Ukanushi wa 'Ni' na 'Ndio' si sawa kama inavyodhaniwa

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, April 18  2017 at  14:50

Kwa Mukhtasari

KATIKA hali ya kukanusha maneno ya Kiswahili, ni jambo faafu mno kuzingatia neno lenyewe kabla ya kufikia tamati na kuidhinisha kuwa neno hilo ndilo jibu sahihi.

 

Ukanusho wa vitenzi vishirikishi vipungufu unahitaji umakinifu mkubwa sana ili kutozua taharuki katika nyanja hizi ya Kiswahili iliyo na umuhimu mpevu sana.

Vitenzi vishirikishi vipungufu huchukua viwakilishi nafsi tu na wala havichukui viambishi vya hali au wakati.

Tunapokanusha vitenzi ‘ni’ na ‘ndio’, lazima tuzingatie kwa kina aina ya neno lenyewe ili tuzuie kusumu na kuvunja sheria adimu ya ukanusho katika lugha hii.

Hivyo basi ‘ni’ ikiwa ni kitenzi katika kitengo hiki, neno litakalo faa kutumiwa katika ukanusho wake ni ‘si’ wala si ‘sio’. Hii ni kwa sababu kuwa vitenzi hivi huwakilisha nafsi ya mtendaji au mtendewa wala si kitu kingine chochote. 

Vile vile, ni muhimu kuhakikisha kuwa mantiki na upatanisho wa kisarufi unazingatiwa katika kila sentensi tunayo iandika na kuitamka.

Kwa mfano;

(i) Mji mkuu wa Kenya ni Nairobi.

(ii) Mji mkuu wa Kenya si Nairobi.

(iii) Mji mkuu wa Kenya sio Nairobi.

Sentensi zilizoko hapo juu zinaashiria hali mbili za kuyakinisha(i) na ukanusho(ii) (iii). Sentensi (ii) inaonyesha kwa kimantiki kwamba Nairobi si mji mkuu wa Kenya na  kwa ufasaha unaozingatia upatanisho wa kisarufi.

Sentensi ya (iii) ingekuwa sahihi pale neno la kukanushwa lingekuwa ‘ndio’ badala ya ‘ni’.

Mfano katika sentensi wa kuonyesha jinsi ‘ndio’ inaweza kukanushwa na kubeba mantiki ndani mwake ni ifuatayo.

 (iv) Anachokisema bwenyenye huyu ndio ukweli.

(v) Anachokisema bwenyenye huyu sio ukweli.

Sentensi ya (v) inaonyesha jinsi ndio imekanushwa vyema bila kuvunja sheria yoyote ya kisarufi na kimantinki.

Ikiwa lazima mwandishi au msemaji atumie ‘ndi-‘ akirejelea nomino basi ni vyema akitumia kwa mfano ‘ndiye’.

Tunapokanusha vitenzi vishirikishi vipungufu tuwe waangalifu ili tusipotoshe wenzetu kwani kila uchao twajifunza kutoka kwa wenzetu. Vyuma vinavyowekwa pamoja hunoana.