TANZANIA YA FURAHA

Na  Shaaban Maulidi 0718526159/ 0763902318

Imepakiwa - Monday, March 4  2019 at  15:27

 

Nabakia Tanzania, siondoki Tanzania,
Nitaishi Tanzania, na kukua Tanzania,
Nitajenga Tanzania, na kuoa Tanzania,
Tanzania nchi bora, busitani ya furaha.

Kuna nini Tanzania, hadi nikuchukie, 
Ulaya kufikiria, Marekani kimbilie,
Kutaka kwenda India, nini nikakigundue?
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha amani.

Tulivu hali ya hewa, miti ya kila aina,
kuna mito na maziwa, samaki kila aina,
Bahari tumeletewa, ile ya Indiana,
Tanzania nchi bora, busitani ya furaha.

Tanzania ya neema, tunacho chakula tele,
Unga dona na mtama, mahindi hata uwele,
Tunda tamu la kuchuma, alizeti na mchele,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha amani.

Tumepewa wengi kuku, wa mayai na wa nyama,
Mbuzi ng'ombe wapo huku, kula nyama za kuchoma,
Kwa maziwa si kapuku, kwa hakika ninasema,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha furaha.

Watu wake watu wema, wapole na wakarimu,
Walojawa na huruma, roho za kibinadamu,
Tena wanayo heshima, ya kauli na salamu,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha amani.

Mlima wa Kilimanjaro, ni ishara ya upendo,
Hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti ni uhondo,
Aridhi ya Morogoro, na mbozi kuna kimondo,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha furaha.

Ziwa refu Tanganyika, ziwa kubwa lipo Mwanza,
Fukwe zilizopangika, bahari hindi ya kwanza,
Migodi iliyotajirika, ya Mwadui na Uvinza,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha amani.

Tembo na pundamilia, simba, twiga na viboko,
Mito ya kuogelea, gesi na maporomoko,
Ndege wa kila jamia, huruka huku na huko,
Tanzania nchi bora, ni kisiwa cha furaha.

Karibuni Tanzania, busitani ya Edeni,
Mbuga zake tembelea, maajabu tazameni,
Tabora Mbeya Songea, Zanzibar kisiwani,
Tanzania nchi bora, busitani ya amani.