Profesa Mukandala ameonyesha mfano bora, aigwe

Profesa Rwekaza S. Mukandala

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza S. Mukandala akihutubu awali. Picha/ HISANI 

Na ERASTO DUWE

Imepakiwa - Tuesday, April 25   2017 at  12:27

Kwa Mukhtasari

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala amekuwa akionyesha uzalendo mkubwa  katika kuienzi lugha ya Kiswahili. Daima ameonyesha juhudi za kuwa mstari wa mbele kuhakikisha Kiswahili kinastawi.

 

Miongoni mwa mambo ambayo ni dhahiri ni kuifanya lugha hiyo kuwa lugha rasmi katika mawasiliano chuoni hapo kwa kuipa nafasi kutumika katika vikao mbalimbali vya utawala.

Taasisi nyingi zimekuwa zikibeza lugha ya Kiswahili na hata wasomi wamekuwa wakipiga vita kwa kuiona kuwa haina  uwezo wa kutumika katika majukumu mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Dhana hiyo inapingana na hali halisi ilivyo. Ndiyo maana Profesa Mukandala kwa kutambua dhima na hadhi ya Kiswahili  kitaifa na kimataifa amekuwa mstari wa mbele kuonyesha kwamba Kiswahili kinaweza na hivyo kukiruhsu kitumike kubeba majukumu mazito ambayo wasomi wengine katika baadhi ya taasisi  hususan za elimu kukiona hakiwezi.

Fikra za baadhi ya wasomi zimeathiriwa na kasumba kuona  kuwa kama hujui lugha ya kigeni wewe si msomi  wala mwanataaluma. Suala hili linapingwa vikali na baadhi ya wasomi wanaotambua nafasi ya tamaduni zetu.

Kwa mfano Profesa Ngugi wa Thiongo kutoka nchini Kenya ni miongoni mwa masomi hao wanaothamini utamaduni wa watu. Anabainisha kwamba hatuna budi kuvienzi vilivyo vyetu.

Katika kitabu chake cha ‘Shetani Msalabani’ anasema, “Mcheza kwao haachi kutunzwa. Tusipozistawisha lugha zetu sisi wenyewe ni mgeni gani atakayejitokeza  kuja kuzistawisha?”

Swali hili la Profesa Thiongo linatoa changamoto kubwa kwetu  husuasn kwa watumiaji wa Kiswahili. Profesa Mukandala kwa uzalendo wake anajiona anawiwa kukiendeleza Kiswahili hivyo anachukua hatua za kukistawisha.

Wakati akitunukiwa tuzo ya Kiswahili iliyoandaliwa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ( TATAKI )  mwishoni mwa mwaka jana, Balozi wa Heshima wa Kiswahili Mama Salma Kikwete alionyesha utayari wake wa kuridhia baadhi ya kozi zinazofundishwa kwa Kiingereza kufundishwa kwa Kiswahili chuoni hapo.

Ufundishaji wa Kiswahili katika shule za Sekondari na elimu ya juu ni suala ambali liko katika mjadala kwa siku nyingina uamuzi wake umekuwa ukisuasua. Profesa Mukandala anatambua kuwa hakuna uhusiano kati ya lugha ya kufundishia na elimu au maarifa.

Maarifa huweza kutolewa  kwa lugha yoyote ambayo anayefundishwa anaifahamu vyema. Wataalamu wa masuala ya elimu wanasisitiza kwamba lugha bora ya kutolea maarifa ni ile apewayo anayeifahamu barabara na aghalabu huwa ni ya kwanza kwa mtumiaji wa lugha hiyo.

Profesa Mukandala alipofuatwa miaka minne iliyopita na mwanafunzi wa uzamili wa somo la Kiswahili alitakiwa kuwasiliana kwa Kiingereza.   

Alishangaa tasnifu hiyo kuwasilishwa kwa Kiingereza  na hivyo kumruhusu kuiwasilisha kwa Kiswahili

Wasomi na viongozi wengi hupigania lugha zao kuenziwa katika nyanja mbalimbali. Mchango na uzalenndo wa Profesa Mukandala katika kukiendeleza Kiswahili hauna budi kuigwa na wasomi wengine kulingana na nafasi na nyadhifa zao.