UJANA

Na SHAABAN ROBERT

Imepakiwa - Monday, July 25  2016 at  17:21

Kwa Muhtasari

Ujana kitu kitamu, tena ni azizi sana,

Maungoni mwangu humu, nilikuwa nao jana,

 

UJANA

Ujana kitu kitamu, tena ni azizi sana,

Maungoni mwangu humu, nilikuwa nao jana,

Kwa wingi katika damu, tahamaki leo sina,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kichwa kimejaa mvi, kinywani meno hamna,

Nikienda kama mlevi, miguu nguvu hamna,

Kama zilizofikichwa, zikang’olewa mashina,

Kumbe ujana ni hivi, rafiki yangu ujana.

Jina langu limekuchwa, na nyota zilizoona,

Ukinitazama kichwa, nywele nyeusi hakina,

Kama zilizofikichwa, ziking’olewa mashina,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Natatizika kauli, midomoni najitafuna,

Nimekusanya adili, walakini hali sina,

Dunia kitu batili, hiki una kile huna,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Nilikuwa ni waridi, furaha, furaha ya wasichana,

Neno hawakunirudi, wakati wa kukutana,

Sasa nanuka baridi, wanionapo waguna,

Nasikitika hadumu, rafiki wengi sana.

Walio wakinihusu, walikuwa wengi sana,

Wanawake wenye busu, uzuri na usichana,

Leo sina hata nusu, ya wanitajao jina,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Wazuri wenye uturi, na mikono yenye ina,

Kila mtu mashuhuri, alipenda kuniona,

Nilifaa kwa shauri, na sasa kauli sina,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Dunia bibi harusi, kwa watu kila namna,

Inapendeza nafsi, wa kati wa kuniona,

Na leo sina nafasi, kwa uzee kunibana,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kilichokuwa gizani, niliwaza kukiona,

Nikakijua thamani, sura yake hata jina,

Leo natazama hasara, hata ikiwa mchana,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kilichotaka fikra, niliweza kukinena,

Kwa mfano na kwa sura, mpaka kikafana,

Leo tazama hasara, nguvu hiyo sina tena,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Hauna dawa uzee, mabega yamepetana,

Anionaye ni wee, ondoka hapa laana,

Wanasema na miye, niliyekuwa na jina,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kaditama nafikiri, uchungu wanitafuna,

Walakini nafikiri, twafuata Subhana,

Katika ile amri, ya kuwa na kutengana,

Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.