,

Udini sio mtamu,  aliona ni haramu,

Hazikuwa zake mbinu, kuigawanya kaumu,

Leo imenilazimu, kumkumbuka Mwalimu.

 

Alimpisha kwa zamu, na Mwinyi alimkarimu,

Tukapata na nujumu, toka kwake Rahimu,

Twangara kama ruhamu, toka Hindi mpaka shamu,

Leo imenilazimu, kumkumbuka Mwalimu.

 

Upeowe kama mlizamu,mwenye wingi ufahamu,

Alikuwa maalumu na wala sintofahamu,

Kwa yale asiyotimu, kwani yeye binadamu,

Leo imenillazimu, kumkumbuka Mwallimu.

 

Kwa lgha ilo nudhumu, shaiiri nalihitimu,

Leo sina mengi humu, nalaga na kaumu,

Namuomba na rahimu, amrehemu Mwlimu,

Leo imenilazimu, kumkumbuka Mwalimu.