http://www.swahilihub.com/image/view/-/2591264/medRes/923032/-/5jmdufz/-/verse.jpg

 

Ushairi ni kama hisabati inayotegemea maneno badala ya nambari

Wanafunzi katika tamasha

Wanafunzi wa kike wa Shule ya Upili ya Kahuhia awali wakiwa jukwaani katika Shule ya Msingi ya Menengai wakikariri shairi la Kiswahili "Tunda" likitahadharisha dhidi ya kujiingiza kwa ngono za mapema. Picha | ANTHONY NJAGI 

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Sunday, January 22  2017 at  18:08

Kwa Mukhtasari

USHAIRI ni sanaa kongwe na pevu sana. Ni kongwe kwa kuwa ndiyo njia ya kwanza aliyoitumia mwanadamu kufafanua hisia zake kupitia lugha na sauti hata kabla ya kuanza kutumia njia nyingine za kujieleza.

 

Ni pevu kwa kuwa ni bahari inayobeba kiwango cha juu cha maarifa. Lakini hapa penye sifa zake ndipo pia penye ila zake kwa kuwa kile ambacho mwingine angekichukulia ni sifa za ushairi, ndicho hicho hicho kilicho ila yake.

Mojawapo ya sifa za ushairi ni uwezo wa kuyasema mambo mengi kwa maneno machache. Kile ambacho mwandishi wa riwaya angehitaji zaidi ya kurasa 300 kukidadavua, mshairi huhitaji mishororo mitatu au minne tu.

Kwa mfano, mtazamo wa wale wasioyaamini matokeo ya wanaokisia au kuagua mambo yajayo yalielezwa hivi majuzi kwa ubeti huu mmoja na mmoja wa marafiki zangu katika mtandao wa Facebook:

 

Kukusanya makuhani, na wapigaji ramli,

Wasomao kiganjani, wakakupa taawili,

Hakulishindi tufani, mja linokukabili,

Analotaka Jalali, huwa kun-faya-kuni.

 

Mara baada ya kuuweka ubeti huo kwenye ukurasa wake, maoni mbalimbali yalimiminika ili kufafanua, kukosoa, kutilia mkazo na hata kuongezea kilichomo katika ubeti huo.

Nilihisi kwamba ubeti huu ulitosha kulitoa joto lote alilokuwa nalo rafiki yangu huyo na baada ya kuuandika na kuubwaga, sidhani alikuwa tena na haja ya kusema zaidi kuhusiana na mada hiyo.

 

 

Sifa

Lakini kwa kuwa sifa hii pia ndiyo ila ya ushairi, ubeti huu ulichochea pia wengine kuyafasiri mawazo yake kwa muktadha wa wanayoyadhani wao, na huenda mengine hata hayakuwamo kabisa katika mtima wa mtunzi wa kwanza wakati alipolisarifu shairi hilo.

Nilipouweka ubeti huu kwenye ukurasa wangu, nilipokea maoni mengi yaliyokwenda mbali sana na pale nilipopakusudia:

Ninataka unitoke, unyonge nilionao,

Ufukara ukopoke, nyumbani nisiwe nao,

Bali nisidhalilike, heshima nibaki nayo.

 

Mmoja kati ya marafiki zangu aliniandikia:

Ufukara ni silaha, subira ukiwa nayo,

Hata mbele ya Wadudi, hisaba huwa hunayo,

Kwa uwezo wa Rabbana, pepo ndio mafikiyo.

 

Hapana shaka kwamba yeye alidhani kuwa nazungumzia ufukara wa mali na hali halisi katika nyumba yangu binafsi, jambo ambalo silo nililokusudia asilani. Mwingine akaenda mbali zaidi ya alipofika yule wa kwanza, akiaminishwa kuwa nimefilisika sana!

Yaonyesha umechoka, dhofulhali haliyo,

Hadi unalalamika, mazito uliyonayo,

Mbona unapapatika, wakosa hata chajiyo?

 

Sifa yake nyingine ni kuwa ushairi ni kulisema neno zaidi ya neno na katika kulisema huko likazua maneno mengine mengi mno hata yakakuzidi kimo wewe msemaji, na huko njiani ukajikuta kama tiara inayoelea kwenye anga ya maneno ukiuacha upepo ukupeleke utakako.

Hebu angalia hapa majadiliano katika beti za marafiki zangu baada ya mmoja wao kuandika: Iki Kinana kinani, kunena maneno yano?

Yasonenwa na waneni, wenye ya ndani maono,

Kicho chayanena kwani, kwa inda na matukano,

Ama chazibeba kuni, za moto wa farakano?

 

Mmoja aliandika:

Kinana tanena sana, ela siye tuwa pano,

Kwa kavu tunashonana, twataka maridhiano,

Na kwao siye hapana, tunachoka majivuno,

Kama kunena nena tena, Kinana domo unalo!

 

Mwingine akaingia na:

Kinana chajichanganya, kwa kisemayo mchana,

Wala busara hakina, ingawa kizee sana,

Nakionea huruma, kisije kufa chaona,

Vijana wamekichoka, wasije kukitafuna!

 

Licha ya uwezo wa ushairi kuligeuza neno kuwa zaidi ya neno, ila yake ni kuwa wakati mwingine ni rahisi sana kujiona unachukuliwa na ukubwa wa maneno yako mwenyewe na kuanza kuwa mtumwa wake. Yakakupeperusha angani kisha yakakuangusha mahali tofauti au

hata kukupoteza kabisa.