Ugumu wa kutenganisha fasihi na maisha ya wanajamii

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Sunday, January 22   2017 at  18:34

Kwa Mukhtasari

NYINGI za fasili ambazo zimetolewa na wataalamu kuhusu fasihi, zimeegemea katika kuileza sanaa hiyo kwa kujikita katika msingi wa uhusiano wake na jamii.

 

Fasili hizi zimeonyesha kwamba fasihi ni moja katika taasisi muhimu za jamii na uhusiano wake na jamii hauwezi kupuuzwa wala kuchukuliwa vivi hivi.

Upo ulazima wa fasihi kuchukuliwa kama taaluma iliyo na uhusiano usiotatanika na maisha ya kawaida ya wanajamii. Fasihi ni taasisi ya kijamii, inayotumia lugha (ambalo ni zao la amana ya jamii) kama mtambo wake.

Isitoshe, kama kioo cha jamii, fasihi huwakilisha maisha ya kila siku kwa kuwa 'haizaliwi’ kwa ombwe tupu. Maisha kwa upana wake huhusu uhalisia wa kijamii, hata ingawa ulimwengu halisi na hata ulimwengu wa ndani ya mtu binafsi ni mambo yanayoweza kuzingatiwa katika fasihi.

Mbali na hayo, tunafahamu kwamba iwapo fasihi hulenga watu fulani, basi bila shaka hiyo fasihi yahusu jamii fulani lau sivyo hapana haja kutungia watu kazi isiyowahusu ndewe wala sikio.

 

Mazingira

Jambo jingine la kutaja hapa ni kwamba, mtunzi mwenyewe ni mwanajamii kwa ambavyo ana nafasi na tabaka fulani katika jamii yake; yeye hutambuliwa na jamii kama mmoja wao.

Hawezi kuepuka nafasi hiyo yake katika jamii wala hawezi kukwepa athari ya jumuiya katika utunzi wake kwani kama mtoto mchanga yeye anafundishwa maadili na itikadi za jamii yake ili kuweza kuenea katika jamii hiyo.

Na kama ambavyo nimetaja tayari, mtunzi hulenga hadhira fulani hata iwe ndogo vipi. Zaidi ya yote, mwanafasihi hupata kichocheo na ilhamu ya utunzi wake kutokana na yanayomzingira katika jamii yake.

 

Uhusiano

Mara nyingi fasihi hutokana na uhusiano wa karibu sana na taasisi maalum za kijamii. Taasisi za kiuchumi, kisiasa na kijamii zimekuwa na uhusiano mkubwa sana na utoaji wa fasihi na kila kazi ya fasihi kwa njia moja au nyingine, hudhihirisha ukweli huu.

Maendeleo na mabadiliko ya jamii yametokea kuwa maendeleo na mabadiliko ya fasihi hivi kwamba hatuwezi kutenganisha fasihi na jamii inamoibukia.

Uhusiano huu unatokea kwa sababu pindi maisha ya jamii yabadilikapo, mielekeo, tamaduni na hata maadili ya jamii pia hubadilika. Aidha, mabadiliko ya fasihi kutoka simulizi hadi andishi ni zao la mabadiliko katika maisha ya jamii ambapo taaluma ya kusoma na kuandika ilitokea.

 

Kielelezo

Kwa hivyo fasihi inalo jukumu kuu katika jamii ambalo sio la kibinafsi, bali ni la kijamii. Katika kuiunga mkono kauli hii, Wellek na Warren (1949) wanasema kwamba uhusiano kati ya fasihi na jamii hujadiliwa kwa kuanza na kauli aliyoitoa De Bonald (1942) kwamba `fasihi ni kielelezo cha jamii’.

Kwa hivyo ni muhimu kuichukulia fasihi kama zao la jamii ambalo pia huathiri na kuathiriwa na jamii.

 

Utengano

Tunaloweza kuongeza ni kwamba pana tatizo linalokumba juhudi yoyote ya kujaribu kutenganisha fasihi na jamii kwani fasihi huathiriwa na mandhari ya kijamii pamoja na mabadiliko na maendeleo yake.

Isitoshe, mtunzi ni mwanajamii anayetumia lugha ya jamii kutunga kazi yake ili kuwafifikia wanajamii husika. Ukweli huu wanaogusia waandishi hawa utategemea mtazamo, matarajio, na tajiriba za anayehusika kwani hali mbalimbali katika jamii hutoa maana mbalimbali kwa watu mbalimbali hata kama ni wa jamii moja.

Hivyo basi ukweli hubainika tu kimuktadha. Wale wanaosisitiza kigezo cha fasihi na jamii katika kuieleza fasihi, wametoa kauli kwamba pana aina mbalimbali za fasihi ambazo zinachukuana na jamii mbalimbali.

 

Uhifadhi

Dhana kama vile fasihi ya Kirusi, fasihi ya Kiafrika, fasihi ya Kiingereza n.k. ni baadhi ya mifano ya kazi za fasihi zinazohusishwa na jamii fulani.

Fasihi kama hizi hulenga jamii fulani pana zenye kaida na maadili yanayopatana katika muundo wa kijumla kwani katika jamii hizo huwa kuna vijamii vidogo vidogo.

Mojawapo ya majukumu ya fasihi ni kule kuihifadhi historia ya jamii husika. 'Dunia Mti Mkavu’ (Said A. Mohamed) ni mfano wa kazi inayoonyesha historia ya unyonyaji na unyanyasaji wa mfumo wa ukoloni, 'Mashetani’ (Ebrahim Hussein) ni mfano wa kipindi cha ukoloni-mamboleo, na utenzi wa 'Al-Inkishafi’ (Sayyid Nassir) ni kielelezo cha historia ya mji wa Pate.

Hivyo basi, dhana kuwa fasihi ina uhusiano mkubwa na jamii ina mashiko. Iwapo tutakubali kwamba kazi ya fasihi si amali ya mtu binafsi, basi tutakuwa tayari tumeonyesha kwamba fasihi na jamii ni vitu visivyotengana.