Ugumu wa kutenganisha ubunifu na uongo katika fasihi

Clara Momanyi

Profesa Clara Momanyi – mwandishi mashuhuri, mtaalamu na mhadhiri maarufu wa Kiswahili ambaye ni Mkuu wa Idara ya Lugha, Fasihi na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA), Nairobi. PICHA/CHRIS ADUNGO 

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Sunday, January 22  2017 at  18:20

Kwa Mukhtasari

INGAWAJE kazi ya fasihi kwa kawaida huwa ikijaribu kuyaumba upya maisha ya binadamu kwa njia moja au nyingine, tunatambua ukweli kwamba yaliyotungwa na mwanafasihi katika sanaa yake si kiwakilishi cha maisha halisi moja kwa moja katika jamii.

 

Kwa mtazamo huu yaelekea kwamba fasihi haisawiri maisha halisi pekee siku zote bali ni tokeo la ubunifu wa mtunzi. Mtunzi ana uwezo wa kubuni visa na wahusika wake kwa njia ambayo haikanganyi hali halisi ya maisha.

Hata hivyo, ubunifu huu lazima uongozwe na kaida au kanuni za hali halisi ya maisha kwa kuwa chochote utakachochagua kwa minajili ya kupendeza, hakikisha kwamba kipo karibu na ukweli.

Yaani, mtunzi anapaswa kuufanya ulimwengu wake wa kubuni kuwa picha halisi ya maisha katika ukamilifu na ukweli wake, hata ingawa aliyoyashughulikia ni ya kubuni tu.

Mwanafalsafa, Horace (1975) anafafanua zaidi kauli hii asemapo kwamba washairi na wachoraji wamekuwa wakifurahia uhuru wa utunzi na kufanya majaribio jinsi watakavyo.

Hili nalifahamu, na mimi kama mshairi hufurahia uhuru huo; lakini si kwa kiwango ambacho kwacho viumbe visivyotangamana vinawekwa pamoja, hivi kwamba ndege na nyoka wanawekwa pamoja, wanakondoo pamoja na simba marara, vifaranga pamoja na mwewe.

 

Uhuru wa kubuni

Anachosisitiza Horace ni kuwa, hatuwezi kumnyima mtunzi uhuru wa kubuni, lakini mtunzi akumbuke kwamba ubunifu wake usikiuke kaida zinazotawala na kuongoza maisha halisi ya kila siku katika jamii. Kumpa mtunzi uhuru wa ubunifu na kisha umtarajie afuate kaida fulani ni kumnyima uhuru kamili.

Kama mtunzi atakanganya hali halisi ya maisha kama mbinu yake ya kutunga, basi na tumpe uhuru huo alimradi kazi yake tutaielewa kwa mtazamo huo.

Kwa hivyo, fasihi si kazi inayohusu mambo ya kipekee bali ni uwasilishaji wa maisha ya jamii kwa njia bunifu isiyo ya moja kwa moja.

Ndiposa Aristotle (1975) anasema kwa uwazi kwamba, si jukumu la mshairi kuendeleza yaliyotokea bali huendeleza yanayoweza kutokea; yaani kinachoweza kutokea katika msingi ya haja au uwezekano.

Hapo ndipo fasihi hutofautiana na historia kwani wakati fasihi huendeleza linaloweza kutokea, historia huendeleza kilichotokea; na fasihi ikieleza lililotokea hulieleza kisanaa, na si kwa njia ya moja kwa moja.

Hivyo basi, fasihi ni utanzu unaoendeleza maisha kwa njia bunifu iliyojikita katika msingi na kaida zinazotawala maisha halisi.

 

Uhalisia

Ili kueleza maana ya fasihi, wataalamu wengi wamejaribu kuzingatia baadhi ya vigezo vinavyoitambulisha, hasa ikiwekwa katika mkabala mmoja na tanzu nyingine za maisha ya jamii.

Tunaweza kusema kwamba dhana ya ubunilizi ni njia nzuri ya kutofautisha fasihi na uhalisia pamoja na ulimwengu halisi. Lakini kupitia kwa dhana hii hatujaelezwa hasa kinachofanyiwa malighafi ya kazi ya fasihi.

Ili kutimiza hilo, dhana nyingine imependekezwa; kwamba kazi ya fasihi yapaswa kuchukuliwa kama muundo, kama mpangilio maalum.

Kila kazi imepangwa kwa hali ya juu sana na viungo vyake vinategemeana hivi kwamba kazi kamilifu huwa ni mwafaka zaidi kuliko kiungo chake kimoja.

Aristotle amelizungumzia swala hili hata ingawa uzingativu wake unaeegemea zaidi kwa upande wa ploti. Kama chombo kizuri, kiwe kiumbe au kitu kizima kilichojengwa kwa vipande, kazi ya fasihi yapaswa kutolewa kama kitu kimoja.

Ploti, kama kitendo, lazima imithilishe kitendo kimoja na muungano wa vipande vya kitu kizima kiasi cha kwamba kipande kimoja kikiondolewa pale, kile kitu kizima hutengana.

Kwani kipande ambacho hakitoi athari kiondolewapo, bila shaka si kipande halisi cha kizima. Tukitazama fasihi kwa njia hii, tunatambua umoja na uwiano wa kila kazi inayotungwa ieleweke na iwe na muundo maalum unaokubalika.

 

Uhusiano

Hivyo basi, kazi ya fasihi ni muundo wa vipande vinavyopatana na kuhusiana ili kujenga kitu kimoja. Kipande kimoja cha kazi hiyo huwa hakina maana yoyote kivyake mpaka kihusishwe na vingine.

Kama ambavyo dhana ya ubunilizi hutusaidia kutofautisha fasihi na matukio halisi maishani, dhana ya muundo hutuwezesha kutofautisha fasihi na matumizi mengine ya lugha.

Inatutolea ile hali ya usababishano, kwamba kazi ya fasihi ni utungo ulioundwa kwa visa vinavyowiana hivi kwamba kimoja hutangulia kingine.

Pia, kisa kimoja hutokea ili kusababisha kingine na vyote vinahusiana kwa njia ambayo kimoja hakiwezi kueleweka bila kingine.

Haya yote yanawezekana kupitia lugha inayotumiwa. Kwa hivyo katika muundo, tunazingatia jinsi lugha inavyotumiwa kwa kuwa ni sura ya nje ya kazi ya fasihi.