Ushirikiano utapiga jeki maendeleo ya Kiswahili Afrika Mashariki

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Sunday, January 22  2017 at  17:20

Kwa Mukhtasari

JINSI ambavyo zipo jamii nyingi za tamaduni mbalimbali duniani, vivyo hivyo ndivyo zilivyo lugha mbalimbali zilizoundwa ili kukidhi haja muhimu ya mawasiliano miongoni mwa watu mbalimbali.

 

Maingiliano ya jamii zenye mila, desturi, tamaduni na lugha mbalimbali yanayotokana na ushirikiano katika shughuli za biashara na nyinginezo za kijamii, huzua haja ya kuwapo kwa lugha moja itakayoweza kuwaunganisha watu hao wenye mielekeo tofauti za kitamaduni.

Maingiliano kama hayo yanaweza kuwa katika viwango mbalimbali. Kiwango cha kwanza ni kile cha mtu binafsi ambapo mtu hutoka katika jamii yake na kuenda kuishi kwenye jamii inayozungumza lugha tofauti kabisa na yake.

Katika hali kama hiyo, itamlazimu mtu huyo ajifunze lugha ya jamii ya pili ili aweze kuwasiliana nao. Kiwango cha pili ni kile kinachohusisha mkusanyiko wa watu waliotoka katika tamaduni mbalimbali na hawana hata lugha moja ya kuwaunganisha.

Watu kama hawa wakikaa pamoja huweza kuzua lugha ya kati ambayo katika hatua za mwanzo itajulikana kama Pijini na baadaye kuitwa Krioli iwapo itakomaa kimatumizi.

Kiwango cha tatu ni kile ambacho maingiliano ya watu wenye tamaduni na lugha mbalimbali husababisha kuteuliwa kwa lugha moja miongoni mwa lugha zao na kutumiwa kama chombo cha mawasiliano na cha kuziunganisha jamii zote husika.

 

Elimu

Wakati wa enzi ya ukoloni katika eneo hili la Afrika Mashariki, haja ya kuwapo kwa lugha moja ambayo ingetumiwa hususan katika elimu katika nchi zote za makoloni ya Mwingereza wakati ule; yaani Tanganyika, Kenya na Uganda ilijitokeza. Matokeo ya haja hiyo ni kuchaguliwa kwa Kiswahili, hususan lahaja ya Kiunguja ambayo ilitumiwa kama lugha ya kufundishia shuleni.

Vilevile, matokeo ya haja hiyo yalikuwa ni kuundwa kwa Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki (KLAM) mnamo 1925 na kuanza kazi katika mwaka 1930; kamati iliyopewa mamlaka ya kuisanifu lugha ya Kiswahili, ili kuwe na namna moja rasmi ya kusema na kuiandika.

 

Mawasiliano

Baada ya nchi za Afrika Mashariki kupata uhuru, haja ya kuwapo kwa lugha moja kwa kila nchi kwa ajili ya mawasiliano na wananchi, na katika shughuli mbalimbali za kiserikali na za kijamii ikajitokeza.

Tanganyika ilipojipatia uhuru mnamo 1961 (Tanzania tangu 1964) ikajichagulia Kiswahili kilichokuwa kimekwishaenea katika nchi nzima kiwe lugha ya Taifa na Kiingereza kiwe lugha rasmi katika uendeshaji wa masuala ya kiserikali na kimataifa.

Kenya ilipopata uhuru mnamo 1963, kwa kuwa haikuwa na lugha iliyokuwa imeenea katika nchi nzima, na kwa kuhofia mivutano ya kuchagua lugha moja ya wenyeji, haikuteua lugha ya taifa. Hata hivyo, Kiingereza kiliteuliwa kiwe lugha rasmi katika masuala ya kitaifa na kimataifa.

Kiswahili ambacho kilikwishaanza kuzungumzwa na watu wengi, kilitumiwa katika kuwasiliana na wananchi katika mikutano ya siasa na biashara.

Uganda ilipata uhuru mnamo 1962. Ijapokuwa katika kipindi hicho, lugha ya Luganda ilikuwa imekwishaenezwa nchini humo na watawala wa Kiganda.

Lugha nyingine ambayo ilikuwa imeenea kwa kiasi fulani kimatumizi nchini humo ilikuwa Kiswahili. Ijapokuwa pendekezo la Gavana Sir W.F. Gowers la kukifanya Kiswahili kiwe lugha ya elimu na utawala na vilevile kama lugha kwa minajili ya mawasiliano (lingua franca) nchini kote lilipingwa vikali na Kabaka Sir Daudi Chwa mnmao 1929, Kiswahili kiliendelea kupata mashiko, tena kwa kasi kubwa.

 

Maenezi

Kwa mujibu wa Whiteley (1969:70-71), Kiswahili kiliendelea kutumiwa na maafisa wa polisi, katika sehemu za Kaskazini mwa Uganda kuwasiliana na watu ambao hawakuwa na ufahamu wa aina yoyote kuhusu Kiingereza na Luganda. Vilevile, Wanilotiki wa Uganda walitumia sana Kiswahili kuwasiliana na makabila mengine katika ujirani wao.

Kiswahili kilitumiwa pia katika michezo ya mpira na sehemu nyingine ambazo Kiingereza na Luganda hazikuhitajika au hazikuwezekana kutumiwa.

Kadri wasomi na wataalamu wa lugha wanapojitahidi kurasmisha shughuli za Tume ya Kiswahili Afrika Mashariki (EAKC), matumizi ya Kiswahili nchini Uganda sawa na hali ilivyo katika maeneo mengi ya Rwanda, yalishika kasi baada ya kuondolewa madarakani kwa Idd Amin Dada na kuingia madarakani kwa Rais Yoweri Kaguta Museveni ambaye aliishi Tanzania kwa miaka kadhaa na kuipata elimu yake ya Chuo Kikuu huko.