Usasa Usasambu sehemu ya Tano B

Na WILLIAM HIMU

Imepakiwa - Monday, June 25  2018 at  14:39

Kwa Muhtasari

Utandawazi una faida nyingi katika maendeleo ya binadamu kijamii, kisiasa na pia kiuchumi ila kwa nchi nyingi za ulimwengu wa tatu utandawazi umekuwa ni kaa la moto.

 

Sehemu ya Tano B

 

Daktari Twalib: Wasichana wengi hufikia hatua hata ya kujiua pindi wanapokosa msaada kama huu lakini angalia makosa uliyoyafanya na unayotaka kufanya yapi ni makubwa zaidi?

Sakina: Ni kweli daktari, hilo tunalielewa vyema lakini huyu ni mwanafunzi anahitaji kusoma.

Daktari Twalib:Hapa leo unatoa mimba unajiona ni shujaa, lakini umeshafikiria kama ungepata Ukimwi ungeenda kuutoa vipi? Wewe unavyohangaika kutoa mimba kuna wanawake wenzako ndani ya ndoa wanahangaika kwa waganga usiku na mchana kutafuta watoto… nakushauri usifanye hivyo.

Sakina:Daktari nashukuru umetushauri vizuri...

Daktari Twalib: Hamtambui tu, kutibiwa sio mpaka mpewe sindano na hata huu ushauri ninaowapa unaponya kuliko dawa.

Sakina:Ni kweli daktari…

Daktari Twalib:Hivi mnafikiri mimba ni kama puto kwamba ukiamua unatoboa tu upepo unakwisha! Mtakufa! Mtakufa nawaambieni…

Mwanawima: Khoo! Khoo! (Anajisikia kichefuchefu, anawahi kuweka mkono mdomoni na kutoka nje mbio mbio.Anaahirisha kutoa mimba na kurudi nyumbani nguo zikiwa zimejaa machozi…. Mama yao anawaona kwa mbali wakija. Anasimama na kuacha kufua, anafuta mikono yake kwenye kanga na kuwafuata chumbani haraka haraka.)

Mama Mwanawima:Vipi jamani, mmefanikiwa?

Sakina:Hapana Mama, Daktari ametushauri kuwa ni hatari mama kufanya hivyo! Ni kuiweka roho ya Mwanawima rehani mama.

Mama Mwanawima:Wapuuzi ninyi, mlipokuwa mnafanya huo upuuzi wenu roho mliweka kwapani? Sasa kama mmeshindwa mnadhani mimi nitamwambia nini baba yenu? Sitaki kusikia habari hizo. Wewe Mwanawima, utaondoka hapa kwangu.

Sakina: (Kwa sauti ya chini) Usiseme hivyo mama.

Mama Mwanawima:Huyu mdogo wako ameshanikosesha amani. Anataka anigombanishe na baba yenu siyo!  Anafurahi nikiwa natukanwa kila siku kwa makosa yake?

Sakina: Mama huyu ameshatenda dhambi ya zinaa, nakuomba asiongeze dhambi nyingine. Kutoa mimba ni dhambi kubwa sana mama kuliko kuipata na sisi tunayemshinikiza kuitoa tutakuwa tumeshiriki moja kwa moja.

Mama Mwanawima:Aondoke aende akafie huko, yeye si anaona  ameshakuwa mkubwa!

Sakina: Hapana mama, tukae tutafute njia nyingine lakini sio kuua. Mhurumie mwanao. Angalia madhara yatakayompata endapo atatoa mimba, fikiria mara mbili mama…

Mama Mwanawaima: Anatakiwa ajue kuwa ukila muwa lazima  ukutane na fundo, basi kama aliona raha sasa hilo ndio fundo lake.

Sakina: Kutoa mimba ni kama mchezo wa bahati nasibu. Unaweza  kupoteza maisha au usizae tena.  Huyu bado ni binti mdogo mama. Hatuwezi kuijua kesho yake, bado ana safari ndefu.

Mama Mwanawima:Haya mwambie aende akamwambie baba yake, mimi siwezi kumvisha paka kengele.

Sakina:Hapana mama, wewe unaweza ukaongea na baba lakini sio Mwanawima wala mimi. Sisi tumekwishamkosea…

Mama Mwanawima:(Anamuangalia mwanaye kwa hasira) Umefurahi enhee, lione pua lake lilivyoning’inia…

(Kimya kinatanda, wote wameinamisha vichwa chini wakiwa wanawaza na kuwazua. Baada ya muda kidogo, Mama Mwanawima anajifunga mtandio wake vizuri na kumfuata mumewe chumbani, anatetemeka na mafua ya ghafla yanamjia.)

Mama Mwanawima:Mume wangu samahani, hali ya hewa hapa nyumbani sio nzuri leo. Kuna jambo limenishtua sana, nimeona nikuambie ili tushauriane cha kufanya mume wangu.

Baba Mwanawima:Jambo gani, Amezidiwa?

Mama Mwanawima:Hapana mume wangu! Ugonjwa wenyewe daktari kagundua kuwa mwanao ni mjauzito.

Baba Mwanawima:Nini? Eti mwanao ni mjauzito (Anabana pua.) Mtoto niliyemzaa mimi hawezi kupata ujauzito nje ya ndoa huyo aliyepata ujauzito ni mtoto wako si wa kwangu.

Mama Mwanawima:Sasa ndio hivyo mume wangu mambo yamekwishaharibika. Mtoto akikunyea mikono, huwezi kuukata mkono kwa kuhofia harufu.

Baba Mwanawima:Kimya wewe! Msinifanye mimi sina akili, wewe unajua yote hayo.Wewe na mwanao lenu moja, mtoto hawezi kuwa na mimba ya miezi mitatu mama usijue… Msinichezee shere miye.

Mama Mwanawima:Sasa tunafanyaje mume wangu, hii aibu ni yetu sote, tuungane katika hili…

(Muda wote huo Mwanawima na Sakina wanasikilizia kwa makini mlangoni nini kitaendelea).

Baba Mwanawima:Hapa kwangu ataondoka… silei makahaba mimi unataka nichekwe? Aende huko huko… Mwaharamu mkubwa!

 Anatoka na panga…Mwanawima kuona vile anakimbia na kupiga kelele kuelekea kwa mama Mwanakombo. Anafika akiwa anahema kama kaona mzimu, anamkuta Jumbe, babu yake Mwanakombo amekuja kusalimia toka kijijini.)

Jumbe:  Hee mbona wima wima sana kuna tatizo?

Mwanawima:Ndio babu, baba anataka kuniua.

Jumbe: Anataka akuue, amechanganyikiwa? Kwani kuna tatizo gani mpaka akuue!

Mwanawima:  Nisaidieni jamani, nisaidie babu nakufa.

(Jumbe anatoka mguu kwa mguu na Mwanawima mpaka nyumbani kwao, anabisha hodi huku Mwanawima akiwa nyuma kwa woga.)

Jumbe: Hodi hapaaa, asalam alaykum jamani.

Baba Mwanawima: Waalaykum salaam, ooh mzee karibu!

Jumbe: Asantee, Mimi nimeingia jana tu hapa mjini, naona watu wanajenga kweli kweli.

Baba Mwanawima: Watu siku hizi wanashindana kujenga majengo marefu tu hapa mjini.

Jumbe: Enheee mbona unataka kuuwa watu tena mwanangu!

(Amemshika Mwanawima mkono.)

Baba Mwanawima:Afadhali umekuja mzee, nimeamua nimfukuze

huyo mjukuu wako, simtaki tena katika familia yangu.

Jumbe: Hee! Kwa nini! Amefanya kosa gani kubwa kiasi cha kumfukuza?

Baba Mwanawima:Mzee najua nikikueleza hutokuwa na radhi na huyu mtoto.

Jumbe: Kafanya nini, hebu niambie (Anavuta kiti anakaa vizuri.)