Riziki ni majaliwa, kuipata si ngekewa

Na Dotto Rangimoto Chamchua

Imepakiwa - Tuesday, November 29  2016 at  12:46

Kwa Mukhtasari

Hakumuumba kilema, akamkosesha mwendo,

Huyo ni Mola Karima, mfalme wa vishindo,

 

Sijitie uyatima fungua yako mafundo,

Rauka ufanye hima, nyumbani haliji windo.

 

Riziki ni majaliwa, kuipata si ngekewa,

Mwenye kupewa ukwasi, katu hakupendelewa,

Fukara ondoa wasi, sababu hukuonewa,

Mitihani ya Qudusi, Mola wa majaliwa.

 

Alichopewa pungusi, perege hakupatiwa,

Riziki ni majaliwa  kuipata si ngekewa,

Raula wahi kazini, upate yako ijara,

Changamoto za windoni, na zikufanye imara.

 

Toa simanzi moyoni, tena sifanye harara,

Bosi avimbe kuchwani, tuli sipoteze dira,

Riziki ni majaliwa,  kuipata si ngekewa,

Subiri mja subiri, hebu wacha kusonona.

 

Mzoee mwajiri, mambo yapate kufana,

Usimletee shari, japo  dhiki waiona,

Kuritadi sifikiri, lisilo mwisho hakuna,

Riziki ni majaliwa, kupata ni majaliwa.

 

Niseme na waajiri, wakosefu wa Imani,

Wenye kufanya kiburi, hadharani bila soni,

Mbaya hawatafakari, shida hana maskani,

Tabu haina tajiri, wala si ya maskini.

 

Riziki ni majaliwa, kuipata si ngekewa.

Hii shida mwajiriwa, shughuli zataka moyo,

Jukumu ulilopewa, litimize pasi choyo.

Ridhika unachopewa, sidhulumu nafsiyo.

 

Siseme hujausiwa, shika wangu mgogoyo,

Riziki ni majaliwa, kuipata si ngekewa,

Wote wategemeana, mwajiri na mwajiriwa,

Riziki ni majaliwa, kuipata si ngekewa.