'Usasa Usasambu' sehemu ya nne B

Na WILLIAM HIMU

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  15:51

Kwa Muhtasari

'Usasa Usasambu' sehemu ya nne B

 

(Kengele ya kuingia darasani inalia, wanafunzi wanaongeza mwendo kuwahi darasani. Kidato cha nne anaingia mwalimu Bashiri na fimbo yake mkononi, anagonga mlango kwa fimbo akiwa amekunja uso. Darasa linakuwa kimya na kila mwanafunzi anarudi kukaa sehemu yake.)

Mwl. Bashiri: Jamani siku ya leo kipindi changu  hakitakuwepo,  kuna kikao cha walimu (Kabla hajamaliza wanafunzi  wote wanashangilia.)

Wanafunzi: Safiiiiiii, oiii oiiii oyeeeeee!

Mwl. Bashiiri: Shiiiiii, kelele! (Anapiga tena fimbo mlangoni kwa nguvu)

Mnashangilia nini? (Anaondoka taratibu.)

Wanafunzi: (Kimya kidogo… Baada ya mwalimu kuondoka kelele zinaendelea. Mwanawima, Mwanaharusi na Mwanakombo wamekaa nyuma kabisa ya darasa wanajadiliana jambo.)

Mwanakombo:  Vipi Mwanawima, Jumamosi tutakwenda kwa shemeji? Nimekumbuka chipsi kuku na juisi (anamtania) kweli umepata kidume.

Mwanawima: Kama kawaida, lazima tukajivinjari. Si anataka hela zake ziliwe.

Mwanaharusi: Mnaona raaaaaaaha! Iko siku zitawatokea puani.

Mwanawima: Hakuna anayemuomba, anazileta mwenyewe. Mmmh! (anaonekana kama amechefukwa na kitu) Ila tangu juzi najisikia kichwa kinauma, jana nilitapika na leo sipo sawa.

Mwanaharusi: Pengine una homa.

Mwanawima: (Anaweka mkono tumboni) Siumwi sana ila najihisi uchovu tu, kichefuchefu na kizunguzungu.

Mwanakombo: Usije ukawa umenasa kwenye mitego ya watu. Maana hizo dalili ni zenyewe kabisaa (anaongea kwa utani kisha anacheka.)

Mwanawima: Una maana gani kusema hivyo?

Mwanakombo: Hizo zote ni dalili za ujauzito shoga au unajifanya hujui/ Wahi kapime kabla kitumbo hakijaonekana.

Mwanawima: Usiseme hivyo Mwanakombo…

Mwanakombo: Nisiseme hivyo nini! Mimi nakutahadharisha ili ujue kama ulijisahau wenzio wamekuwahi.

Mwanaharusi: Sisi tunakutahadharisha tu shoga, kama unajisikia kizunguzungu endelea kula chipsi kuku za watu, utasikia mpaka kichina china mwaka huu (Anatania na wote wanacheka. Ghafla ananyanyuka na kukimbia nje huku akiwa ameziba mdomo. Anatapika! Kwa muda anabaki ameinamisha kichwa chini, wenzake wanamfuata na kumwinua.

Mwanaharusi: Sasa tufanyeje? Niliwaambia vitawatokea puani, twende kwa mwalimu wa zamu…

Mwanakombo: Kweli wewe chizi… Kama hauna cha kuongea funga kopo lako, uende kwa mwalimu wa zamu kufanyaje?

Mwanaharusi: Chizi mwenyewe, huu ni ushauri wangu na wewe toa wa kwako. Unajiona una akili sana! (Ananyanyuka na kujitenga na wenzake, anakaa pembeni yao kidogo na kuanza kuimba).

 

Sizipendi simu hizi, simu za smartphone,

Mambo yote ya kishetani, yaoneshwa hadharani,

Uchafu wote u wazi, kwa watoto na wazazi,

Hii si teknolojia, ni teke tutalojutia.

 

Watu hukesha na simu, picha ngono kuziona,

Kutongozana kwa simu, si lazima kujuana,

Kipewa namba za simu, mchezo kumalizana,

Wakubwa kwa wadogo, balaa limewakumba,

Si watoto wa vigogo, hata wa mlo mmoja,

Masomo wapa visogo, kutwa kujipiga picha.

 

Twita nazo fesibuku, zina sumu za vileo,

instragramu na whasapu, wanaiga mavalio,

Kuonesha mili yao, waita usasa wao,

Macho mnatupofua, sisi watoto wadogo,

Maadili mnaua, oneni haya kidogo.

 

(Wenzake wanamsogelea ananyanyuka na kuondoka huku akiwa na hasira.)

Mwanawima: Mwanaharusi usiondoke nisaidieni…