Uandishi ni kama kufuma mkuki gizani

John Habwe

Profesa John Habwe. Picha/ CHRIS ADUNGO 

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Sunday, January 22  2017 at  18:41

Kwa Mukhtasari

INGAWA mojawapo ya changamoto kubwa zinazotatiza jitihada za kueneza na kukiendeleza Kiswahili humu nchini ni kukosekana kwa tafiti nyingi zinazohusu lugha hiyo, wachapishaji na waandishi wa vitabu pia ni sehemu kubwa zaidi ya masaibu hayo.

 

Kukosa uhakika wa kupokea mrabaha na ulazima wa waandishi kusubiri kwa muda mrefu kula jasho la jitihada zao ni tatizo jingine linalotatiza makuzi ya Kiswahili hasa katika janibu hizi za Afrika Mashariki.

Uchache wa kazi zilizotungwa aghalabu huchangiwa pia na makusudi ya wachapishaji kuwabagua waandishi chipukizi ambao hujitahidi kila uchao kuboresha viwango vya lugha kutokana na udhati wa mapenzi yao katika kukichapukia Kiswahili.

Huku tukisisitiza umuhimu wa vijana katika kuendeleza taaluma za Kiswahili na nafasi yao katika uandishi wa kazi za kibunifu, baadhi ya mashirika ya uchapishaji hukataa kutoa vitabu vya watunzi chipukizi na badala yake kuzichapisha tungo za waandishi wakongwe wenye majina ya kutajika.

Jambo hili huwavunja mioyo sana waandishi wanaoinukia katika Kiswahili pamoja na wale ambao wangependa kujiendeleza kitaaluma kupitia sanaa ya utunzi.

Hii huenda ikawa sababu ya mwandishi mmoja au wawili kutawala baadhi ya tuzo zinazotolewa na mashirika mbalimbali katika jitihada za makuzi ya Kiswahili pamoja na fasihi yake.

Katika Tuzo za Fasihi za Wahome Mutahi mwaka huu kwa mfano, kitabu Kovu Moyoni chake Profesa John Habwe ambacho kilichapishwa na kampuni ya Bookmark Africa kiliibuka cha kwanza katika Kitengo cha Kiswahili na kuvipiku Mashetani ya Ulepo na Narejea vilivyotungwa na Dkt Tom Olali (mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi) na Bw Jeff Mandila mtawalia. Viwili hivyo vilichapishwa na shirika la Jomo Kenyatta Foundation (JKF).

Prof Habwe ambaye amezitawala na kutamalaki tuzo hizo kwa muda mrefu tangu kuasisiwa, alitawazwa mshindi wa makala ya kwanza ya tuzo zenyewe mnamo 2006 kutokana na kitabu chake Paradiso kabla ya Cheche za Moto kumtwalia taji hilo kwa mara nyingine mnamo 2010.

Ingawa hivyo, mwalimu mtajika Guru Ustadh Wallah Bin Wallah ambaye ni mwandishi mashuhuri wa Kiswahili humu nchini anashikilia kwamba baadhi ya changamoto wanazozipitia watunzi ni za kujitakia wao wenyewe.

Msomi huyo maarufu ambaye pia ni mwanzilishi wa WASTA Kituo cha Utafiti wa Kiswahili Mufti kilichopo mjini Ngong anasisitiza kwamba kubwa zaidi ambalo wengi wa waandishi wamekosa kulizingatia kwa kina cha fikira ni kupanga vyema jinsi ya kuzitumia fedha chache zitokanazo na mauzo ya vitabu wanavyochapishiwa.

Akiwa mmoja kati ya waandishi wachache wa Kiswahili wanaojivunia tija na fahari tele kutokana na upekee wa vipaji vyao vya kukisarifu Kiswahili pamoja na kuzihifadhi kwa busara tamaduni za lugha hiyo vitabuni, uandishi umemvunia Wallah Bin Wallah mambo makubwa yanayompa kitulizo kamili katika maskani yake ya kuvutia katika eneo la Matasia, Ngong.

Ufanisi huu wote ambao Doyen huyo wa Kiswahili anajivunia katika himaya yake umetokana na uandishi wa vitabu, hasa msururu wa Kiswahili Mufti na Mazoezi na Marudio Mufti ya Kiswahili ambavyo vimebadilisha pakubwa sura ya viwango vya usomaji na ufundishaji wa Kiswahili katika shule nyingi ndani na nje ya Afrika Mashariki.

“Uandishi ni sawa na hatua ya mtu kurusha mkuki gizani kwa sababu hujui utakifuma nini hatimaye. Baada ya kujinyima mengi kisha kufanikiwa kupata mrabaha japo mdogo, jambo ambalo waandishi wengi hukosa kabisa kufanya ni kuziwekeza kwa busara fedha zao,” anakiri Guru Ustadh.

Japo anasisitiza kwamba ni vigumu kwa baadhi ya vitabu kupenyeza na kudumu sokoni kwa muda mrefu, waandishi wengi hujipata katika ulazima wa kukabiliwa na pigo hilo kutokana na uchapwa wa kazi zao.

“Mwandishi yeyote huwa na wazo ambalo anataka kuliwasilisha kwa hadhira yake kwa sababu hupata ilhamu ya kuandika kutokana na mambo yanayomzingira katika jamii yake.

Baadhi ya waandishi, ijapokuwa wana wazo, hawajui kabisa namna ya kuliwasilisha, jinsi ya kulisuka na kulikuza kisha kuliendeleza ipasavyo katika kazi wanazozitunga.

Wengi wa waandishi hawa hukosa waelekezi ambao wanaweza kuwaongoza au kuwashauri vilivyo kuhusu taaluma nzima ya uandishi wa vitabu,” anasisitiza Guru Ustadh ambaye pia anajivunia Mazoezi na Marudio ya Gateway KCPE Kiswahili, Taswira ya KCPE Kiswahili, Insha Mufti na Chemsha Bongo tangu kutia guu katika ulingo wa uandishi mnamo 1988 kwa kutunga Malenga wa Ziwa Kuu, diwani ambayo inatumiwa sana katika Vyuo vya Ualimu kote nchini Kenya kufundishia taaluma ya ushairi.

Tatizo la ni yapi maudhui yanayopaswa kuipa dira kazi ya mwandishi ni changamoto nyingine. Kilicho muhimu kwa mtunzi ni kutambua kiwango cha umuhimu na uzito wa mawazo yake kwa jamii anayoiandikia.

Maudhui ya mapenzi na ndoa, ushirikina, dini, ukoloni mamboleo na uhalifu yalishamiri sana katika kazi za uandishi wa Kiswahili katika miaka ya awali japo bado kuna waandishi wanaong’ang’ania kuyaandikia masuala hayo.

Na ni kweli asemavyo Wallah Bin Wallah kwamba mwandishi si mtu wa ajabu awezaye kuishi kwa kula hewa au kunywa ukungu.

“Mwandishi ni binadamu ambaye sawa na watu wengine wa desturi, hafarijiwi kwa hasara. Anapokaa chini kuandika anatarajia kitabu chake kitoke vizuri na kwa haraka iwezekanavyo, kisomwe na watu wengi iwezekanavyo na apate chochote kiwezekanachokutokana na jasho lake.”