Tanzania ya viwanda mtaji kwa Kiswahili

Na ERASTO DUWE

Imepakiwa - Tuesday, May 1  2018 at  15:27

Kwa Muhtasari

Lugha ya Kiswahili kama nyenzo kuu ya mawasiliano nchini Tanzania, ndiyo itakayorahisisha na kuwezesha mawasiliano mbalimbali kufanyika katika Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.

 

MIKAKATI ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, inakipa Kiswahili fursa ya pekee.

Halkadhalika, suala hilo ni mtaji pia kwa Waswahili waliotaalamikia Kiswahili na taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na maendeleo ya Kiswahili.

Hii ni kwa sababu uwekezaji unaofanyika na utakaoendelea kufanyika katika viwanda, unaenda sambamba na mawasiliano.

Lugha ya Kiswahili kama nyenzo kuu ya mawasiliano nchini Tanzania, ndiyo itakayorahisisha na kuwezesha mawasiliano mbalimbali kufanyika katika Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati. Ikiwa uwekezaji huo unafanywa na Serikali yenyewe, wawekezaji wazawa nchini au wawekezaji wa kutoka nchi za kigeni, matumizi ya Kiswahili hayawezi kuepukika.

Mathalani, wawekezaji wa kigeni watahitaji kukijua Kiswahili ili kuweza kufanikisha mawasiliano yao kiutendaji. Watahitaji kuwasiliana na wafanyakazi wengine ambao pasi na shaka baadhi yao ni watumiaji wa Kiswahili.

Ukiachana na wawekezaji, wafanyakazi wengine wa kigeni wasiokijua Kiswahili watahitaji kukijua Kiswahili ili kuweza kuyamudu mazingira ya kazi zao kama vile kukidhi haja ya mawasiliano na wafanyakazi na watu wengine wanaowazunguka.

Aidha, kwa kuwa mazingira ya uzalishaji ni ya Watanzania ambao kwa kiasi kikubwa ni Waswahili, wateja wa bidhaa zitakazouzwa ndani ya nchi ni Waswahili hao ambao ni watumiaji wa Kiswahili.

Kutokana na umuhimu wa mawasiliano katika biashara, hapana budi upande wa uzalishaji kukijua vizuri Kiswahili. Dhana ya uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda ambayo Serikali imedhamiria kuitekeleza, inaweza tu kuelezwa na kufikishwa vizuri kwa Watanzania wote kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Hii ni kwa sababu Kiswahili kwa Watanzania wengi ni lugha yao ya pili na kwa kiasi fulani ni lugha yao ya kwanza. Kiswahili kinaeleweka vizuri zaidi kwa Watanzania wote. Kwa sababu hiyo, Watanzania wengi wanaweza kulibeba bango la uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda akilini mwao kwa Kiswahili kuliko wanavyoweza kufanya hivyo kwa lugha ya kigeni.

Mashine

Vilevile, dhana ya viwanda inaendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Wapo Watanzania wavumbuzi ambao kwa vipawa vya kuzaliwa au ujuzi walionao wamevumbua mashine ambazo zinaweza kutumika katika uzalishaji.

Watu hao kwa kiasi kikubwa ni Watanzania ambao wengi wao hawazijui lugha za kigeni. Kwa hivyo, hao wanaweza kuueleza vizuri ubunifu wao na kufafanua utendaji kazi wa mashine walizovumbua kwa kutumia lugha yao ya uvumbuzi ambayo ni Kiswahili.

Pia, kama ilivyo kwa viwanda vinavyopatikana katika sehemu nyingine duniani, vifungashio vya bidhaa ni bendera kubwa ya upeperushaji wa lugha yoyote iwayo duniani. Hatuna mashaka kwamba, viwanda vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali nchini Tanzania hata kama ni vya wawekezaji wa kigeni, miongoni mwa lugha zitakazotumika katika vifungashio mojawapo ni lugha adhimu ya Kiswahili. Kwa kufanya hivyo, Kiswahili kitapeperushwa kokote duniani bidhaa hizo zitakakopelekwa.

Kutokana na umuhimu huo wa Kiswahili, ipo haja kubwa ya jamii ya Waswahili kuandaa mazingira yatakayorahisisha mawasiliano kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Kwa mfano, taasisi zenye mamlaka zinapaswa kuandaa kozi na machapisho ya Kiswahili kwa wageni yanayohusiana na biashara, viwanda, uchumi na uzalishaji.