Uambishaji katika vitenzi vya Kiswahili

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, April 18  2017 at  14:31

Kwa Mukhtasari

KATIKA uzoefu wangu wa kufundisha Kiswahili, hakuna wakati darasa linapochangamka zaidi kama wakati wa mada ya Uambishaji, na mahsusi kuhusu vitenzi.

 

Kuambisha ina maana ya kuweka viambishi kwenye mzizi wa neno ili kutoa maana inayokusudiwa. 

Uambishaji ni dhana inayowakilisha upachikaji wa vipashio vya kisarufi kwenye mzizi wa neno kwa minajili ya kujenga ama neno jipya au kubadilisha tu hali ya neno.

Kuna viambishi awali na tamati, kwa mujibu wa wapi kinatokea kwenye huo mzizi wa neno. Kwa mfano, mzizi wa neno -pig- ukiwekewa viambishi ku-pig-a unakuwa kitenzi au kitenzi nomino na ukiwekewa pig-o unakuwa nomino. Inaweza kuwa u-pig-aji, ma-pig-ano, m-pig-aji na kadhalika. 

Kiambishi huweza kubadilisha kitenzi kuwa nomino, nomino kuwa kivumishi, kitenzi kuwa kielezi na, juu ya yote, uambishaji katika Kiswahili hukifanya kitenzi kimoja kuwa sentensi nzima yenye sehemu zote kuu nne – mtenda, kitendo, mtendwa au mtendewa na hali ya utendaji.

Ukiacha Kiarabu, lugha ambayo inaruhusu kiwango fulani cha uambishaji kwenye kitenzi, ni Kiswahili ninachokiona kinaongoza.

Nakubali kusahihishwa ikiwa nimekosea. Hata hivyo, hebu angalia mfano huu na neno moja tu “Nimemuona” ambalo kama lingetafsiriwa kwa Kiingereza, yangekuwa maneno manne:

Kiingereza: “I have seen him/her.”
Ndani ya neno moja la Kiswahili, mna kila kitu kinacholifanya kuwa sentensi kamili:
NI - inawakilisha kiambishi cha nafsi ya kwanza umoja – mimi, mtenda
ME - inawakilisha kiambishi cha hali timilifu ya wakati uliopita
MU - inawakilisha kiambishi cha nafsi ya tatu umoja – yeye, mtendwa
ON - inawakilisha mzizi wa kitenzi – kuona
A - inawakilisha kiambishi cha hali ya kitendo – utendaji

Sentensi nzima imesemwa kwa neno moja tu na maana kamili ikawasilishwa.

Hoja hapa si kwamba Kiswahili pekee ndicho chenye urejeshi, lakini ni kwamba dhana hii ni pana sana katika lugha hii kuliko katika lugha nyingine.

Viambishi na vipashio vya Kiswahili vinavyotumiwa kuwakilisha urejeshi ni vingi na vinapatikana katika mazingira mbalimbali.

Swali la kwanza kulijibu ni maana ya urejeshi kama dhana katika muundo wa lugha. Dhana hii inawakilisha viambishi au vipashio vya maneno yanayorejelea nomino, viwakilishi au vivumishi katika maneno.

Katika sentensi hii, kwa mfano, “Ni yeye mwenyewe ndiye mwenye matatizo, si mimi,” maneno “mwenyewe”, “ndiye” na “mwenye” yote ni virejeshi.

Kwa Kiingereza, sentensi hii ingesomeka: 
“It is he/ she himself/ herself who has got problems, not me.” (Pengine tafsiri hii si sahihi kuelezea dhana kamili kwa lugha ya Kiingereza). 

Na hapa ndipo ninapohoji upekee wa Kiswahili. Kwamba urejeshi wake ni mpana sana. Katika mfano huu, maneno “mwenyewe”, “ndiye” na “mwenye” yanarejea kiwakilishi yeye, ambacho nacho ki katika nafsi ya tatu umoja, inayoweza kuwa kwa mfano Zubeda au Rashid.

Zingatia jambo moja muhimu sana hapa: kwamba maneno yote matatu yanazingatia kile kinachoitwa “upatanisho wa kisarufi”, yaani utawala wa nomino (kiwakilishi) dhidi ya aina nyingine za maneno katika sentensi.

Dhana hii ya upatanishi wa kisarufi inashurutisha kuwepo kwa uwiano kwa aina ya kundi la nomino na maneno mengine yanayohusu nomino hiyo, viwakilishi vyake, vivumishi vyake na hata vitenzi.

Katika mfano wa hapo juu, maneno hayo yanawiana kama hivi: “YEYE” ni kiwakilishi nafsi ya tatu umoja kinachotokana na kundi la nomino YU-A-WA.

Anaweza kuwa mtu, mnyama au ndege. Katika mfano wetu, bila shaka amekusudiwa mtu, anayeweza kuwa mwanamke au mwanamme. 

“MWENYEWE” ni kipashio cha urejeshi kinachosimama kumaanisha “huyo hasa” 
“NDIYE” ni kipashio cha urejeshi kinachosimama kumaanisha “ni yeye” 
“MWENYE” ni kipashio cha urejeshi kinachosimama kumaanisha “aliye na”

Urejeshi katika Kiswahili haumalizikii kwenye hivi vinavyoweza, peke yake, kuitwa viwakilishi, bali umo pia ndani ya vitenzi kupitia kwa viambishi “-ji-” , “-amba” na pia “-o-” (mara nyingine –ye- katika ngeli ya YU-A-WA). Mifano hii inathibitisha hayo:

“JI” - Watoto wamejipaka rangi 
“O” - Watoto waliojipaka rangi wamependeza 
“YE” - Mtoto aliyejipaka rangi amependeza
“AMBA” - Mtoto ambaye alijipaka rangi anapendeza

Ambapo “-ji-” ndani ya kitenzi inarejea dhana ya 'kujitenda’, “-o-” na “-ye-” zinarejelea mtendaji mwenyewe (hapa) au katika mifano mingine mtendwa.

Huu ndio ninaouita upekee na upana wa dhana za uambishaji na urejeshi katika lugha Kiswahili. Ni sifa ya kipekee inayoitofautisha Kiswahili na lugha nyinginezo.